Mataifa ya Ghuba yaitaka UN kutumia nguvu kuilinda Hormuz
3 Aprili 2026
Kiongozi wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) alitoa wito siku ya Alhamisi kwa Umoja wa Mataifa kuidhinisha matumizi ya nguvu kulinda Mlango-Bahari wa Hormuz dhidi ya mashambulizi ya Iran, siku moja kabla ya kura muhimu ya Baraza la Usalama.
Iran imekaza udhibiti kwenye njia hiyo muhimu ya usafirishaji, hatua inayotishia upatikanaji wa mafuta na kuyumbisha uchumi wa dunia, ikiwa ni kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyoanzisha vita ya Mashariki ya Kati iliyodumu mwezi mmoja sasa.
Katibu Mkuu wa GCC, Jasem Mohamed AlBudaiwi, alisema Iran imefunga njia hiyo, kuzuia meli za biashara na meli za mafuta kupita, na kuweka masharti kwa baadhi ya meli zinazoruhusiwa kupita.
Akizungumza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, AlBudaiwi alilitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua za haraka kulinda njia za baharini na kuhakikisha usafiri wa kimataifa unaendelea kwa usalama.
Bahrain ambayo inashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi wa Aprili, imependekeza azimio linaloruhusu mataifa kutumia nguvu kuhakikisha uhuru wa kupita katika mlango huo, lakini pendekezo hilo limegawanya wanachama wa Baraza la Usalama.
China, Urusi na Ufaransa zimepinga matumizi ya nguvu, zikisisitiza kuwa suluhisho la kisiasa ndilo njia bora ya kumaliza mgogoro huo. China ilionya kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza mvutano na kusababisha madhara makubwa zaidi, huku Urusi ikikataa kuunga mkono kile ilichokiita hatua za upande mmoja. Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, pia amesema operesheni ya kijeshi kufungua njia hiyo siyo halisi.
Rasimu mpya ya azimio sasa inaruhusu matumizi ya "njia zote za kujilinda” badala ya matumizi ya nguvu moja kwa moja. Kura ya uamuzi inatarajiwa kupigwa Ijumaa, huku Bahrain ikisema kupitishwa kwake kutaonyesha umoja wa kimataifa katika kulinda njia muhimu ya biashara na nishati duniani.
Kwa kawaida, karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia hupitia katika Mlango-Bahari wa Hormuz, lakini kufungwa kwake kumepunguza sana usambazaji na kusababisha kupanda kwa bei za nishati duniani.
Zelenskiy atoa utaalamu wa Ukraine kusaidia
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alitoa pendekezo la kushirikisha utaalamu wa nchi yake katika usalama wa baharini ili kusaidia kuifungua Hormuz wakati wa mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
Alisema Waziri wa Mambo ya Nje Andrii Sybiha alishiriki katika mkutano wa mataifa takriban 40 kujadili namna ya kufungua upya njia hiyo muhimu.
Zelenskiy alisisitiza kuwa Ukraine ina uzoefu mkubwa wa kulinda njia za majini, hasa kutokana na mafanikio yake katika Bahari Nyeusi, ikiwemo matumizi ya droni za majini zilizosaidia kukabiliana na meli za Urusi.
Aliongeza kuwa Ukraine iko tayari kusaidia washirika wake kwa kutumia utaalamu, teknolojia na uzoefu wake wa kivita. Pia inaendeleza ushirikiano wa kiulinzi na nchi za Mashariki ya Kati, ikiwemo Saudi Arabia, UAE, Qatar na Jordan, huku mazungumzo yakiendelea na Bahrain, Kuwait, Iraq na Uturuki.
Iran yaendeleza mashambulizi licha ya kauli za Trump
Iran ilirusha makombora zaidi kuelekea Israel na nchi za Ghuba, ikionyesha kuwa bado ina uwezo wa kijeshi licha ya madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba tishio lake limepungua.
Udhibiti wa Iran juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz umevuruga usambazaji wa nishati duniani na kuwa faida yake kubwa ya kimkakati katika vita hii.
Uingereza imeongoza juhudi za kidiplomasia za kujadili namna ya kufungua njia hiyo baada ya vita. Trump amesema mlango huo unaweza kufunguliwa kwa nguvu, lakini si jukumu la Marekani kufanya hivyo, akizihimiza nchi zinazotegemea mafuta kuchukua hatua.
Kabla ya vita, karibu asilimia 20 ya mafuta ya dunia yalipitia njia hiyo.
Mashambulizi yaliendelea pia ndani ya Iran, ambapo daraja la B1, linalotajwa kubwa refu zaidi katika Mashariki ya Kati, lilishambuliwa na kusababisha vifo vya watu wanane na majeruhi 95. Iran imekosoa mashambulizi hayo, ikisema kulenga miundombinu ya kiraia kunaonyesha kushindwa kwa maadui wake.
Mabadiliko ya ghafla ndani ya Pentagon
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amemuomba Jenerali Randy George kujiuzulu na kustaafu mapema, katika hatua inayoongeza mabadiliko makubwa ndani ya Pentagon.
George, aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu tangu 2023, anaungana na orodha ya maafisa wakuu waliotimuliwa huku Hegseth akitekeleza ajenda ya usalama ya Trump.
Ufaransa yapiga marufuku mkusanyiko wa Waislamu
Ufaransa imepiga marufuku mkusanyiko wa Waislamu uliopangwa kufanyika karibu na Paris kutokana na sababu za kiusalama.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa maelekezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani Laurent Nunez, kufuatia kuongezeka kwa tahadhari za ugaidi baada ya jaribio la shambulio la bomu kuzuiwa katika ofisi za Banki ya Amerika.
Masoko ya hisa yapanda huku mafuta yakivuka $110
Masoko ya hisa yalifunga siku ya Alhamisi kwa faida ndogo, yakirekodi wiki ya kwanza yenye mafanikio tangu vita ianze, licha ya msukosuko uliosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta.
Bei ya mafuta ya Marekani ilifikia dola 111.54 kwa pipa, huku bei ya mafuta ghafi ya Brent ikizidi dola 109. Kupanda huku kunahusishwa na usumbufu wa usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hisa za kampuni ya magari ya Tesla zilishuka zaidi ya asilimia 5, huku kampuni za usafiri pia zikikumbwa na hasara.
Wataalamu wanaonya kuwa mfumuko wa bei unaweza kuongezeka zaidi, jambo linalopunguza matumaini ya kupunguzwa kwa viwango vya riba. Kwa ujumla, vita hii imeendelea kuwa chanzo kikuu cha kuyumba kwa uchumi wa dunia.