Mataifa sabaa tajiri kiviwanda yapania kuyaokoa masoko ya fedha
11 Oktoba 2008Washington:
Mataifa sabaa tajiri zaidi kiviwanda yanaandaa mpango wa vitendo wa kuepukana na balaa la kuenea mzozo wa fedha.Mawaziri wa fedha na wakuu wa benki kutoka mataifa sabaa tajiri zaidi kiviwanda wamekubaliana mjini Washington,kuhusu mpango huo wa vifungu vitano kwa lengo la kuzihifadhi benki kubwa kubwa zisifilisike na kutengwa fedha za serikali ili kugharimia mikopo.Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Peer Steinbrück amezungumzia juu ya "ishara bayana" iliyotolewa.Amedokeza hata serikali kuu ya Ujerumani itachangia katika mpango huo wa kuzinusuru benki. Waziri mwenzake wa Marekani Henry Paulson amesema baada ya mkutano huo mjini Washington,viongozi wa Marekani wataanza hivi karibuni kununua hisa za benki zilizo hatarini.Mawaziri wa fedha na wakuu wa benki wamekutana mjini Washington baada ya mipango ya serikali tofauti ya kumimina mafedha na kupunguza viwango vya riba kushindwa kutuliza hali ya mambo katika masoko ya hisa.