Mataifa yanayoendelea yaonyesha umoja katika majadiliano ya WTO.
16 Novemba 2007Kiasi cha nchi 100 zinazoendelea za kusini zimeonyesha umoja , msimamo imara, na utayarifu wa kujadiliana , amesema waziri wa mambo ya kigeni wa Brazil Celso Amorim , mratibu wa kundi la mataifa 20 yanayoendelea yanayoletwa pamoja na maslahi yao ya pamoja katika kilimo.
Taarifa kadha za pamoja zilizotolewa siku ya Alhamis mjini Geneva na wawakilishi wa mataifa yanayoendelea zinaonesha madai yao katika nyanja zote za majadiliano ya Doha, ambayo ni pamoja na kodi za viwanda , huduma, sheria za biashara na nyanja nyingine muhimu kwa mataifa hayo masikini, kama vile uhusiano maalum na tofauti na utekelezaji wa ahadi zilizopo zinazogusa mataifa hayo yanayoendelea.
Azimio la Doha , lililoidhinishwa hapo Novemba 14 , 2001 katika mji mkuu wa Qatar na mkutano wa nne wa mawaziri wa mataifa wanachama wa WTO, lilizindua majadiliano juu ya kufungua milango ya biashara. Lakini majadiliano hayo yamekwama.
Tofauti baina ya mataifa tajiri na yale masikini zimekingama katika njia kuelekea makubaliano juu ya kuweka sheria ama mifumo ambayo itatawala katika hatua ya mwisho katika mazungumzo kuhusu kilimo, wakati wanaojadili watakapoamua juu ya maridhio ambayo kila upande utapaswa kutoa.
Makubaliano juu ya kilimo , suala la juu katika mazungumzo ya Doha, kama mataifa yanayoendelea yalivyodokeza kwa mara nyingine, yanapaswa kusaidia maelewano katika maeneo yote. Lakini hilo bado ni suala lisolo dhahiri hadi sasa, wamesema washiriki wa majadiliano kutoka mataifa masikini. Waziri wa mambo ya kigeni wa Argentina Jorge Taiana ameliambia shirika la habari la IPS kuwa njia pekee , mkwamo katika mazungumzo ya Doha unaweza kuepukwa ni kwa njia ya ahadi nzuri zaidi kutoka kwa mataifa yenye viwanda. Amesisitiza kuwa ikiwa hilo halitafanyika , hakuna suluhisho linalowezekana. Kuhusiana na nafasi kwamba mataifa tajiri yanaweza kuyafanya bora zaidi mapendekezo yao , Taiana anasema , haoni kama hilo linawezekana , katika muda mfupi ujao.
Kutokana na sababu hiyo, anaweka msisitizo wa majadiliano kufanyika mjini Geneva, ambapo amesema , kumekuwa na umoja na uratibu miongoni mwa mataifa yanayoendelea. Amorim amedokeza kwa upande mwingine vichwa vya habari vya vyombo vya habari katika mataifa tajiri katika muda wa siku chache zilizopita kuwa vimetaja kile kinachoonekana kuwa mgawanyiko miongoni mwa mataifa yanayoendelea na kuishutumu Brazil na India kwa kuzuwia majadiliano.
Waziri huyo amedokeza kuwa wenye shaka na wale wakosoaji , waangalie nyaraka kadha zilizoidhinishwa na mataifa yanayoendelea, ambazo zinalinda malengo yao ya pamoja.
Mafanikio katika mazungumzo ya Doha pia yameoneshwa katika mijadala miongoni mwa mataifa yanayoendelea kama chombo cha uokozi katika hali ya wasi wasi wa kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi duniani unaosababishwa na mzozo wa kifedha nchini Marekani na Ulaya. Mafanikio ya matokeo ya majadiliano ya Doha katika muda wa miezi michache ijayo yatakuwa dawa mjarabu ya hali hii isiyokuwa na uhakika.