Mataifa yajiandaa kwa COP23
3 Novemba 2017Hii haijawahi kutokea. Kwa kawaida, nchi inayokuwa mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kujadili tabia ya nchi ndiyo inayoongoza mkutano huo. Lakini mwaka huu mambo ni tofauti. Mji wa Bonn wa hapa Ujerumani ndio utakuwa mwenyeji, wakati Visiwa vya Fiji chini ya uongozi wa jenerali wa zamani Frank Bainimarama, vikisimamia mkutano huo. Hiyo ni kwasababu viongozi wa Fiji wamekiri kuwa hawana ukumbi mkubwa wa mikutano wa kutosha watu 25,000 - walinzi wa mazingira, waandishi wa habari na wawakilishi wa mataifa mbalimbali. Kwa visiwa 300 vya Fiji, mabadiliko ya tabia ya nchi ni mada nzito. Ni jambo linalotishia maisha ya wananchi.
Walinzi wa mazingira wanatarajia kwamba Bainimarama ataweza kuleta pamoja hoja za pande tofauti na kuwafanya watu wafikie muafaka. Sabine Minninger wa shirika la misaada la hapa Ujerumani, Brot für die Welt, ametembelea Visiwa vya Fiji mara kwa mara. "Watatutmia fursa hii kufahamisha kuhusu hali ya hatari inayovikumba visiwa vya Bahari ya Pasifiki. Wao ndio wanaoathirika zaidi, kwa mfano kwa kiwango cha bahari kupanda. Hiyo imesababisha wakazi wote wa kijiji kimoja cha Visiwa vya Fiji kuhamishwa, jambo ambalo ni la kipekee duniani."
Nchi nyingine zitamfuata Trump?
Mwaka 2015, mataifa ya dunia yalifanya mkutano wa mabadiliko ya tabia ya nchi Paris na kusaini makubaliano ya kudhibiti ongezeko la joto duniani, lisizidi nyuzijoto mbili. Katika mkutano wa Bonn, Ujerumani inawakilishwa na Waziri wa Mazingira Barbara Hendricks. Hii itakuwa mara yake ya mwisho kuhudhuria mkutano kama huu, kwani baada ya uchaguzi uliopita, chama chake cha SPD kitakuwa sehemu ya upinzani. Hendricks anashikilia wadhifa wa uwaziri hadi serikali mpya itakapoundwa. "Natarajia kwamba tutakubaliana juu ya hatua za kufuata ili kutimiza makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi. Kwa juu juu hilo linaonekana kama jambo dogo, lakini ikumbukwe kwamba makubaliano yaliyofikiwa Paris Disemba 2015 yalikuwa kama sheria mpya kwa dunia nzima kwahiyo lazima sasa tuweke masharti ya kutekeleza."
Lakini lipo jambo linaloweza kuzuia mafanikio. Donald Trump, mara baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani, aliitoa nchi yake kwenye makubaliano ya Paris ya kulinda mazingira. Sabine Minninger wa shirika la misaada la Brot für die Welt hata hivyo haamini kwamba nchi nyingine zitafuata mfano wa Marekani. "Tulichoshuhudia katika majadiliano ya awali yaliyofanyika Bonn Mei mwaka huu, ni kwamba mataifa ya dunia yanaendelea kukaribiana na kushirikiana. Pamoja na mambo mengine, hali hiyo inachangiwa na majanga kama vile vimbunga ambavyo vimekumba visiwa vya Carribean. Hatua ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya Paris pia imeimarisha mshikamano baina ya mataifa yaliyobakia."
Mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia ya nchi utaanza tarehe 6 mwezi huu na kumalizika tarehe 17.
Mwandishi: Jens Thurau
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman