1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya G7 yaungana kujadili vitisho vya ulimwengu

4 Mei 2021

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la nchi  zilizoendelea zaidi kiviwanda, G7 wanaendelea leo na mkutano wa siku mbili mjini London,  ukiwa ni wa kwanza wa ana kwa ana baada ya zaidi ya miaka miwili.

England | G7 Treffen der Außenminister in London: Heiko Maas und Dominic Raab
Picha: Ben Stansall/AP/picture alliance

Mkutano huo ambao unatarajiwa kutoa majawabu kwa changamoto ya kiafya ya ulimwengu, ustawi wa mataifa yao pamoja na demokrasia kwa upana wake.

Taifa mwenyeji, Uingereza limeonya juu ya kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji vya Urusi, China na Iran. Mataifa hayo kwa namna tofauti yanaonekana kusababisha changamoto katika mustakabali wa ufanikishwaji wa demokrasia na utawala wa sheria duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Diminic Raab amesema urais wa Uingereza wa mataifa ya G7, unakuwa nafasi muhimu kuyaleta pamoja masuala muhimu kama ya kidemokrasia na pia kuonesha umoja katika muda huu ambao unahitajika sana katika kukabiliana changamoto wanazokabiliana nazo kwa pamoja sambamba na kuongezeka kwa vitisho mbalimbali.

Mzozo wa jimbo la Tigray la Ethiopia kujadiliwa.

Wakimbizi wa Ethiopia wakiwa kambini nchini SudanPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Wanadiplomasia hao wa ngazi ya juu kutoka Uingereza, Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Japan wanakutana kwa siku mbili kwa kujadili ajenda kadhaa miongoni mwa hizo ni mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar, mgogoro ya jimbo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray, hali ya usalama ya Afghanistan, ambako jeshi la Marekani na washirika wake wa Umoja wa Kujihami wa NATO wanahitisha jukumu la uwepo wao katika ardhi ya taifa hilo ulidumu kwa takribani miongo miwili.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema kundi la mataifa hayo ya G7vilevile litavijadili vitendo kadhaa vya vurugu za Urusi kikiwemo cha kukusanya wanajeshi wake katika mpaka wa taifa lake na Ukraine, sambamba na kufungwa kwa mkosoaji wa serikali ya Rais Vladimr Putin Alexei Navalny.

Mjadala wa kutawanya chango katika maeneo yote ya ulimwengu.

Mataifa hayo yenye nguvu ya uchumi wa kiviwanda yataaangaliwa uwezekano wa kufanikisha upatikanaji wa chango ya virusi vya corona katika maeneo yote ya ulimwengu. Kimsingi mataifa mengi tajiri yamekuwa yakisita kutoa akiba yake ya chanjo kwa wengine ili kwanza wafanikishe zoezi hilo kwa raia wao.

Katika mkutano huu wa siku mbili wa ana kwa ana wa London waandaaji wamechukua hatua madhubuti ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona ikiwemo kwa kuweka kizuizi cha plastiki baina ya mtu na mtu ambayo, inamwezesha kuona upande mwingine, ikiwa pia kuwepo na kipimo cha vurusi vya corona cha papo kwa papo.

Katika mkutano huu Uingerea kama taifa mwenyeji umewaalika mawaziri wakuu wengine kutoka mataifa ya Australia, India, Korea Kusini, Afrika Kusini. Kufanyika kwa mkutano huo kutatoa nguvu ya kimkakati kuelekea mkutano wa kilele wa mataifa hayo unaotarajiwa nchini Uingereza mwezi Juni.

Chanzo: AP