Mataifa ya magaharibi yataka timu ya UN kuchunguza Sudan
5 Oktoba 2023Uingereza, Ujerumani, Norway na Marekani zimetoa wito huo kwa Baraza la Haki za Binadamu kuwateua wajumbe watatu watakaochunguza na kubaini ukweli juu ya uhalifu dhidi ya wakimbizi, wanawake na watoto nchini Sudan iliyotumbukia kwenye machafuko na mvutano wa muda mrefu kati ya pande mbili za kijeshi.
Umoja wa Mataifa unakadiria watu wapatao 5,000 wameuawa na wengine zaidi ya12,000 wamejeruhiwa tangu mzozo huo uanze mnamo mwezi Aprili. Zaidi ya watu milioni 5.2 wameyakimbia makazi yao, pamoja na wengine wapatao milioni moja ambao wamevuka mpaka na kwenda nchi Jirani.
Umoja wa mataifa umesema karibu watu milioni 25 ambao ni nusu ya wakazi wa nchi ya Sudan wanahitaji misaada. Rasimu ya azimio hilo imepangwa kuletwa mbele yawanachama 47 wa baraza la haki mjini Geneva mwishoni mwa wiki ijayo, kabla kumalizika vikao vyake vya msimu huu wa mapukutiko.