1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Mataifa ya Kiislamu yalaani udhibiti wa Ukingo wa Magharibi

9 Februari 2026

Saudi Arabia na mataifa mengine saba ya Kiislamu yamelaani hatua mpya za Israel za kuimarisha udhibiti wa eneo la Ukingo wa Magharibi na kusafisha njia ya kudhibiti makazi zaidi katika eneo hilo la Palestina linalokaliwa

Saudi-Arabia Riyadh 2024 | Erdogan katika mkutano maalum wa OIC na Ushirikiano wa Mataifa ya Kiarabu
Mataifa ya Kiarabu yamelaani vikali hatua ya Israel ya kuyadhibiti zaidi maeneo ya Ukingo wa Magharibi iliyotangazwa Februari, 2026 na kusema haina mamlaka kwenye eneo hilo la PalestinaPicha: Turkish Presidency/Murat Kula/Anadolu/picture alliance

Israel imeidhinisha hatua zilizotangazwa kupitia taarifa ya pamoja ya Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich pamoja na Waziri wa Ulinzi Israel Katz siku ya Jumapili. Hatua hizo zinajumuisha kuwaruhusu Wayahudi wa Israel kununua ardhi Ukingo wa Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Indonesia, Pakistan, Misri na Uturuki yamelaani vikali uamuzi huo haramu wa Israel pamoja na hatua zilizolenga kuharakisha majaribio ya kulinyakua eneo hilo kinyume cha sheria na hatimaye kuwafukuza watu wa Palestina, imesema taarifa ya Saudi Arabia.

Hatua za Israel pia zinalenga kuzinyang'anya manispaa za Palestina mamlaka za utoaji wa vibali vya ujenzi wa makazi katika sehemu za miji ya Palestina, ikiwa ni pamoja na Hebron, na kuzihamishia Israel.

Kulingana na Smotrich, hatua hiyo ilimaanisha kukita mizizi zaidi katika maeneo yote ya ardhi ya Israel na kulifuta kabisa wazo la taifa la Palestina. Ni uamuzi unaochukuliwa siku chache kabla Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hajazuru Marekani atakakokutana na Rais Donald Trump, anayeunga mkono hatua ya taifa hilo ya kupinga uamuzi wa Israel wa Kuunyaku Ukingo wa Magharibi.

Mamlaka ya Palestina imekosa vikali hatua ya Israel ya kuyadhibiti zaidi maeneo ya Ukingo wa Magharibi iliyotangazwa Februari, 2026 Picha: AP

Hatua ya Israel yalaaniwa

Ofisi ya Rais wa Palestina iliyoko Ramallah, ambayo ina udhibiti mdogo kwenye baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi pia ililaani uamuzi huo, ikisema ulilenga "kuimarisha zaidi majaribio ya kuunyakua Ukingo wa Magharibi unaokaliwa", kama Naibu waziri wa Mambo ya Nje Omar Awadallah anavyosema:

Amesema "Tunalaani na tunakataa maamuzi haya yote yanayokiuka sheria ya kimataifa. Israel haina mamlaka juu ya eneo la Palestina, kwa hivyo maamuzi haya yote ni batili. Na tutaiomba jumuiya ya kimataifa kukutana ili kuchukua maamuzi ya kukabiliana na majaribio hayo ya Israel kulazimisha utawala wake kwa kujenga makazi ya walowezi au kunyakua eneo lolote la Palestina inalolikalia."

Umoja wa Ulaya nao umelaani hatua hizi mpya za Israel za kuimarisha udhibiti wake Ukingo wa Magharibi na kusema ni mwelekeo mwingine mbaya uliochukuliwa na taifa hilo, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wake Anouar El Anouni alipozungumza na waandishi wa habari.

Saudi Arabia pamoja na mataifa ya Kiislamu yalaani hatua mpya za Israel za kuimarisha udhibiti wa eneo la Ukingo wa Magharibi. Picha inaonyesha mwanakijiji wa Kipalestina Salameh akiwa Ras Ain al-Auja kusini mwa Bonde la Yordan la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.Picha: Tania Krämer/DW

Zaidi ya Waisrael 500,000 wanaishi kwenye makazi ya walowezi wa Kiyahudi na maeneo yanayokaliwa na Wapalestina yaliyoko kwenye eneo hilo, suala ambalo pia ni kinyume cha sheria ya kimataifa. Karibu Wapalestina milioni 3 wanaishi Ukingo wa Magharibi.

Kundi la Jamaa Islamiya laishutumu Israel kwa kumteka kiongozi wake

Mbali na hayo, kundi la wanamgambo la Kiislamu la Lebanon limeishutumu Israel hii leo kwa kumteka mmoja ya wapiganaji wake katika uvamizi wa kuvuka mpaka kusini mwa Lebanon. Israel inamtuhumu mpiganaji huyo kuwa ni kinara wa ugaidi.

Mapema leo, kundi hilo la Jamaa Islamiya lenye mafungamano na wanamgambo wa Hamas wa Palestina waliishutumu Israel kwa kumkamata afisa huyo Atwi Atwi akiwa nyumbani kwake mtaa wa Hasbaya na kumpeleka mahali pasipojulikana. Jeshi la Israel limekiri kumshikilia kwa mahojiano zaidi, huku likilishutumu kundi hilo kwa mashambulizi dhidi ya Israel na raia wake waishio eneo la kaskazini.

Na taarifa kutoka Gaza City zimesema jeshi la Israel limewaua wanamgambo wanne waliowashambulia wanajeshi wake walipokuwa wakitokea kwenye handaki kusini mwa Gaza na kutaja kama ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha vita

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW