1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ulaya yaionya Syria

4 Oktoba 2011

Vikosi vya serikali ya Syria vimeendelea na mashambulizi dhidi ya waandamanaji, vikiwauwa zaidi ya watu 10, huku mataifa ya Ulaya yakimuonya Rais Bashar Al-Assad dhidi ya kuwashambulia wapinzani wake walio Ulaya.

Maandamano dhidi ya Rais Bashar Al-Assad katika mji wa Homs.
Maandamano dhidi ya Rais Bashar Al-Assad katika mji wa Homs.Picha: dapd

Taarifa za mauaji haya ya karibuni zaidi zinakuja katika wakati ambapo kamanda wa ngazi ya juu aliyeasi kutoka jeshi la Syria, Kanali Riad Al-Asaad, akikanusha ripoti za vyombo vya habarai vya serikali kwamba amekamatwa na jeshi.

Kanali Asaad ameliambia Shirika la Habari la Uturuki, Anatolia, kwamba yuko salama nchini Uturuki na kwamba serikali ya Uturuki imekuwa ikimpa huduma zote muhimu za kujikimu kimaisha.

Kanali Asaad na mamia ya wapinzani wako kwenye mji wa kusini wa Hatay, ambao Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyib Erdogan, anapanga kuutembelea hapo kesho, siku jeshi la nchi yake linapoanza mazoezi yake ya siku 10.

Erdogan, ambaye upinzani wake dhidi ya Rais Assad uko wazi, amesema kwamba hiyo kesho atatangaza mpango wa vikwazo vya nchi yake dhidi ya utawala wa Rais Assad. Kiasi ya Wasyria 7,000 wanaishi mjini Hatay kama wakimbizi tangu mashambulizi ya wanajeshi dhidi ya waandamanaji yaanze miezi sita iliyopita.

Rais Bashar Al-Assad wa Syria.Picha: dapd

Upinzani dhidi ya Rais Assad umeanza kugeuka sura kutoka ule wa maandamano ya amani hadi wa silaha, baada ya wanajeshi walioasi kujiunga pamoja kuwalinda raia dhidi ya vikosi vya serikali.

Akizungumza na Shirika la Habari la Reuters, Kanali Asaad amesema kwamba zaidi ya wanajeshi 10,000 wameasi na kuamua kuwalinda waandamanaji na miji yao. Wiki iliyopita, serikali ilipeleka vikosi vya jeshi vilivyosaidiwa na helikopta na vifaru kwenye mji wa Rastan ili kumkamata Kanali Asaad na wenzake, lakini havikufanikiwa.

Vikundi viwili vya wanajeshi vinavyojuilikana kama Free Officers Movement na Syrian Free Army vimejiunga pamoja dhidi ya jeshi la Rais Assad.

Katika hatua nyengine, Ufaransa na Sweden zimeuonya utawala wa Rais Assad juu ya kuwatisha na kuwashambulia wapinzani wake walio uhamishoni kwenye nchi hizo. Onyo hili limekuja huku kukiwa na taarifa za mashambulizi na vitisho katika miji mikuu ya mataifa ya magharibi.

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limesema kwamba wanaharakati wa Syria wameshambuliwa katika nchi za Ufaransa, Uingereza, Canada, Chile, Ujerumani, Hispania, Sweden na Marekani.

Ufaransa imethibitisha kuanzisha uchunguzi dhidi ya mashambulizi hayo na kuapa kwamba itachukuwa hatua zinazofaa kwa wahusika. "Hatutovumilia dola ya nje kufanya matendo ya fujo au vitisho katika ardhi yetu. Na tumemueleza hivyo kwa lugha kali balozi wa Syria mjini Paris." Amesema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, Bernard Valero.

Kwa mujibu wa gazeti la Ufaransa, Le Monde, kundi la Wasyria ambalo limekuwa likikusanyika kwenye uwanja uliopo katikati ya jiji la Paris, wamewahi kutukanwa, kupigwa picha na hata kushambuliwa.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Carl Bildt, ameonya kuwa ikiwa kuna mabalozi wanaojihuisha na kazi zisizoafikiana na masharti ya kimataifa watafukuzwa nchini mwake. Amnesty Interanational imeyataka mataifa ya magharibi kuwachukulia hatua kali maafisa wa kibalozi wa Syria wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Mara kadhaa ndugu na jamaa wa wanaharakati wa Syria walioko ndani ya Syria, hukamatwa na kuadhibiwa kwa kosa la watoto na ndugu zao kushiriki maandamano dhidi ya Rais Assad nje ya nchi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi