1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Kiarabu yatazamia biashara ya Marekani

12 Mei 2025

Rais wa Marekani Donald Trump anazuru Saudi Arabia, Qatar na UAE kuanzia Mei 13 hadi 16. Mataifa hayo yanatazamia kuimarisha kuimarisha ushirikiano na Marekani katikati mwa mivutano kuhusu Gaza, Israel na Iran.

Rais wa Marekani Donald Trump
Trump ameahidi kutoa tangazo kubwa wakati wa ziara yake ya Mashariki ya Kati.Picha: Saul Loeb/AFP

Kabla ya ziara rasmi ya kwanza ya Rais wa Marekani Donald Trump nje ya nchi ambayo imepangwa kufanyika kati ya Mei 13-16, tayari ametangaza zawadi yake ya ukarimu kwa nchi mwenyeji — Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, Trump ataanza kutumia jina "Ghuba ya Kiarabu" (Arabian Gulf) au "Ghuba ya Arabia" badala ya "Ghuba ya Uajemi" (Persian Gulf), jina linalohusishwa kihistoria na Iran ya kisasa. Ghuba hii ipo mashariki mwa nchi za Ghuba na Saudi Arabia, na kusini mwa Iran.

Ingawa Trump hana mamlaka ya kubadilisha rasmi jina la ghuba hiyo, hatua hiyo ina ishara kubwa ya kisiasa. Nchi za Kiarabu zimekuwa zikitaka jina libadilishwe kwa muda mrefu, huku Iran ikisisitiza uhusiano wake wa kihistoria na eneo hilo.

Trump pia ameahidi tangazo "kubwa sana” wakati wa ziara yake ya Mashariki ya Kati.

"Itakuwa moja ya matangazo muhimu zaidi yaliyotolewa kwa miaka mingi kuhusu mada fulani ya maana sana,” Trump alisema bila kufafanua zaidi.

Matumaini na wasiwasi wa Waarabu

"Kila moja ya nchi anazotembelea – Saudi Arabia, Qatar na UAE – ina vipaumbele vya kisera kwa Rais Trump,” alisema Burcu Ozcelik, mtafiti mwandamizi wa taasisi ya RUSI yenye makao mjini London.

"Riyadh inahitaji uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni ili kufanikisha malengo ya mageuzi ya Vision 2030 na haitaki kubaki nyuma ya fursa zilizopatikana na UAE kupitia makubaliano ya Abraham [makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani ya kurejesha uhusiano kati ya Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu],” alisema.

Trump amekuwa na uhusiano wa karibu na mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman tangu muhula wake wa kwanza.Picha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Kabla ya shambulizi la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023 na vita vilivyofuata huko Gaza, Saudi Arabia ilikuwa karibu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel. Makubaliano hayo yaliyochochewa na Marekani yangekuwa karibu na muundo wa makubaliano ya pande tatu, ambapo Marekani ingetoa dhamana ya usalama kwa Saudi Arabia na kusaidia mpango wa nyuklia wa kiraia wa Saudi Arabia.

Soma pia:Mataifa ya Kiarabu yasaka namna ya kumkabili Trump kuhusu Gaza 

Hata hivyo, kwa sasa makubaliano kati ya Saudi Arabia na Israel hayaonekani kuwa karibu kutimia kwani, kwa mujibu wa Ozcelik, "ufalme huo hauwezi kuachana na ‘msimamo wake mkuu' kwamba lazima kuwe na njia ya kuaminika ya kuelekea kwenye taifa la Palestina.”

Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia mjini Washington, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Prince Faisal bin Farhan, alisisitiza alipokuwa Ikulu mwezi Aprili kwamba suala la Israel lisiwe sehemu ya ajenda ya ziara ya Trump.

"Upande wa Saudi unalenga biashara ili kuepuka hali isiyo na faraja,” alisema Emily Tasinato, mtafiti wa Ghuba katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni (ECFR).

Wakati huo huo, kuna viashiria kwamba Riyadh na utawala wa Trump wanakamilisha vipengele vingine vya makubaliano makubwa pasipo kushirikisha mchakato wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Saudi Arabia na Israel.

"Moja ya vipengele hivyo ni mpango wa nyuklia wa kiraia wa Saudi Arabia, ambapo Trump sasa anaonekana tayari kujadili ushirikiano bila kuhitaji ufalme huo kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel,” alisema Tasinato. "Kipengele kingine kinahusu ulinzi, ingawa si kwa mkataba wa ulinzi wenye nguvu kisheria, bali kwa ushirikiano wa kijeshi unaowezekana pasipo makubaliano na Israel.”

Sanam Vakil, Mkurugenzi wa Mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa Chatham House, naye anaamini kwamba mgogoro kati ya Israel na Gaza utaachwa kando wakati wa ziara ya Trump.

