1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ulaya kusitisha uingizaji wa mafuta kutoka Urusi

31 Mei 2022

Viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya wamekubaliana kupiga marufuku kwa hadi asilimia 90 uingizaji wa mafuta kutoka Urusi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Belgien Brüssel | EU GIpfeltreffen - Olaf Scholz
Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP/picture alliance

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa siku ya kwanza ya mkutano wa kilele mjini Brussels uliotawaliwa na suala la mzozo wa Ukraine. 

Taarifa ya makubaliano hayo imetolewa na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya muda mfupi baada ya kumalizika kwa mashauriano marefu juu awamu mpya ya vikwazo dhidi ya Urusi katika mkutano wa siku mbili ulioanza jana mjini Brussels.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel amearifu kupitia ukurasa wa Twitter kuwa wakuu wa nchi 27 wanachama wa umoja huo wamefikia uamuzi wa kuzuia kununua sehemu kubwa ya mafuta kutoka Urusi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Uamuzi huo ni sehemu ya mkururo wa vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi tangu nchi hiyo ilipoivamia Ukraine mnamo mwezi Februari. Katika awamu ya sasa mafuruku hiyo itahusisha mafuta ya Urusi yanayosafirshwa kwa meli kuingia barani Ulaya.

Shehena ya mafuta kwa njia hiyo ya bahari ni karibu theluthi mbili ya mafuta yote ya Urusi yanayouzwa kwa mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Vikwazo vya sasa havitaligusa bomba la mafuta la Druzhba 

Rais wa Baraza Kuu la Ulaya Charles Michel Picha: Irina Yakovleva/picture alliance/dpa/TASS

Michel amesema uamuzi huo ambao ulikuwa mgumu kufikiwa utaidhabu Urusi kwa kuikatia chanzo kikuu cha mapato "kinachofadhili vita vyake".

Hata hivyo marufuku ya sasa haitahusisha mafuta yanayosafirishwa kwa kutumia bomba kubwa la tangu enzi ya dola ya Kisovieti la Druzhba linalosafirisha nishati ya mafuta moja kwa moja kutoka Urusi hadi mataifa kadhaa ya katikati na mashariki mwa Ulaya.

Hungary ilikuwa miongoni mwa mataifa kadhaa ya kanda hiyo yaliyopinga vikali kuweka vikwazo kwa mafuta yanayosafirishwa kupitia bomba hilo.

Kwa sasa bomba la Druzhba linapitisha karibu theluthi moja ya mafuta yote ya Urusi yanayotumika ndani ya Umoja wa Ulaya.

Viongozi wa EU wapitisha pia msaada wa nyongeza kwa Ukraine 

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen Picha: Valeria Mongelli/ZUMA/IMAGO

Akizungumzia awamu hiyo mpya ya vikwazo dhidi ya Urusi Kiongozi wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amewasifu viongozi wa mataifa ya kanda hiyo kwa kufikia makubaliano akisema ilikuwa hatua ngumu lakini muhimu kufikiwa.

"Kwa sasa kilichosalia ni kama asilimia 10 au 11 ya mafuta tunayoagiza kutoka Urusi ambayo yanapitia kwenye bomba la Druzhba na kwa kweli tumekubaliana kuwa kwa sasa tusiliweke kwenye vikwazo. (Lakini) tumekubaliana na Baraza kuu la Umoja wa Ulaya kurejea kujadili suala hilo kwa njia moja au nyingine haraka iwezekenavyo", amesema Von der Leyen.

Mbali ya sekta ya nishati ya mafuta awamu hiyo ya sita ya vikwazo inajumuisha pia kuzuia mali za raia kadhaa wa Urusi pamoja na kuiondoa benki kubwa ya Urusi ya Sberbank kutoka mfumo wa kimataifa wa malipo na miamala ya kibenki wa SWIFT.

Mkutano huo mjini Brussels pia umefikia makubaliano ya kuipatia Ukraine msaada wa ziada wa dola bilioni 9.7 kufidia gharama za kuendesha serikali ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi wa umma na kuendelea kutoa huduma za jamii ikiwemo shule na hospitali.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW