1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ghuba yapinga matamshi ya "kuudhalilisha Uislamu"

6 Juni 2022

Chama tawala cha India BJP kimemsimamisha kazi msemaji wake Nupur Sharma kufuatia kauli aliyoitoa wakati wa mdahalo wa runinga kuhusu mtume Mohammed wakati nchi kadhaa za kiislamu duniani zikiitaka India kuomba radhi.

Nupur Sharma
Msemaji wa chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi Sharma NupurPicha: Saumya Khandelwal/Hindustan Times/imago

Chama tawala cha India ambacho kimekuwa kikishtumiwa mara kwa mara kwa ukiukaji wa haki za waislamu walio wachache nchini humo, kupitia taarifa kwenye tovuti yake, kimesema kinaheshimu dini zote na kwamba kinalaani vikali matusi dhidi ya mtu wa dini yoyote.

Msemaji wa chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi Sharma Nupur, aliandika katika mtandao wake wa Twitter kuwa, kauli yake ilikuwa ni jibu kwa kile alichokiita "matusi" dhidi ya mungu wa Kihindu Shiva lakini haikuwa nia yake kuumiza hisia za kidini za mtu yeyote.

Bi Sharma amesema, "Ikiwa maneno yangu yamemkwaza mtu au kuumiza hisia za kidini za mtu yeyote kwa namna yoyote ile, naiondoa kauli yangu bila masharti."

Soma pia: Mzozo kuhusu zuio la kuvaa hijab India waongezeka

Chama hicho kimeongeza kuwa, msemaji mwengine wa BJB Naveen Jindal pia amefukuzwa chamani kufuatia kauli aliyoitoa kuhusu uislamu kwenye mitandaoni ya kijamii.

Jindal aliandika kwenye Twitter kuwa, alikuwa na maswali juu ya matamshi yaliyotolewa juu ya miungu ya Kihindu. Chama hicho tawala kimesema kupitia taarifa, "Chama cha Bharatiya Janata kinapinga itikadi yoyote inayomtukana au kumdhalilisha mtu kwa misingi ya madhehebu au dini. Chama chetu hakiungi mkono watu kama hao au falsafa hizo." 

Nchi za kiislamu zikiwemo Qatar, Kuwait, Pakistan na Saudi Arabia zimeshtumu kauli zilizotolewa na maafisa hao wa ngazi ya juu wa chama tawala cha India juu ya mtume Mohammed kwa kuziita kauli hizo "chuki dhidi ya uislamu."

Nchi kadhaa za kiislamu duniani zaitaka India kuomba radhi 

Picha: Anushree Fadnavis/REUTERS

Kauli ya msemaji wa chama cha Waziri Mkuu Narenda Modi wiki iliyopita imelaumiwa kwa kuchochea ghasia huku miito ya kumtaka msemaji huo kukamatwa ikitolewa. Kauli hiyo pia imeibua hasira katika nyengine za kiislamu duniani.

Saudi Arabia kupitia taarifa ya wizara ya mambo ya nje imesema kauli ya msemaji huyo ni kama matusi na imetaka kuheshimiwa kwa imani na dini zote. Qatar pia imeitaka India kuomba radhi kwa kauli za chuki dhidi ya uislamu katika wakati ambapo makamu wa rais wa India Venkaiah Naidu anafanya ziara katika nchi hiyo tajiri ya ghuba kwa nia ya kuimarisha uhusiano wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Soma pia:Miili kadhaa yagunduliwa kwenye mto India

Balozi wa India mjini Doha Deepak Mittal, aliagizwa kufika kwenye wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo katika siku ya pili ya ziara ya Naidu na wafanyibiashara wengine wakubwa kutoka India.

Balozi huyo alikabidhiwa barua rasmi ya malalamiko ambayo Qatar imesema inataraji serikali ya India itaomba radhi kwa umma.

Kumeibuka miito kwenye mitandao ya kijamii hasa kutoka kwa mataifa ya ghuba kususia bidhaa za India katika nchi hizo za kiislamu.

Hata hivyo India haikutoa jibu mara moja lakini ubalozi wake mjini Doha ulitoa taarifa ikisema hatua kali imechukuliwa dhidi ya wahusika waliotoa kauli hizo dhidi ya uislamu. Ubalozi huo haukotoa maelezo zaidi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW