1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa mengi yaendelea kupiga marufuku ndege za Uingereza

21 Desemba 2020

Waziri Mkuu wa Uingereza anatarajiwa kuongoza mkutano wa dharura wakati mataifa kadhaa ya ulaya yakifungia safari za ndege kutoka Uingereza kufuatia aina mpya ya kirusi cha corona ambacho Uingereza inataabika kukidhibiti

London Premierminister Boris Johnson
Picha: Toby Melville/Pool/AP/picture alliance

Boris Johnson amesema kutokana na aina hiyo mpya ya kirusi cha corona amelazimika kuweka masharti magumu hata katika kipindi cha sherehe za krismasi. Kwa upande wake waziri wa afya wa Uingereza Matt Hancock amesema kwa sasa aina hiyo ya kirusi hakidhibitiki lakini wanafanya kila wawezalo kukizuia kusambaa zaidi.

Mwezi Septemba wanasayansi wa Uingereza waligundua aina mpya ya kirusi cha corona wanaochoamini kinaambukiza kwa asilimia 70 na siku ya Ijumaa Idara ya afya ikaijulisha serikali ya Uingereza mara moja baada ya hatari yake kuthibitishwa.

Picha: Tolga Akmen/Getty Images/AFP

Kutokana na hilo Mataifa mengi yameendelea kupiga marufuku ndege kutoka Uingereza kuingia nchini mwao, hatua iliyomlazimu Waziri Mkuu Johnson kupanga mazungumzo na kamati ya dharura mjini London kuhusu suala hilo.

Mataifa kadhaa ya Ulaya tayari yamechukua uamuzi huo wa kupiga marufuku ya ndege pamoja na wasafiri kutoka Uingereza kuingia nchini mwao huku nchi nyengine zaidi zikitarajiwa kuchukua hatua hiyo.

soma zaidi: Ubelgiji na Uholanzi zapiga marufuku ndege kutoka Uingereza

Hong Kong pia imesema ndege kutoka Uingereza zitapigwa marufuku kuingia nchini mwake kuanzia siku ya Jumanne.

Shirika la afya duniani  limetoa wito wa kuchukuliwa mikakati zaidi ya kudhibiti virusi vya corona kote barani ulaya, ambayo hadi sasa watu zaidi ya 500,000 wamekufa kutokana na ugonjwa wa COVID 19.

Ufaransa yafungia bidhaa na wasafiri kutoka Uingereza kuingia nchini mwake

Ufaransa ambayo ni muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa kuingia Uingereza nayo haikuachwa nyuma katika kuchukua mikakati ya kulinda watu wake kutokana na virusi vya corona kwa kupiga marufuku bidhaa na hata wasafiri kutoka Uingereza kuingia nchini humo, huku uholanzi ikisema wasafiri watakaoingia huko kupitia ferry watanyimwa nafasi ya kuingia.

Picha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Marufuku hii inakuja wakati baadhi ya kampuni zikijaribu kuhamisha bidha zao kukiwa kumesalia siku kadhaa tu kabla ya Uingereza kuondoka rasmi katika mifumo ya kibiashara ya Umoja wa Ulaya tarehe 31 Desemba.

soma zaidi: Brexit: Kila upande wamtaka mwenzake alegeze masharti kuhusu swala la uvuvi

Kulingana na msemaji wa shirika la Afya ulimwenguni WHO aliyezungumza na shirika la habari la AFP, Maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kukuwa kwa kasi barani ulaya na mataifa ya bara hilo yanapaswa kuchukua mikakati zaidi ya kuzuwia kusambaa kwa virusi hivyo.

Duru kutoka Ujerumani zinazungumzia marufuku ya safari za ndege kutoka Uingereza huenda ikachukuliwa na wanachama wote 27 wanaounda Umoja wa Ulaya na kwamba mataifa hayo pia yanajadili jibu la pamoja kuhusu kufunga njia nyengine za barabarani, ardhini na reli kutoka na kuingia Uingereza.

soma zaidi: Wenye mzio wadhurika na chanjo ya Pfizer, Uingereza

Lakini licha ya wasiwasi uliopo waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema  waatalamu wa Ulaya wamesema hili linaloendelea halitoathiri nguvu ya chanjo ya corona iliopo kwa sasa.

Huku hayo yakiarifiwa wabunge wa Marekani wamekubaliana kutoa kitita cha dola bilioni 900 zitakazowasaidia wamarekani waliaothirika na virusi vya corona. Fedha hizo pia zitatumika kusambaza chanjo ya corona kote nchini humo na kusaidia katika masuala ya fedha. Bunge la Congress linatarajiwa kuidhinisha mpango katika taifa lililo na midadi ya juu kabisa ya vifo vitokanavyo na covid 19.

Chanzo: Amina Abubakar/afp/reuters/ap

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW