1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mataifa yasitisha misaada kwa Palestina

9 Oktoba 2023

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesema hii leo kwamba inaipitia upya misaada yake yote kwa Palestina yenye thamani ya yuro milioni 691 pamoja na kusimamisha malipo yote mara moja.

Moshi ukifuka katika anga ya jiji la Gaza wakati Israel ilipoishambulia Oktoba 9, 2023.
Moshi ukifuka katika anga ya jiji la Gaza wakati Israel ilipoishambulia Oktoba 9, 2023. Picha: Mahmud Hams/AFP

Umoja wa Ulaya unachukua hatua ya kupitia upya misaada yake kwa Palestina, wakati mapigano yakiendelea kati ya wanamgambo wa Hamas na Israel, huku waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwaonya wanamgambo wa Hamas na kuahidi kuibadilisha Mashariki ya Kati. 

Kamishna wa Umoja wa Ulaya Oliver Varhelyi, anayeshughulikia makazi na upanuzi amesema kupitia ukurasa wa X kwamba hakutakuwa na jambo la kawaida kufuatia uvamizi huo wa Hamas, akisema kiwango cha ugaidi na ukatili dhidi ya Israel pamoja na watu wake sasa kinabadilika.

Wanamgambo wa Hamas waliwaua Waisrael 700 na kuwateka mamia katika uvamizi mkubwa kuwahi kufanyika kwa miaka 50 sasa, tangu vita vya Yom Kippur kati ya Israel na muungano wa mataifa ya Kiarabu ukiongozwa na Misri na Syria kati ya Oktoba 6 hadi 25, 1973.

Soma pia: Baada ya shambulio la Hamas, Netanyahu asema Israel iko vitani

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kukutana kesho

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana kesho kujadiliana juu ya shambulizi la kushtukiza la wanamgambo wa Hamas nchini Israel. Mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya Josep Borrell ameandika kupitia ukurasa wa X kwamba kesho ataitisha mkutano wa dharura wa mawaziri hao ili kushughulikia hali nchini Israel na ukanda mzima.

Mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya Josep Borrell amesema anaitisha mkutano na mawaziri wa mambo ya kigeni kuangazia hatua zaidi za kuchukuaPicha: Denis Doyle/Getty Images

Mawaziri hao watakutana kuangazia namna ya kushughulikia shambulizi hilo na hatua zitakazofuata ikiwa ni pamoja na hiyo ya kuangazia upya msaada wa maendeleo na kulingana na msemaji wa Borrell, Peter Stano, kwa sasa wanafanya tathmini ya namna matukio haya ya karibuni yanavyoweza kuathiri msaada huo kwa sasa na siku za usoni.

"Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yamesema wazi kabisa katika kujibu mashambulizi ya kutisha na ya kiholela ya Hamas dhidi ya Israel ya kwamba Israel ina haki ya kujilinda kwa kuzingatia sheria ya kimataifa" alisema Stano.

Umoja wa Ulaya unasaidia huduma muhimu zaidi kwa Wapalestina na kutoa michango ya moja kwa moja kwa serikali ya Mamlaka ya Palestina. Mawaziri hao watakutana Muscat, Oman ambako Umoja wa Ulaya na Baraza la Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba, GCC walikuwa wanakutana na kwa mwaka 2021 hadi 2024 ilipanga kuipatia yuro bilioni 1.18.

Netanyahu awaonya Hamas na kuapa kuibadilisha Mashariki ya Kati

Huku hayo yakiendelea, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa hii leo kuibadilisha Mashariki ya Kati katikati ya vita kati yao na Hamas. Netanyahu amenukuliwa Hamas itakabiliwa na hali ngumu na ya kutisha na kuongeza kuwa wataibadilisha Mashariki ya Kati.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwakabili vilivyo wanamgambo wa Hamas baada ya shambulizi dhidi ya IsraelPicha: Abir Sultan/Pool via REUTERS

Netanyahu amewaambia maafisa wake kusini mwa taifa hilo, ambako wanamgambo wa hamas walifanya mashambulizi ya kushtukiza siku ya Jumamosi.

Hadi hii leo, watu 560 wamekufa katika Ukanda wa Gaza wakati Israel ikiendelea kuishambulia kwa siku ya tazu mfululizo.

Marekani imearifu mchana wa leo kwamba raia wake 9 wameuawa na wengine hawajulikani walipo, kufuatia shambulizi hilo la Jumamosi, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nje Matthew Miller. Amesema wanashirikiana na washirika wao wa Israel ili kujua waliko raia hao. Msemaji wa Usalama wa taifa pia amethibitsiah idadi hiyo.

Soma pia:Nchi nyingi wanachama wa Baraza la Usalama la UN zimelaani mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel 

Huko mjini Geneva, Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa limekuwa na dakika moja ya ukimya ya kuwakumbuka waliouawa kwenye mzozo huo. Balozi wa Marekani Michelle Taylor aliliomba Baraza hilo kuwa na dakika moja ya ukimya na kusisitiza kwamba maisha ya watu wasio na hatia yamepotea kote Israel na Gaza.

Taylor amelaani mashambulizi hayo mabaya kabisa akiyataja kuwa ni janga lililosababisha vifo vya raia wasio na hatia na kulaani vikali matukio yote ya ugaidi.

Na mjini Berlin, Ujerumani imetangaza kusitisha kwa muda msaada ya maendeleo kwa maeneo ya Palestina na kusema wizara yake ya uchumi na maendeleo itapitia kwa kina mchakato wa msaada wa kifedha.

Soma pia: Miito ya mataifa imeanzia kuiunga mkono Israel na kulaani vikali mashambulizi ya Palestina, huku wengine wakiipongeza Hamas

Pamoja na Berlin, Austria pia imesitisha msaada wenye thamani wa yuro milioni 19 kwenye maeneo ya Palestina kwa sasa, hii ikiwa ni kulingana na waziri wa mambo ya nje, Alexander Schallenberg.

Jeshi la Israel aidha mchana wa leo limesema limewaua watu wanaodhaniwa kuwa ni wanamgambo walioingia Israel kutokea Lebanon. Jeshi hilo limesema linaendeleza operesheni zake, na kusaidiwa na helikopta wakati vyombo vya habari vikiripoti kusikika milio ya risasi na watu wanaoishi kaskazini mwa Israel waliagizwa kubaki majumbani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW