1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa masikini kuanza kupelekewa chanjo dhidi ya COVID-19

16 Februari 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO hapo jana limeridhia chanjo dhidi ya virusi vya corona ya AstraZeneca kuanza kupelekwa kwenye mataifa masikini, baada ya kuithibitisha kwa dharura.

Symbolbild I Erste PFIZER Impfdosen erreichen Kolumbien
Picha: Guillermo Legaria/Getty Images

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO hapo jana limeridhia chanjo dhidi ya virusi vya corona ya AstraZeneca kuanza kupelekwa kwenye mataifa masikini, baada ya kuithibitisha kwa dharura. Mataifa ya kipato cha chini na cha kati yanatarajiwa kupata dozi ya kwanza ya chanjo mwishoni mwa mwezi Februari ikiwa ni sehemu ya mpango wa kimataifa wa mgawanyo wa chanjo, COVAX. 

Shirika hilo linataraji kupeleka dozi milioni 336 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka na hadi bilioni 2 ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba.

Kulikuwa na matarajio kwamba mpango huo wa COVAX ungeanza sambamba na utoaji wa chanjo kwa mataifa tajiri. Hata hivyo, miezi miwili baada ya mataifa hayo kuanza, hakuna chanjo hata moja iliyoanza kutolewa miongoni mwa watu bilioni 2.5 waliopo kwenye mataifa masikini zaidi yapatayo 130.WHO yazilaumu nchi tajiri kwa kujilimbikizia chanjo za COVID-19

COVAX ilisaini makubaliano na wazalishaji kadhaa, lakini ni chanjo za AstraZeneca na BioNTech-Pfizer pekee ambazo zilitarajiwa kuingizwa kwenye mpango huu wa awali.

Taasisi ya Serum ya India ilikubali kuzalisha dozi bilioni 1.1 kwa ajili ya mpango huo. India tayari imeanza kutoa msaada wa chanjo kwa baadhi ya majirani zake.

Chanjo ya BioNTech-Pfizer ni miongoni mwa chanjo zilizoko kwenye awamu ya kwanzaPicha: Valeria Mongelli/ZUMA/picture alliance

COVAX, hadi sasa imefanikiwa kupata ahadi ya dola bilioni 6 lakini itahitaji angalau dola bilioni 2 kwa mwaka huu.

Mpango huo wa COVAX uliozinduliwa na WHO unalenga kuhakikisha upatikanaji wa kimataifa wa chanjo ya virusi vya corona na hasa kwa mataifa masikini.

Mataifa 198 yapo kwenye mpango huo, na baadhi yakiwa yanalipia dozi zao. Mataifa 92 ya kipato cha chini kabisa yanapata chanjo kama msaada tu. Mengi ya mataifa hayo yanaitegemea WHO katika upatikanaji na kuthibitisha chanjo zinazoingizwa nchini mwao.

Katika hatua nyingine mkuu ajaye wa shirika la kimataifa la biashara, WTO Ngozi Okonjo Iweala ameonya dhidi ya kukosekana kwa mshikamano wa kimataifa katika mgawanyo wa chanjo dhidi ya virusi vya corona, akisema hali hiyo inaweza kupunguza kasi ya kukabiliana na janga la COVID-19 na kudhoofisha ukuaji wa uchumi kwa mataifa masikini na hata matajiri.

Hata hivyo ameahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha shirika hilo linafanya kwa sehemu yake kikamilifu katika kupambana na janga hilo.

Alisema "Vipaumbele vyetu ni kuboresha sheria zetu, tunahitaji kuangalia ni nini WTO inaweza kuchangia ili kupata suluhu ya janga hili, tunahitaji kuangalia taratibu zetu, na idara za taasisi. Kuna mengi yanahitajika kufanywa, ndiyo sababu nazungumza juu ya mageuzi ya kina na makubwa. Lakini kwa kweli haitakuwa rahisi."

Amesema, hakuna aliye salama na kukosekana kwa mshikamano katika mgawo wa chanjo hakutasaidia chochote kwa kuwa virusi vinavyojibadilisha navyo vinazidi kushika kasi, na kuongeza kuwa kama baadhi ya nchi hazitapata chanjo itakuwa ni kazi bure.

DW/RTRE

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi