Mataifa ya Kiarabu yaujadili mgogoro wa Syria
15 Aprili 2023Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka nchi sita za ushirikiano wa nchi za Ghuba ambazo ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Misri, Iraq na Jordan walikutana nchini Saudia kwa mwaliko wa nchi hiyo.
Wamesisitiza "umuhimu wa kuwa na nafasi ya uongozi wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu katika juhudi za kumaliza mgogoro", kulingana na taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Saudia mapema siku ya Jumamosi (15.04.2023).
Pia walijadili "taratibu muhimu za jukumu hili" na kukubaliana kuzidisha "mashauriano kati ya nchi za Kiarabu ili kuhakikisha mafanikio ya juhudi hizi". Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Saudia iliyotolewa Jumamosi, ni kwamba wanadiplomasia wakuu wa mataifa ya Kiarabu "walikubaliana juu ya umuhimu wa kusuluhisha mzozo wa kibinadamu" nchini Syria na kufikia masharti ambayo yataruhusu kurejea kwa wakimbizi.Saudi Arabia kuanzisha mahusiano upya na Syria
Akiungwa mkono na Iran na Urusi, Rais wa Syria Bashar al-Assad alitengwa na nchi nyingi za Mashariki ya Kati na nchi za Magharibi kuhusu vita ambavyo vimeua zaidi ya watu nusu milioni na kulazimisha karibu nusu ya raia wa Syria kukimbia makaazi yao.
Syria ilisimamishwa uanachama kutoka Jumuiya ya nchi za Kiarabu mwaka 2011 kutokana na ukandamizaji wa Rais Assad dhidi ya maandamano ya amani.
Juhudi za Saudia za kupunguza mivutano ya kikanda
Siku ya Jumatano wiki hii, katika ishara ya hivi karibuni ya kupungua kwa mvutano na Damascus, waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal Mekdad aliwasili mjini Jeddah, ikiwa ni ziara ya kwanza kama hiyo tangu vita kuanza. Mekdad na mwenzake wa Saudia walijadili "hatua muhimu" kumaliza kutengwa kwa Damascus.
Mkutano wa Jeddah ni mojawapo ya mipango mingi kufuatia tangazo la kihistoria lililotolewa na China mnamo Machi 10 kwamba Saudi Arabia na Iran zitarejesha tena uhusiano, miaka saba baada ya kuvunjika.
Siku ya Ijumaa, mabadilishano ya karibu wafungwa 900 wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen kati ya waasi wa Kihuthi wanaoungwa mkono na Iran na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia yalianza wakati ndege zilizobeba wafungwa ziliposafiri kati ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi na serikali.
Soma hapa: Saudi Arabia yaukaribisha ujumbe wa Iran na Syria
Balozi wa Saudia nchini Yemen wiki hii alifanya mazungumzo na vikosi vya Kihuthi kwa lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimeshamiri tangu uingiliaji wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uanze mwaka 2015.
Wachambuzi wanasema Saudi Arabia sasa inajaribu kutuliza eneo hilo ili kuliruhusu kuangazia miradi kabambe ya ndani inayolenga kuleta utulivu wa kiuchumi unaotegemea nishati.