1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 kuviimarisha vikosi vya anga na majini vya Ukraine.

12 Julai 2023

Rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky aliungana na viongozi wa NATO wakati wa kutolewa tamko la pamoja la mataifa ya G7 kuhusu kuihakikishia Ukraine usalama wa muda mrefu katika mji wa Vilnius, Lithuania.

Litauen Vilnius | NATO-Gipfeltreffen 2023 | Selenskyj spricht zur Presse
Picha: Mindaugas Kulbis/AP Photo/picture alliance

Baraza hilo jipya limeundwa ili kuimarisha ushirikiano kati ya Ukraine na muungano wa mataifa 31 washirika wa kimataifa ambao wametangaza mpango wa muda mrefu wa usalama wa Ukraine.

Kundi la mataifa ya Magharibi yaliyoendelea kiviwanda, G7 yameahidi kutoa msaada wa kijeshi wa muda mrefu kwa Ukraine ili kuisaidia nchi hiyo kupambana na majeshi ya uvamizi ya Urusi na kuzuia kurejea tena vita mara tu vitakapomalizika.

Rais wa Ukraine Volodymir ZelenskyPicha: Ints Kalnins/REUTERS

Nchi hizo wanachama wa G7 zinapanga kuipa Ukraine vifaa vya kisasa kwa ajili ya vikosi vyake vya anga na vya majini. Mataifa ya G7 tayari yametoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine, hasa vifaa vinavyotumiwa na vikosi vya nchi kavu ingawa ndege za kivita au meli za kivita hadi sasa bado hazijawasilishwa.

Soma:NATO yashindwa kutoa mwaliko rasmi wa uanachama kwa Ukraine

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema ahadi za usalama wa Ukraine zilizotolewa na nchi kadhaa ndani ya mfumo wa G7 zinakusudiwa kuwa sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuisaidia Ukraine. Scholz ameyasema hayo pembezoni mwa mkutano wa kilele wa NATO katika mji wa Vilnius.

Ujerumani, Marekani, Ufaransa, Italia, Uingereza, Japan, na Canada zinaunda kundi hilo la mataifa ya Magharibi yaliyoendelea kiviwanda.

Katika mkutano wa kilele wa viongozi wa NATO mjini Vilnius, viongozi hao wamekubaliana juu ya malengo kuhusu matumizi ya kijeshi hata hivyo maswali kuhusu mtoaji mkuu katika muungano huo, Poland yanaangazia ugumu wa matumizi ya fedha ipasavyo katika jumuiya hiyo.

Mkutano wa Baraza jipya la NATO/Ukraine katika mji wa Vilnius, Litrhuania.Picha: Aytac Unal/AA/picture alliance

Poland ilipanda kileleni mwa chati ya matumizi ya NATO katika mwaka huu, utabiri wa hivi punde wa muungano huo unaonyesha nchi hiyo inatumia asilimia 3.9 ya pato lake la taifa katika malengo ya kijeshi, hiyo ni karibu ya mara mbili ya lengo la sasa la NATO la uchangiaji wa asilimia 2.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema maamuzi yaliyofikiwa yanaashiria mwanzo wa sura mpya ya uhusiano kati ya NATO na Ukraine.

Soma:Zelensky akasirishwa na NATO kusuasua kuikubali Ukraine

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepongeza ahadi mpya ya nchi yake kupewa silaha na vifaa vya kupambana na uvamizi wa Urusi. Amesema ahadi hizo zitakuwa ni mafanikio muhimu sana n.a NATO.

Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Kwa upande wake urusi imesema ahadi hizo kwa ajili ya usalama wa muda mrefu zilizootolewa na nchi za G7 kwa Ukraine ni tishio kwa usalama wa Urusi.

Vyanzo: AFP/DPA/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW