1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya G7 yajadili kupambana na China kiuwekezaji

12 Juni 2021

Katika siku ya pili ya mkutano wa G7, viongozi wanatarajiwa kujadili majanga ya kiafya, mabadiliko ya tabianchi, kushughulikia mpango wa upanuzi wa China pamoja na mzozo wa kidiplomasia na Uingereza unaotokana na Brexit.

UK G7 2021 Cornwall | Biden, Merkel und Jan Hecker
Picha: Guido Bergmann/Bundesregierung/REUTERS

Kundi la mataifa saba tajiri yaliyoendelea zaidi kiviwanda la G7 linapanga

mpango mkubwa wa miundombinu wa kuwekeza katika nchi maskini ili kuweza kupambana na mpango wa kibiashara wa China ujulikanao maarufu kama "Barabara ya Hariri".

Soma zaidi: Mkutano wa G7 waanza nchini Uingereza

Maafisa wa Marekani wametangaza mpango huo Jumamosi, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa siku tatu wa G7, unaofanyika katika kijiji cha pwani Uingereza.

Kuna pengo la miundombinu linalohitaji dola trilioni 40 katika baadhi ya sehemu ulimwenguni, na mpango huo mpya unakusudiwa kuzisaidia nchi hizo, wamesema maafisa hao.

Mpango huo uliopewa jina la "Jenga Tena Ulimwengu Bora", unatarajiwa

kujadiliwa kwenye mazungumzo ya Jumapili ya viongozi hao.

Ingawa hakuna ahadi za kifedha zilizotolewa hadi hivi sasa, maafisa wamesema Marekani, mshirika wa G7, sekta binafsi na wadau wengine watakusanya mamia ya mabilioni kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya miundombinu katika nchi zenye kipato cha chini na cha wastani.

Maafisa hao wanaukosoa mpango wa China kwa kukosa uwazi, na kuwa na viwango vibaya vya kulinda mazingira na vya kazi.

Kupitia mpango huo unaotajwa kuwa na dosari nyingi, China inawekeza kwenye ujenzi wa barabara, njia za reli, bandari na miradi mingine ya miundombinu ili kujenga uhusiano mpya wa biashara na Ulaya, Afrika, Amerika Kusini na Asia.

China inawekeza katika nchi ambazo  vinginevyo ingekuwa vigumu kwao kupata misaada ya kimataifa.

Wakosoaji wanasema mpango huo wa China unazitumbukiza nchi maskini kwenye deni, mtego wa utegemezi wa kisiasa na ujenzi wake mara nyingi huwa ni wa kukwepa sheria za kulinda mazingira. Halikadhalika ni kampuni za Kichina pekee zinazohusishwa katika miradi hiyo ya ujenzi.

Waandamanaji wa kutetea mazingira wafika kwenye mkutano wa G7

Wakati mkutano huo ukiendelea mamia ya watu wameandamana kwa lengo la kuwakumbusha viongozi hao wa G7 pamoja na vyombo vya habari juu ya umuhimu wa kuyalinda mazingira.

Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wenzake kutoka mataifa saba tajiri wanakutana karibu na mji wa St. Ives kwa mazungumzo yanayozingatia janga la maambukizi ya virusi vya corona na mabadiliko ya tabianchi.

Max Lawson, mkuu wa sera wa shirika la misaada la Oxfam, amesmea wanaharakati wanawataka viongozi wa kundi la G-7 la mataifa ya - Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japani, Uingereza na Marekania - kuweka mikakati ya kiwangi kikubwa cha kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kuzifadhili nchi masikini kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

G7 2021 Cornwall | Charles Michel, Ursula von der Leyen na Boris JohnsonPicha: Andrew Parsons/Avalon/Photoshot/picture alliance

Umoja wa Ulaya watishia kuichukulia hatua Uingereza 

Aidha pembezoni mwa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alifanya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, katika wakati ambapo kuna mvutano kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya unaotokana na mtafaruku wa makubaliano ya baada ya Brexit.

Johnson pia amekutana na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pamoja na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel Jumamosi katika hoteli ya mapumziko ya Carbis Bay ambapo viongozi wa G-7 wanakutana.

Soma zaidi: Mawaziri wa Fedha wa nchi za kundi la G7 wakutana jijini London

Pande hizo mbili zimo kwenye mzozo wa kidiplomasia unaozidi kushika kasi kila uchao, kuhusu Ireland ya Kaskazini, eneo pekee la Uingereza lenye mpaka wa ardhini na Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya umekasirishwa na Uingereza  kuchelewesha kuweka vituo vya kukagua bidhaa zinazoingia Ireland ya Kaskazini kutoka maeneo mengine ya Uingereza.

Uingereza inadai kwamba hatua hiyo itadhoofisha biashara na kuhatarisha makubaliano ya amani na Ireland ya Kaskazini yaliyopatikana kwa bidii kubwa.

Mvutano huo pia unampa wasiwasi Rais wa Marekani Joe Biden, juu ya uwezekano wa kuhatarisha maubaliano hayo ya amani ya Ireland ya Kaskazini.

Umoja wa Ulaya unatishia kuichukulia Uingereza hatua za kisheria iwapo kuanzia mwezi ujao itashindwa kukagua zinazoingia Ireland ya Kaskazini, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku nyama baridi kama vile sausage kutoka Uingereza, Scotland na Wales.

Vyanzo: (ap,rtre, dpa)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW