Mataifa makubwa yataka serikali ya wote Afghanistan
23 Septemba 2021Msimamo huo umefikiwa baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi wa nchi hizo ulioitishwa na Uingereza na kufanyika pembezoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea mjini New York.
Mawaziri wa Marekani, Urusi, Ufaransa na Uingereza walikutana uso kwa uso mjini New York, wakiungana kwa njia ya video na mwenzao wa China. Nchi hizo tano zina viti vya kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na kura ya turufu.
Soma zaidi: Taliban wataka kuzungumza katika baraza la Umoja wa Mataifa
Maafisa wa Marekani wamesema mkutano wa mawaziri hao ulioitishwa na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Liz Truss ulikuwa wenye mafanikio, ambapo washiriki walikubaliana kuhusu masuala mengi, likiwemo la matumaini kuwa Taliban wataheshimu haki za wanawake na wasichana.
Hakuna anayeafikiana na Taliban juu ya muundo wa serikali yake
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hadhani kuna upande wowote unaoridhishwa na muundo wa baraza la mawaziri la Afghanistan lililotangazwa na Taliban.
Akizungumza baada ya mkutano wa mawaziri hao, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres nchi zilizowakilishwa zinataka Afghanistan yenye amani, ambako msaada wa kibanadamu unaweza kusambazwa bila bugudha wala ubaguzi. Guterres amesema kwa wakati huu ni vigumu kuelewa vizuri kinachoendelea Afghanistan.
''Kitu kimoja kilicho dhahiri kwangu kwa sasa, ni kwamba Afghanistan haitabiliki. Tunashuhudia mvutano wa kimadaraka miongoni mwa viongozi wa Taliban, na tunaona mienendo isiyofanana katika maeneo tofauti ya nchi hiyo,'' amesema Guterres.
Soma zaidi: Wito watolewa kwa EU kuongeza msaada nchini Afghanistan
China na Urusi ziliuelezea ushindi wa Taliban mwezi uliopita kuwa ni kushindwa kwa Marekani na ziliamua kufanya kazi na kundi hilo, lakini hadi sasa hazijachukua hatua ya kuitambua serikali yake inayojumuisha watu ambao jumuiya ya kimataifa inawachukulia kama wahalifu.
China iko chonjo na kitisho cha ugaidi kutoka Afghanistan
Siku za nyuma China iliikosoa Marekani kwa kushikilia mabilioni ya dola ya Afghanistan, lakini China hiyo hiyo inafuatilia kwa karibu kuhakikisha nchi hiyo ambayo ni jirani yake haigeuzwi kituo cha makundi yenye misimamo mikali.
Soma zaidi: Msuguano waongezeka kati ya pande mbili za uongozi wa Taliban
Hali ya Afghanistan haikuangaziwa tu na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwani hata kundi la nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani zimefanya mkutano kwa njia ya video, zikialika pia baadhi ya nchi nyingine zisizo wanachama wa kundi hilo, kama Qatar ambayo ni makao ya wanadiplomasia wa Taliban.
Katika mkutano huo, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema ukweli kwamba serikali ya Taliban imewatenga wanawake na kuwajumuisha washukiwa wa ugaidi, ni kosa kubwa la kimkakati ambalo linazizuia nchi nyingine kushirikiana na watawala hao wapya wa Afghanistan.
afpe, ebu