Mauaji ya Khashoggi: Trump aweka pesa mbele ya haki za binadamu

01:22

This browser does not support the video element.

"Nchi za Kiarabu zinatarajia ziara ya Trump itachochea ushirikiano wa kiuchumi, na pia italenga kukuza ushirikiano wa usalama wa kikanda kupitia mkutano wa GCC [Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba],” aliambia DW.

Hata hivyo, kwa mtazamo wake, "mkutano huo utakuwa kisingizio cha kutokuwa na maendeleo halisi kuhusu Gaza.”

Ingawa atakuwa katika eneo hilo, Trump hajaandaa mkutano wowote na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

 Kipaumbele kikubwa: Biashara

"Naona biashara kama kipengele muhimu cha kuchambua maslahi katika ziara ya Trump kwenye Ghuba,” anasema Tasinato wa ECFR.

"Wakuu kadhaa wa makampuni ya ulinzi ya Marekani wanatarajiwa kuandamana na Trump katika ziara yake nchini Saudi Arabia,” alisema, akiongeza kuwa "Riyadh, Doha na Abu Dhabi zote zimeahidi uwekezaji mkubwa Marekani kabla ya ziara hiyo.”

"Uongozi wa Saudi Arabia unalenga ushirikiano na makampuni ya Kimarekani, na umeahidi dola bilioni 600 kwa biashara na uwekezaji kwa kipindi cha miaka minne,” alisema.

"Hali ni kama hiyo kwa UAE, inayopanga kuwekeza dola trilioni 1.4 nchini Marekani ndani ya miaka 10 ijayo, kwa kuzingatia miundombinu ya akili bandia na semiconductors,” aliongeza.

Soma pia: Biden kusitisha mauzo ya silaha UAE na Saudi Arabia

Hivi karibuni, mikataba kadhaa ya Marekani ya kuuza ndege na makombora kwa nchi za GCC imetangazwa pia.

"Jukwaa la Uwekezaji la Saudi-US [linalofanyika Riyadh wakati wa ziara ya Trump] linapaswa kuangaliwa katika muktadha huu, kwani Riyadh inataka kupanua sekta yake ya teknolojia kupitia fursa katika data centres, huduma za wingu (cloud computing) na akili bandia miongoni mwa mengine,” alisema Tasinato.

Kabla ya kumaliza muhula wake wa kwanza, Trump alifanikisha makubaliano kati ya UAE na Israel, yanayojulikana kama Makubaliano ya Abraham.Picha: Alex Wong/Getty Images

Je, "tangazo kubwa” linaweza kuwa nini?

Kwa kuzingatia hali ya sasa ya Mashariki ya Kati, tangazo la Trump linaweza kuwa kuhusu mateka wa Hamas walioko Gaza, mpango wa nyuklia wa Iran na Marekani, au kundi la Houthi linaloungwa mkono na Iran nchini Yemen.

"Kwa Trump, litakuwa ushindi mkubwa wa kimaadili na kidiplomasia ikiwa kutafikiwa makubaliano ya kuwaachia mateka wa Hamas kabla au wakati wa ziara yake,” alisema Ozcelik wa RUSI.

Kwa upande wa Tasinato wa ECFR, inaonekana tangazo hilo litaangazia ama mpango wa nyuklia kati ya Marekani na Iran au makubaliano na Wahouthi, waliokubali kusitisha mashambulizi ya meli katika Bahari Nyekundu kupitia upatanishi wa Oman — ingawa bado wanashambulia Israel.

Vyanzo kadhaa vimesema Iran ilishiriki kwa njia chanya katika majadiliano hayo, ishara kuwa inaweza kuwa tayari kusaini makubaliano ya nyuklia na Marekani, ambayo yangesaidia kupunguza vikwazo vya kiuchumi dhidi yake na kuzuia uwezekano wa kushambuliwa kijeshi na Israel.

"Kuna muafaka unaokua kati ya Saudi Arabia na Marekani kuhusu kujumuisha suala la Yemen katika mazungumzo ya nyuklia kati ya Tehran na Washington kama sehemu ya mchakato mpana wa kupunguza mvutano wa kikanda,” alisema Tasinato.

Hatimaye: Ziara yenye faida kwa Marekani

"Rais Trump anatambua fursa za biashara na uwekezaji katika Ghuba, na anataka kuweza kujiondoa Mashariki ya Kati huku Marekani ikielekeza nguvu zake kwa China, kama ilivyo sera ya muda mrefu,” alisema Ozcelik.

"Kujenga uhusiano wa karibu na Saudi Arabia, Qatar na UAE — mataifa ambayo hayakubaliani kikamilifu baina yao, lakini yote yanataka kuwa na ushawishi mkubwa — kunamaanisha kuwa Marekani inaweza kuviamini mataifa haya kushughulikia masuala ya usalama wa kanda,” aliongeza.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW