Matarajio ya wataalamu wa haki za binadamu kwa utawala wa rais Barack Obama.
23 Januari 2009Katika moja ya vikao vyake vya kwanza baada ya kushika madaraka nchini Marekani , rais Barack Obama amesitisha kesi zote zinazosikilizwa na mahakama ya kijeshi katika gereza la Guantamano. Hatua hiyo imewagusa hususan washtakiwa, ambao tayari wamefikishwa mbele ya mahakama hiyo , kama vile Khalid Sheikh Mohammed na Ramsi Binalshib. Hali hii inatimiza matarajio ya wanasiasa wa kimataifa ambao walikuwa wakizungumzia dhidi ya gereza hilo na pia serikali ya Ujerumani ambayo ilikwisha sema kuna haja ya kulifunga gereza hilo la Guantanamo nchini Cuba.
Ufungaji wa gereza hilo hata hivyo ni mgumu, hadi sasa kile kisichofahamika ni kwamba , ni vipi itawezekana kuwashughulikia wale wafungwa ambao tayari wameshanza kufikishwa mahakama , pamoja na wale ambao hawajafikishwa mahakamani. Kwa hivi sasa kuna wafungwa 250 katika gereza la Guantanamo, ambao hadi sasa hakuna anayefahamu kwa undani tofauti ya hadhi yao, kundi moja ambalo ni wafungwa wapatao 60 , wanasema maafisa wa Marekani kuwa halina hatia. Wafungwa hawa wanaweza mara moja wakaachwa huru, iwapo kutapatikana nchi ambazo zinaweza kuwachukua, ambapo watakuwa wameepushwa na mateso na kukamatwa tena katika nchi zao.
Hertha Däubler-Gmelin , mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu katika bunge la Ujerumani anaona kuwa Marekani inawajibu wa kwanza.
Kwanza Marekani ni lazima iwachukue, kwa kuwa gereza hilo ni kinyume na sheria. Hapa kuna wajibu na lazima utekelezwe. Iwapo mmoja wa wafungwa hawa atasema, kuwa tunachuki fulani na Marekani, na hatutaki kwenda huko, na kwa kuwa katika nchi yake pia hawezi ama hataki kwenda, kwa kuwa ana wasi wasi, inaweza hapo kuleweka , na mtu anapaswa kuangalia, iwapo nchi nyingine inaweza kumchukua. Hapa itachukuliwa hatua ya haraka na inawezekana pia kufunga mkataba , ambao utaongoza utaratibu huu kisheria.
Amesema hayo Hertha Däubler -Gmelin alipokuwa akizungumza na radio ya WDR.
Wiki ijayo baraza la mawaziri la umoja wa Ulaya litafanya kikao chake mjini Brussels, ili kuweza kujiweka tayari na mada hii. Wolfgang Heinz mtaalamu wa sheria za kimataifa katika taasisi ya haki za binadamu nchini Ujerumani anaona matatizo yafuatayo.
Mtu anapokuwa katika gereza la Guantanamo kwa muda wa miaka mitatu, minne ama mitano, si rahisi kupuuzia kutokana na kile kilichotokea. Ningependa kuona , kuwa watu hawa wanapelekwa katika nchi , ambako watapata usaidizi kuhusu utibabu wa madawa na kisaikolojia. Pale ambapo pia wataweza kupata kuwasiliana na familia zao, ili watu hawa waweze kurejea katika hali ya kawaida, kutokana na kile walichokumbana nacho katika gereza la Guantanamo.
Lakini kwa jumla kila mmoja anaona kuwa hatua hii ya kwanza aliyoichukua rais Obama kuwa ni sahihi kabisa. Manfred Novak ambaye ni mtaalamu wa masuala ya sheria za kimataifa na mchunguzi maalum wa haki za binadamu wa umoja wa mataifa kuhusu mateso anataraji kuwa wale wote waliohusika katika kuwafanyia mateso wafungwa hao wawajibishwe na serikali ya rais Obama.
►◄