1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yaahidi dola milioni 345 kusaidia Warohigya

24 Oktoba 2017

Jumuiya ya kimataifa imeahidi kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 345 kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh, katika hatua iliyoelezwa kuwa ya kutia moyo.

Schweiz UN-Geberkonferenz Rohingya Flüchtlinge
Picha: Reuters/D. Balibouse

Umoja wa Mataifa unasema unahitaji Dola milioni 434 kutoa msaada hadi mwezi Februari mwakani, kwa Warohingya 900,000 waliokimbilia nchini Bangladesh, na vile vile wenyeji 300,000 wa Bangladesh waliowapokea wakimbizi hao.

Mkurugenzi wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock aliitaja michango hiyo kuwa ya kutia moyo na kuwasifiu wafadhili walioonyesha mshikamano na mapenzi kwa familia na jamii zenye kuhitaji.

Baadhi ya fedha hizo ziliahidiwa kabla ya mkutano huo na Lowcock alisema anataraji ahadi zaidi katika siku zijazo.

"Tunatarajia serikali na washirika kuendeleza kasi hii katika nyanja zote. Ufadhili ili kuongeza msaada, kugeuza maneno kuwa vitendo, na kufikia suluhu za kudumu zinazoshughulikia mizizi ya mgogoro huu ili kuukomesha mara moja" alisema Lowcock.

Mkurugenzi wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock (katikati) akiwa na Mmarekani William Lacey Swing (kushoto), Mkurugenzi wa IMO, na Mtaliana Filippo Grandi (kulia), Mkurugenzi Mkuu wa UNHCR, wakati w amkutano na waandishi habari mjini Geneva, Uswisi, Oktoba 23,2017.Picha: picture-allianvce/AP Photo/S. Di Nolfi

Msisitizo wa kutolewa fedha taslimu

Lowcock alisisitiza umuhimu kwa mataifa kutoa pesa taslimu, kwa kuzingatia uzoefu wa huko nyuma ambapo Umoja wa Mataifa ulikabiliwa na ahadi zisizotimizwa katika migogoro iliyopita. Aliwaambia waandishi habari kuwa ahadi ni jambo moja, lakini muhimu ni kwa ahadi hizo kugeuzwa michango halisi haraka iwezekanavyo.

Miongoni mwa mataifa 35 na kanda zilizoahidi misaada ni pamoja na Uingereza ilioahidi kutoka dola milioni 63, Umoja wa Ulaya uliahidi dola milioni 42, Marekani dola milioni 38 na Sweden dola milioni 24 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Mnamo wakati hakuonekani kuwapo na suluhisho la mgogoro huo katika muda mfupi, Lowcock alibainisha kuwa huenda kukawa na haja ya kuchagisha tena mwakani.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la uhamiaji, IMO William Lacey Swing, alilitaja wimbi la wakimbizi wa Rohingya wanaokimbilia Bangladesh kuwa mgogoro wa wakimbizi unaokuwa kwa kasi kubwa zaidi duniani, akiuelezea kama jinamizi.

Serikali ya Bangladesh na jamii ya wilaya ya Cox's Bazar iliopo mpakani mwa Bangladesh na Myanmar wamemuagiwa sifa kwa jinsi walivyoitikia wimbi la wakimbizi wa Rohingya, hasa kwa kuacha wazi mpaka.

"Na mimi naungana na nyinyi, kuishukuru Bangladeshi chini ya uongozi wa waziri mkuu wake, kwa kuonesha mfano kwa dunia nzima, kwa kuacha mipaka wazi kwa watu walioathirika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na masuala ya ulinzi," alisema Filipo Grandi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR.

Picha hii iliyopigwa Oktoba 7, 2017, inaonyesha makaazi ya muda ya wakimbizi wa Warohingya katika ya Kutupalong katika wilaya ya Cox's Bazar.Picha: Getty Images/AFP/I. Mukherjee

Marekani kuliweka vikwazo jeshi la Myanmar

Jamii ya Rohingya imenyimwa haki zozote za msingi kwa miongo kadhaa katika taifa la Myanmar lenye idadi kubwa ya Waumini wa dini ya Budha. Katika ukandamizaji wa karibuni zaidi, vikosi vya usalama vya Myanmar vimewafyatulia risasi bila kuchagua, raia wasio na silaha wakiwemo watoto, na kutenda uhalifu mkubwa wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana, kulinga na taarifa za Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, Marekani imesema inatafakari kuiwekea Myanmar vikwazo kuhusiana na ukandamizaji huo, ikisema katika taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje, kwamba watu binafsi na taasisi zilizohusika katika ukatili huo laazima ziwajibishwe.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtre.

Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW