Mataifa yaombwa kutekeleza mkataba wa Paris
18 Mei 2016Shabaha kubwa ya wajumbe wa mkutano huo ni kuona mataifa tajiri na yale yanayoendelea yanafikia makubaliano ya awali kabla ya kufikia kutia saini mkataba wa Paris mwezi Disemba mwaka huu.
"Kama unataka kujua kwanini ninafikiri tutakwenda haraka sasa, ni kwasababu , ndio, vitisho vimeeleweka. Na mwaka huu tena, leo tena, tunazidi kupata taarifa za wanasanyansi kuwa joto lizidi kuongezeka katika uso wa dunia," alisema mkuu wa sekritariat ya mabadiliko ya tabianchi ya Umoja wa Mataifa Christiana Figueres.
Lengo kubwa ni kuhakikisha kiwango cha joto kinapungua na kufikia nyuzi joto mbili katika kipimo cha Celsius. Ili hilo liweze kutimia patahitajika kuhamasisha uchangiaji wa matrilioni ya fedha ili kuzisaidia nchi maskini kuimarisha uchumi wake na kuleta matokeo ya mabadiliko ya tabianchi.
Ni kwa namna gani hayo yatafanikiwa?
Wanasayansi wanasema ingawa mataifa kwa hiari yao wameahidi katika mkataba huo wa Paris kupunguza gesi ya ukaa ili isilete madhara ifikapo mwaka 2020, lakini bado wanaona ongezeko la joto katika uso wa dunia linaweza kufikia katika nyuzi joto 3 katika kipimo cha Celsius.
Nyuzi joto 1 katika kipimo cha Celsius tangu mageuzi ya viwanda imeweza kuleta madhara ya dhoruba, ukame pamoja na mabadiliko katika bahari. Wanasayansi nchini Marekani wamesema mwishoni mwa juma kuwa, mwezi uliopita wa Aprili ulikuwa mwezi wa joto kupindukia.
Waziri wa mazingira wa visiwa vya Maldives na mwenyekiti wa umoja wa visiwa vidogo, Thoriq Ibrahim aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba "swali muhimu la kujiuliza ni endapo tutaunganisha nguvu haraka na kwa ujasiri ili kuepuka majanga".
Moja ya kazi kubwa ya Umoja wa Mataifa ni kuchochea mipango katika ngazi ya kitaifa baina ya wanachama ya kuondoa uchafuzi wa gesi ya ukaa.
Hofu ya kukengeuka ahadi za kifedha
Wakati huo huo mataifa yanayoendelea yanahofia kuwa fedha zilozaahidiwa kutolewa na mataifa tajiri karibu dola bilioni 100 sawa na euro bilioni 88 kila mwaka kuanzia mwaka 2020, zitatumika katika kupambana na gesi chafu na hazitasaidia kuongeza ujasiri wa kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Ujumbe kutoka nchi za G77 na ukanda wa China umesema ili hayo yote yaweze kufanikiwa msaada wa kifedha na kiteknolojia ni lazima utolewe.
Nchi maskini ambazo tayari zimeshakumbwa na madhara katika sekta ya kilimo pamoja dhoruba kuipiga miji ya pwani, nazo zinataka kuongezewa fungu chini ya kifungu cha "hasara na uharibifu" ili ziweze kurekebisha madhara hayo na sio kujiandaa tu kwa ajili ya athari za siku za mbeleni.
Wataalamu wanasema kuridhiwa kwa mkataba wa Paris mapema mwakani huenda kukasaidia jukwaa la wanamazingira kuja na sheria na taratibu mpya zinazohitajika kusongesha suala hili katika hatua nyingine.
"Kuna kazi kubwa ya kufanya kabla ya mwaka 2020, ili kutoa uhai kwa ahadi tulizoziweka" anasema Alden Meyer mchambuzi wa masuala tabia ya nchi kutoka jijini London.
Viongozi wa kisiasa pia wamewatia moyo wajumbe wa mkutano huo wa kubadili mitazamo. Waziri wa mazingira wa Ufaransa, Segoleni Royal, aliwaambia wanadiplomasia kuwa "wao sasa sio sehemu ya mazungumzo pia ni wajenzi".
Mkutano huo wa siku 10 mjini Bonn utafuatiwa na mkutano mwingine utakaofanyika mapema mwezi Novemba mjini Marrakesh nchini Morocco.
Sikiliza pia hapo chini mazungumzo kati ya Sudi Mnette na mjumbe wa bodi ya dunia ya mfuko wa mabadiliko ya tabianchi - Green Climate Fund anaeiwakilisha Afrika, ambaye pia ni naibu mkurugenzi anaehusika na mazingira katika ofisi ya makamu wa rais nchini Tanzania.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef