1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya EU yaidhinisha mkataba na Uingereza

28 Desemba 2020

Mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya yameidhinisha siku ya Jumatatu utekekelezaji wa makubaliano ya biashara na Uingereza kuanzia Januari Mosi.

Brüssel | Boris Johnson trifft Ursula von Der Leyen
Picha: Avalon/Photoshot/picture alliance

Mabalozi kutoka mataifa hayo wameidhinisha makubaliano hayo mjini Brussels, wakitumia utaratibu utakaoanza kutumika majira ya tisa za usiku siku ya Jumanne, na kuruhusu kuendelea kwa biashara huru na Uingereza baada ya kuondoka katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya mwanzoni mwa mwaka mpya.

Sebastian Fischer, msemaji wa urais wa Ujerumani wa Umoja wa Ulaya, amesema mabalozi wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha kwa kauli moja utekelezaji wa muda wa makubaliano ya biashara na ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza.

Soma pia:Maoni: Licha ya kufikiwa makubaliano kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, BREXIT bado ni hadaa. 

Hatua ya mataifa wanachama kuidhinisha mpango huo inauruhusu kuanza kutekelezwa katika wakati kabla ya kuvurugwa kwa biashara kati ya pande mbili.

Lakini makubaliano hayo bado yanahitaji kuridhiwa na bunge la Ulaya, yumkini mwishoni mwa mwezi Februari. Bunge la Uingereza linatarajiwa kuyaidhinisha siku ya Jumatano.

Mpinzani wa Brexit akionesha bendera za Umoja wa Ulaya karibu na majengo ya bunge la Uingereza mjini London, Januari 30, 2020. Uingereza iliondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya Januari 31, 2020.Picha: Tolga Akmen/AFP/Getty Images

Serikali ya Uingereza imezionya kampuni kuwa tayari kwa uvurugaji wowote na nyakati ngumu wakati sheria hizo zitakapoanza kutekeleza usiku wa Jumanne.

Kampuni zimekuwa zikipambana kuyaelewa kwa kina na kujua athari za makubaliano hayo yenye kurasa 1,240, yaliofikiwa na Umoja wa Ulaya na Uingereza katika siku ya mkesha wa Krismas.

Soma pia: Mkataba wa baada ya Brexit kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya wapatikana

Makubaliano hayo yaliosainiwa baada ya miezi tisa ya majadiliano makali, yatahakikisha kuwa Uingereza na kanda ya Umoja wa Ulaya yenye wanachama 27, wanaweza kuendelea kufanya biashara bila kuwepo na ushuru au ukomo.

Hilo litasaidia kulinda kiasi cha pauni bilioni 660 katika biashara ya kila mwaka kati ya pande hizo mbili, na mamia kwa maelfu ya ajira zinazotegemea biashara hiyo.

Usumbufu na misukosuko bado vinatarajiwa

Lakini mwisho wa uanachama wa Uingereza katika soko kubwa la pamoja la Umoja wa Ulaya na umoja wa forodha, bado vitaleta usumbufu na gharama mpya kwa watu na pia biashara.

Soma pia: Von der Leyen: Mianya mikubwa ingalipo kuhusu Brexit

''Nadhani biashara kwa sehemu kubwa iko katika nafasi nzuri. Lakini bila shaka, panapokuwa na mabadiliko yoyote, kipindi chochote cha mpito, kunakuwa na nyakati za misukosuko ya hapa na pale na hicho ndicho serikali yetu ipo kuzisaidia biashara kuwa tayari,'' alisema waziri wa maandalizi ya Brexit wa Uingereza Michael Gove.

Mchoro uliohamaishwa na mchakato wa Brexit ukiashiria kuondoka kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Uingereza itaondoka katika umoja wa forodha na soko la pamoja la Umoja wa Ulaya usiku wa manane, Desemba 31, 2020.Picha: Gareth Fuller/empics/picture alliance

Serikali ya kihafidhiina na waziri mkuu Boris Johnson inahoji kwamba uvurugaji wowote wa muda mfupi kutokana na Brexit utakuwa unastahili, kwa sababu Uingereza sasa itakuwa huru kutunga sheria zake yenyewe na kuingia makubaliano mapya ya biashara na mataifa na kanda mbalimbali duniani.

Soma pia: Barnier: Mazungumzo ya Brexit yanaelekea pazuri

Hata hivyo wavuvi wa Uingereza wamelalamikia makubaliano hayo na kusema wanahisi wamesalitiwa na serikali ya Johnson, wakisema wamepata sehemu ndogo tu ya kile ilichowaahidi kupitia Brexit.

Uingereza iliondoka katika Umoja wa Ulaya karibu mwaka mmoja uliyopita, lakini iliendelea kuwa sehemu ya kanda ya kiuchumi ya umoja huo wakati wa kipindi cha mpito ambacho kitamalizika saa sita za usiku kwa saa za Brussels, sawa na saa tano usiku kwa saa za London, Desemba 31.

Chanzo: Mashirika

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW