1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Mataifa yatolea kauli hali ya Afghanistan

Angela Mdungu
16 Agosti 2021

Baada ya kundi la Taliban kufanikiwa kupenya na kuudhibiti mji mkuu wa Afghanistan Kabul na kutwaa madaraka, mataifa mbalimbali na mashirika ya kimataifa yameendelea kutolea kauli hatua hiyo

Afghanistan | Mullah Baradar Akhund
Picha: Social Media/REUTERS

Zaidi ya mataifa 60 jana Jumapili 15.06.21 yalitoa kauli ya Pamoja baada ya kundi la Taliban kushika madaraka nchini Afghanistan yakisema kuwa raia wa mataifa mengine wanaotaka kuondoka nchini humo wanapaswa kuruhusiwa kufanya hivyo na kwamba viwanja vya ndege pamoja na mipaka inapaswa kubaki wazi.

Katika kauli hiyo ya Pamoja Marekani sambamba na nchi nyingine zaidi ya 60 zikiwemo Australia, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Korea Kusini na Uingereza katika kauli yao ya pamoja zimesema walio katika nafasi na madaraka nchini Afghanistan wanalo jukumu na wanawajibika kulinda maisha ya watu na mali ili kuhakikisha amani, ulinzi na maisha ya kila siku yanarejea katika hali ya kawaida.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa watu wa Afghanistan wanastahili kuishi kwa usalama, ulinzi na utu.  na kwamba jumuiya ya kimataifa iko tayari kuwasaidia.

Marekani yabebeshwa lawama

Katika hatua nyingine msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Urusi Maria Zakharova ameibebesha lawama Marekani akisema, dunia inaendelea kushuhudia kwa hofu matokeo ya majaribio ya kihistoria ya Marekani. Tofauti na balozi za mataifa ya magharibi, ubalozi wa Urusi unaendelea na shughuli zake Afghanistan kama kawaida.

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan  alisema jana kuwa serikali yake itaendeleza kila juhudi kuisaidia Afghanistan ili kuhakikisha nchi hiyo inakuwa na utulivu. Pia  alisisitiza kwamba taifa jirani la Pakistan lina jukumu la msingi katika kuhakikisha hilo linafanikiwa. Pakistan yenyewe kupitia kwa waziri wake wa mambo ya kigeni  Shah Mahmood Qureshi imesema wakati utakapofika, itaitambua serikali ya Taliban kwa kuzingatia makubaliano ya pamoja ya kimataifa.

Mpiganaji wa Taliban akiwa na silaha nje ya uwanja wa ndege wa Hamid Karzai, KabulPicha: REUTERS

Bado mataifa ya Asia ya kambayo ni pamoja na Uzbekistan, Tajikistan, Kyrgyzstan na Turkmenistan hayajatoa msimamo wao kuhusu kile kinachoendelea hivi sasa nchini Afghanistan. Gavana wa eneo la  Uzbekistan linalopakana na Afghanistan amekanusha wasiwasi kuwa Afghanistan inavisuka upya vikosi vya serikali karibu na daraja linalounganisha mataifa hayo mawili. Nchini Somalia, vyombo vya habari vinavyohusishwa na kundi al-Shaba lenye mafungamano na al Qaeda vilishangilia hatua ya Taliban kuidhibiti Afghanistan. 

Taliban imetwaa madaraka Afghanistan ikiwa ni muda mfupi baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuondoa wanajeshi wake waliokuwa wakisaidia kupambana na kundi la Taliban nchini humo. Awali, Rais Biden alisema, hakuwa na namna bali kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo na asingeweza kumrithisha rais yeyote ajaye vita vya Afghanistan.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW