1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yaliopoteza raia ajali ya ndege ya Ukraine kukutana

Sekione Kitojo
13 Januari 2020

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine, amesema mataifa matano ambayo raia wake wamefariki katika ajali ya ndege wiki  iliyopita yatakutana mjini London siku ya Alhamis kujadili uwezekano wa kuchukua hatua ya kisheria.

Iran | Überreste des abgestürzten Flugzeugs der Ukraine International Airlines
Picha: Reuters/West Asia News Agency

Wakati huo huo, msemaji wa wizara ya mambo ya  kigeni  nchini  Ujerumani amesema  watu wa  Iran wanapaswa  kuruhusiwa  kufanya maandamano  ya  amani  na  huru, baada ya  maafisa  nchini  Iran kukiri kuiangusha  ndege ya  abiria  ya  Ukraine. 

Akizungumza  kandoni mwa  ziara  rasmi  nchini  Singapore leo, waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ukraine  Vadym Prystaiko amesema  nchi  hizo pia  zitajadili  kulipwa  fidia  na  uchunguzi kuhusiana  na  ajali  hiyo. Watu  wote  176  waliokuwamo  katika ndege  hiyo  walifariki  katika  ajali  hiyo  siku  ya  Jumatano, dakika chache  baada  ya  ndege  hiyo  kuruka kutoka  katika  uwanja  wa ndege  wa  Tehran.

Prystaiko  amesema  maelezo  kutoka  Iran  kuwa  ndege  hiyo  ya shirika  la  ndege  la  Ukraine iliangushwa  wakati  ikiruka  karibu na eneo  nyeti  la  kijeshi  wakati  wa  kipindi cha  wasi wasi  wa  hali ya  juu , yalikuwa ni "upuuzi". Amesema  Tehran  imekubali  kukabidhi visanduku  vyeusi  vya  ndege  hiyo  kwa  Ukraine  ili  kufanya uchunguzi  zaidi.

Maandamano makubwa mjini Tehran baada ya viongozi wa nchi hiyo kukiri kuangushwa kwa ndege ya abiria ya Ukraine na jeshi la nchi hiyo.Picha: picture-alliance/dpa/Photoshot/A. Halabisaz

Waziri wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ujerumani Heiko Maas  ameitaka Iran  leo kuacha  kuingilia  kati  mizozo  katika  eneo  hilo  wakati wa ziara  yake nchini  Jordan.

Wairani wana haki ya kuandamana

"Tumekubaliana. Iwapo Iran inataka  kupunguza hali ya  kuongezeka kwa  wasi wasi, inapaswa  kuacha  uchokozi katika  eneo  hilo, ambalo  ni  pamoja  na  Iraq," Maas  amesema  hayo  baada  ya kukutana  na  mwenzake  wa  Jordan , Ayman Safadi.

"Wairani wana  haki ya  kuingia  mitaani  kuelezea "masikitiko yao na  pia  hasira  zao" baada  ya  ajali  ya  ndege, msemaji  wa  wizara ya  mambo  ya  kigeni  ya  Ujerumani  Maria Adebahr  amesema.

"Tunaamini  hili  linapaswa  kutokea  kwa  amani , uhuru na  bila vizuwizi."

Maandamano yalizuka  mwishoni  mwa  juma baada  ya  majeshi  ya ulinzi  ya  Iran  kukiri kusababisha  ajali  ya  ndege  wiki  iliyopita ambayo imeuwa  watu  wote  katika  ndege  hiyo  ya  abiria.

Wakati  huo  huo  Uingereza  imemuita  balozi wa  Iran  nchini  humo leo  kupinga  kukamatwa  kwa  afisa  wa  ubalozi  wa  Uingereza mjini Tehran  mwishoni  mwa  juma, serikali  imesema.

Waombolezaji wakiweka mishumaa kuombolewa wahanga wa ajali ya ndege ya Ukraine nchini IranPicha: picture-alliance/dpa/Photoshot/A. Halabisaz

London  inataka  kueleza  kupinga  kwake  kwa  nguvu  kabisa  juu ya  ukiukaji  mkubwa  wa  itifaki  ya  kidiplomasia, msemaji  wa waziri  mkuu Boris Johnson amesema leo. Msemaji wa  serikali ya Iran Ali Rabiei akijibu  swali kuhusu hatua  hiyo ya  Uingereza alisema:

Hatua hii ya  balozi wa  Uingereza ni kinyume  kabisa  na  kazi yake na haikubaliki  na  kwa  kumuita katika wizara  ya  mambo ya  kigeni tumewasilisha  upinzani wetu kwa  balozi  na  serikali ya  Uingereza. Uingereza  ina  rekodi ya ripoti  mbaya juu ya  uingiliaji  masuala  ya  ndani ya  Iran."

Balozi Rob Macaire  alikamatwa  siku ya  Jumamosi baada  ya maandamno  kuzuka  katika  kumbukumbu ya  watu 176 waliofariki katika  ajali ya  ndege  baada  ya  majeshi  ya  Iran kuidungua  kwa makosa.