1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Magharibi yaahidi msaada zaidi kwa Ukraine

20 Aprili 2022

Marekani na mataifa ya Magharibi yameahidi msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine katika mapambano yake na Urusi.

Ukraine | Boris Johnson und Wolodymyr Selenskyj in Kiew
Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau wameahidi kutuma silaha zaidi. Johnson amewaambia wabunge kwamba huo ni sehemu ya msaada inaouhitaji Ukraine mbali na misaada mingine na Uingereza italitekeleza hilo.

Trudeau kwa upande wake amesema Canada itatuma silaha nzito Ukraine ila hakutoa maelezo zaidi. Rais Biden naye kupitia msemaji wa ikulu ya White House Jen Psaki amesema msaada wa kiusalama, kiuchumi na kiutu kwa Ukraine ni mambo yatakayozingatiwa na Marekani.

Viongozi hao watatu mapema Jumanne walizungumza na viongozi wengine wa Magharibi ili kushirikiana katika kuyajibu mashambulizi ya Urusi mashariki mwa Ukraine.

Eneo la Donbas linaendelea kushambuliwa kwa mabomu na Urusi

Vyombo vya habari vya Marekani vinasema nchi hiyo itaidhinisha msaada wa kijeshi wa dola milioni 800 kwa ajili ya Ukraine. Msaada huu unakuja chini ya wiki moja tu baada ya msaada mwingine wenye thamani ya kima sawa na hicho cha fedha kuidhinishwa kwa ajili ya nchi hiyo inayovamiwa na Urusi.

Silaha zilizowasilishwa Ukraine kutoka MarekaniPicha: Lithuanian Ministry of National Defense/AP/picture alliance

Wizara hiyo ya ulinzi imesema sehemu ya kwanza ya msaada huo umeshawasili katika mpaka wa Ukraine na kwa ajili ya kukabidhiwa jeshi la nchi hiyo.

Wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema Urusi inaendelea kuishambulia kwa mabomu Ukraine hasa eneo la Donbas ila majeshi ya Ukraine yamefanikiwa kuzuia majaribio kadhaa ya Urusi kuingia katika eneo hilo.

Huku hayo yakiarifiwa Urusi imeshambulia miji katika mapambano ya kuchukua udhibiti wa migodi ya makaa ya mawe na viwanda mashariki mwa Ukraine. Iwapo watafanikiwa kuchukua udhibiti wa eneo la Donbas basi Ukraine itagawika mara mbili.

Umoja wa Mataifa watoa wito wa kusitishwa kwa vita

Katika mji wa Mariupol, majeshi ya Ukraine yanasema jeshi la Urusi linakishambulia kwa mabomu kiwanda cha chuma eneo hilo ili kukiharibu kabisa na fauka ya hayo wanajeshi hao pia wameishambulia kwa mabomu hospitali moja ambapo mamia ya watu walikuwa wanaishi.

Shinikizo laongezeka kwa Ujerumani kutuma silaha nzito Ukraine

02:05

This browser does not support the video element.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi Meja Jenerali Igor Konashenkov amesema majeshi ya Urusi yameshambulia kambi kadhaa za kijeshi za Ukraine katika miji na vijiji kadhaa. Madai hayo lakini hayakuweza kuthibitishwa. Pande zote mbili katika vita hivyo zinasema mapambano hayo yamechukua mwelekeo mpya.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano nchini Ukraine kuanzia Alhamis ili kutoa nafasi ya wiki takatifu ya Wakristo wa dhehebu la Orthodox akidai wanakaribia kuadhimisha sikukuu ya Pasaka.

Chanzo: AFP/DPA

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW