Mataifa ya Ulaya kujadiliana namna ya kukabiliana na droni
26 Septemba 2025
Siku ya Ijumaa, Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa masuala ya Ulinzi Andrius Kubilius amesema atazungumza kwa njia ya video na maafisa wa mataifa kama 10 hivi kati ya 27 ya umoja huo kuangazia mapendekezo ya kuwa na mifumo hiyo ya kuzuia droni.
Washiriki wengi ni wale wanaotoka kwenye mataifa ya Umoja wa Ulaya lakini yanayopakana na Urusi na Ukraine. Hata hivyo, Denmark iliongezwa kwenye orodha ya washiriki kufuatia matukio ya karibuni ya droni kuingia kwenye anga yake.
Ukraine ambayo licha ya kuwa na mfumo wake wa kugundua na kudungua droni za Urusi pia itashiriki.
Wito watolewa wa kuunda "drone wall"
Mapema mwezi huu, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von de Leyen alitoa wito wa kuwa na mfumo kama huu ama "drone wall" alipokuwa akitoa hotuba, masaa machache baada ya marubani wa NATO kudungua droni za Urusi nchini Poland.
Mjini Copenhagen, kisa kipya cha droni iliyoonekana kwenye anga ya Denmark kimesababisha uwanja wa ndege kufungwa hii ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha masaa machache, baada ya Waziri Mkuu Mette Frederiksen kusema kwamba safari za ndege ni sehemu ya "mashambulizi mseto" ambayo huenda yanafanywa na Urusi.
Droni zimeonekana zikirandaranda kwenye eneo kuliko viwanja vya ndege vya Denmark tangu siku ya Jumatano na kusababisha moja ya viwanja hivyo kufungwa kwa masaa kadhaa baada ya tukio kama hilo kusababisha kiwanja kikubwa cha Copenhagen kufungwa mapema wiki hii.
Mette amesema "Wapi tulipo kufikia sasa? Kwanza mamlaka zimeongeza hali ya tahadhari. Na zinajiandaa kwa matukio ya aina yoyote. Hii inamaanisha, kwamba, pamoja na mambo mengine wanajeshi na polisi wengi zaidi watakuwa na uwezo mkubwa na mbinu za kuzuia mashambulizo ya droni katika maeneo ya miundombinu muhimu siku za usoni."
Visa kama hivi tayari vimeshuhudiwa kwenye mataifa ya Norway na Romania pamoja na ukiukwaji ulioshuhudiwa kwenye anga ya Estonia baada ya ndege za kijeshi za Urusi kuingia kwenye eneo hilo, hali iliyoibua wasiwasi katikati ya uvamizi wa Urusiuvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
IAEA laonya kitisho cha droni kwenye vinu vya nyuklia
Katika hatua nyingine, Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA limesema leo kwamba kwa mara nyingine droni zimesababisha kitisho cha kiusalama kwenye vinu vya nyuklia nchini Ukraine.
Mkuu wa shirika hilo Rafael Grossi amesema kwenye taarifa yake kwamba droni hizo zinazoruka karibu sana na vinu hivyo zinaviweka hatarini baada ya droni moja kudunguliwa ikiwa umbali wa mita 800 kutoka kwenye kinu kilichopo mkoa wa Mykolaiv jana usiku. Droni nyingine kama 22 zilikaribia kinu hicho kiasi cha mita 500, ingawa hakukuripotiwa uharibifu.
Huku hayo yakiendelea, Kyiev imeendeleza mashambulizi yake ya kupanga ya droni kwenye vituo vya mafuta vya Urusi mamlaka zimesema hii leo, huku wataalamu wakikisia kwamba Urusi imekwishapoteza robo ya uwezo wake wa kuchakata mafuta kutokana na mashambulizi ya kila mara kwenye vituo vyake.