Mataifa ya Sahel kuunda muungano dhidi ya wanajihadi
22 Januari 2025Kikosi cha pamoja chenye wanajeshi 5,000 kutoka mataifa jirani yanayoongozwa na jeshi—Niger, Burkina Faso, na Mali—kinatarajiwa kutumwa hivi karibuni katika eneo lenye migogoro la Saheli ya Kati, Mkuu wa Ulinzi wa Niger alitangaza kupitia televisheni ya taifa. Serikali za kijeshi katika nchi hizo za Afrika Magharibi zilichukua mamlaka kufuatia mfululizo wa mapinduzi kati ya 2020 na 2023. Mwaka jana, zilikubaliana kukabili vitisho vya kiusalama kwa pamoja baada ya kukatisha uhusiano wa muda mrefu wa kijeshi na kidiplomasia na washirika wa kikanda, Ufaransa, na mataifa mengine ya Magharibi.
Soma pia: Burkina Faso, Mali na Niger zakamilisha mpango wa ushirikiano wao
Waziri wa Ulinzi wa Niger, Salifou Mody, alisema kikosi hicho kitakuwa na uwezo wake wa anga, vifaa, na rasilimali za kijasusi, na kitafanya shughuli zake katika maeneo ya mataifa hayo matatu, ambayo yameunda mkataba wa ushirikiano ujulikanao kama Muungano wa Nchi za Saheli (AES). Akizungumza Jumanne, Mody alisema kikosi cha AES kimekaribia kukamilika, kikiwa na wanajeshi wapatao 5,000. Aliongeza kuwa ni suala la wiki chache kabla kikosi hicho kuonekana uwanjani, na kwamba baadhi ya operesheni za pamoja tayari zimekwisha kufanyika.
Soma pia: Burkina Faso na Mali zatangaza vita dhidi ya yeyote atakaeivamia Niger
Ghasia zinazochochewa na vita vya muongo mmoja dhidi ya makundi ya Kiislamu yaliyounganishwa na Al Qaeda na Islamic State zimeongezeka tangu mapinduzi hayo. Takriban watu milioni 2.6 wameyakimbia makazi yao ndani ya eneo hilo hadi mwishoni mwa Desemba, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA). Kuundwa kwa muungano huo wa mataifa matatu kunafuatia uamuzi wa nchi hizo kujiondoa kutoka jumuiya kuu ya kisiasa na kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambayo bado inazitaka zirudi nyuma kwenye uamuzi huo unaobadilisha miongo ya juhudi za ushirikiano mpana kikanda.