Mataifa yapongeza kufikiwa makubaliano Mashariki ya Kati
8 Aprili 2026
China imepongeza leo usitishaji vita Mashariki ya Kati, na ikasisitiza jukumu lake katika kuhimiza makubaliano ya amani kati ya Marekani na Iran kwa muda wa wiki mbili.
Msemaji wa mambo ya nje Mao Ning, ameelezea kujitolea kwa nchi hiyo kwa amani ya Mashariki ya Kati.
Tunaunga mkono juhudi za mapatano zilizofanywa na Pakistan na mataifa mengine, kusitishwa kwa mapigano na kukomesha migogoro haraka iwezekanavyo, kutatua mizozo kwa njia za kisiasa na kidiplomasia, na hatimaye kupatikana kwa amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati na eneo la Ghuba. China pia imefanya juhudi zake katika hili.
Mao Ning pia amesema China itaendeleza juhudi za kupunguza mvutano na kufikia makubaliano ya kudumu ya kumaliza vita hivyo.
India yatarajia uhuru wa usafirishaji bidhaa kupitia Hormuz
India imesisitiza kuwa kupunguzwa kwa vita, mazungumzo na diplomasia ni muhimu kumaliza haraka mzozo huo.
Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema tayari mzozo huo umesababisha mateso makubwa kwa watu na kuvuruga usambazaji wa nishati duniani pamoja na mitandao ya kibiashara.
Imesema wanatarajia uhuru wa usafirishaji wa bidhaa kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz utazingatiwa.
Wakati huo huo, Uturuki imesema itaunga mkono mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika nchini Pakistan.
Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesisitiza haja ya usitishaji huo wa mapigano kutekelezwa kikamilifu na kwamba pande zote lazima zizingatie makubaliano hayo.
Kallas asifu makubaliano ya amani
Katika Umoja wa Ulaya ,mkuu wa sera za nje Kaja Kallas, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu ya kupunguza vita hivyo baada ya wiki mbili za malumbano makali.
Kwenye chapisho katika mtandao wa X, Kallas amesema amezungumza na waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Mohammad Ishaq Dar na kuongeza kuwa mlango wa mazungumzo lazima ubaki kuwa wazi wakati ambapo masuala nyeti ya vita hivyo bado hayajapata ufumbuzi.
Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema tangazo hilo la makubaliano ni hatua nzuri . Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Usalama na Ulinzi mjini Paris, Macron ameongeza kuwa ni muhimu kwa Ufaransa kuhakikisha kwamba usitishaji kamili wa vita hivyo unajumuisha pia Lebanon.
Mataifa kadhaa ya Kiarabu pia yamepongeza makubaliano hayo na kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz.
Waziri wa mambo ya nje wa Oman amesema nchi hiyo imesisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za kupata suluhisho linaloweza kumaliza mzozo huo kabisa.
Nayo wizara ya mambo ya nje ya Misri imesema kusitishwa kwa operesheni za kijeshi za Marekani nchini Iran, kunatoa fursa muhimu ya diplomasia na mazungumzo.
Upinzani Israel wapinga usitishaji vita nchini Iran
Hata hivyo Israel imesema inaunga mkono uamuzi wa Marekani wa kusitisha mapigano lakini ikasisitiza kuwa makubaliano hayo hayaijumuishi Lebanon. Lakini kwa upande wake, kiongozi mkuu wa upinzani wa nchi hiyo Yair Lapid, amekosoa vikali hatua ya Netanyahu kuunga mkono usitishaji vita na kuitaja kuwa "janga la kisiasa" huku akimtuhumu Waziri Mkuu huyo kwa kushindwa kufikia malengo ya vita na kutokomeza kabisa kitisho kwa Israel.