Matamshi ya Waziri wa Israel yakosolewa na nchi za Magharibi
8 Agosti 2024Waziri huyo wa fedha wa Israel na mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia ni Bezalel Smotrich aliyesema kuwa kwa sasa Israel hawana budi ila kutuma misaada ya kibinadamu huko Gaza kwa kuwa jumuiya ya kimataifa haiwezi kuruhusu kuwaua njaa watu milioni 2, ingawa alisema hiyo ingelikuwa "haki" hadi waachiliwe mateka hao.
Smotrich ambaye ni mshirika muhimu wa serikali ya mseto ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, aliitoa kauli hiyo mapema wiki hii alipokuwa akihutubia mkutano wa kuwaunga mkono walowezi. Mwanasiasa huyo anaunga pia mkono kukaliwa tena kwa Gaza, kuanzisha tena ujenzi wa makazi ya walowezi ambayo yaliondolewa mwaka 2005, na anapendekeza Wapalestina waondoke kwa hiari katika ardhi yao.
Mataifa ya Magharibi ambayo ni washirika wakuu wa Israel yamelaani kauli hiyo ya Bezalel Smotrich na kubainisha kuwa kusababisha njaa ya makusudi kwa raia ni uhalifu wa kivita. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliyataja matamshi hayo kuwa ni "aibu kubwa" akisema yanadhihirisha kwa mara nyingine tena, kutoheshimu wala kuzingatia sheria za kimataifa na kanuni za misingi ya ubinadamu.
Soma pia: Israel yaapa kumwangamiza kiongozi mpya wa Hamas
Israel imeendelea kuvutana na mataifa ya Magharibi ambapo leo hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Israel Katz amesitisha uwakilishi wa kidiplomasia wa wajumbe wa Norway kwenye Mamlaka ya Palestina kutokana na kile alichosema ni uhasama wa Oslo dhidi ya Israel tangu kuanza kwa vita vya Gaza Oktoba 7 mwaka jana. Norway imesema hatua hiyo itakuwa na matokeo mabaya.
Vita vyaendelea kupamba moto Gaza
Israel imezidisha mashambulizi yake leo Alhamisi katika Ukanda wa Gaza ambako kumeripotiwa vifo vya Wapelestina 25 katika kambi za wakimbizi wa ndani za Al- Nuseirat na Al-Bureij ambazo Israel inadai kuwa zinatumiwa kama maficho ya wanamgambo wa Hamas. Eneo la kusini pia lilishambuliwa ambapo watu 12 wameuawa katika shule mbili. Najib Ali, ni mkazi wa Deir el-Balah:
" Wapalestina hapa Gaza tunakabiliwa na mashambulizi ya kila siku. Jana usiku, tuliambiwa tuhame nyumba zetu na waliteketeza jengo la ghorofa liliokuwa jirani yetu. Hakika, sielewi kwanini walilenga nyumba hiyo kwa sababu hakuna mtu aliyeishi hapo."
Idadi ya vifo huko Gaza inaendelea kuongezeka na sasa Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas imesema watu 39,699 ndio tayari wameuawa.
Wakati hofu ikizidi kutanda kuhusu kutanuka kwa mzozo wa Gaza na kuwa vita vya kikanda, kaimu waziri wa mambo ya nje wa Iran Ali Bagheri amesema hivi leo kuwa Israel ilitenda "kosa la kimkakati" wiki iliyopita, kumuua kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran na kwamba kitendo hicho kitawagharimu pakubwa.
(Vyanzo: AFP, DPAE, Reuters, AP)