1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayoongoza kiuchumi yatazamwa kuwa fisadi

23 Januari 2020

Mataifa yenye nguvu duniani kiuchumi yanatazamwa kuendelea kuwa fisadi. Hayo ni kulingana na faharasa ya uchunguzi wa hivi karibuni wa shirika la Transparency International.

Indien Protest gegen Korruption in Westbengalen
Picha: DW/P. Samanta

Serikali za Canada, Ufaransa, Uingereza na Marekani zimeendelea kuwa fisadi zaidi machoni mwa wataalamu na wakurugenzi wa kibiashara. Hayo ni kulingana na faharasa hiyo ya rushwa duniani iliyochapishwa leo na shirika la Transparency International.

Mkuu wa Transparency International Delia Ferreira Rubio amesema hatua ya kuhangaishwa na ufisadi wa serikali, pamoja na ukosefu wa imani katika taasisi, zinaelezea haja ya uadilifu mkubwa wa kisiasa.

Faharasa hiyo huziorodhesha nchi na kanda kulingana na mitizamo ya viwango vya ufisadi katika serikali zao, kwenye kipimo cha kuanzia 0 - 100, ambapo sifuri huashiria sekta ya umma ambayo ni fisadi zaidi. Jumla ya nchi 180 hushirikishwa na matokeo hutegemea tafiti za wataalamu na wakurugenzi wa kibiashara.

Denmark na New Zealand ndizo zimepata pointi nyingi katika kupambana na rushwa, huku Somalia, Sudan Kusini na Syria zikishika mkia.

Matokeo mabaya ya mataifa wanachama wa kundi la G-7 ambayo yanaongoza kiuchumi duniani yameonyesha hali ya kutopiga hatua mbele katika vita dhidi ya rushwa.

Canada ilishuka nafasi nne nyuma ikilinganishwa na mwaka wa 2018. Ufaransa na Uingereza zilishuka daraja kwa pointi tatu huku Marekani ikishuka chini kwa pointi mbili. Ujerumani na Japan hazikusajili mabadiliko yoyote, lakini Italia ilipiga hatua moja mbele.

Faharasa hiyo imebaini kuwa nchi ambako vyama vya kisiasa vinafadhili uchaguzi, ziko katika hatari ya kushawishiwa na makundi yenye malengo maalum ya kimaslahi na hazina uwezo wa kukabiliana na ufisadi.

Rubio amesema ni lazima serikali ishughulikie suala la fedha kutumika kisiasa kwa njia ya ufisadi ili kushawishi na kutoa shinikizo katika mifumo ya siasa.

Marekani imeorodheshwa nambari 69 mwaka huu, hiyo ikiwa nafasi mbaya zaidi ambayo imewahi kushika katika kipindi cha miaka minane iliyopita.

Je nchi yako ni fisadi kwa kiwango gani?Picha: DW/C.Vieira Teixeira

Kulingana na faharasa hiyo, nchi 22 zilisajili mabadiliko makubwa katika vita dhidi ya ufisadi kati ya mwaka 2012 na 2019, zikiwa ni pamoja na Ugiriki, Guyana na Estonia.

Nchi 21 zilisajili matokeo mabaya katika orodha hiyo ikiwa ni pamoja na Canada, Nicaragua na Australia.

Denmark na New Zealand ndizo zilishika nafasi ya kwanza bora, zikiwa na pointi 87 huku Somalia, Sudan Kusini na Syria zikiorodheshwa katika nafasi za mwisho.

Shirika la Transparency International limeonya kuwa ufisadi unadhoofisha demokrasia na unahujumu utawala wa kisheria nchini Malta na Brazil.

Vyanzo: DPA, AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW