1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matatiizo ya kimsingi yapo palepale

19 Oktoba 2011

Mada kuu katika magazeti ya leo huku Ujerumani ni kuachiliwa huru mwanajeshi wa Kiisraeli kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina na uamuzi wa Mahakama ya Ulaya kuhusu hakimiliki ya utafiti wa viinitete.

In this image from Egypt TV Tuesday Oct 18 2011 Israeli soldier Gilad Schalit is seen at an undisclosed location, during a pre-recorded interview released Tuesday. Schalit was moved to Egypt from captivity in Gaza and then on to Israel an elaborate prisoner swap deal in which hundreds of Palestinian inmates are to be freed in return for the captured tank crewman. (Foto: Egypt TV/AP/dapd) TV OUT NO SALES
Mwanajeshi wa Kiisraeli Gilad Shilat baada ya kuachiliwa huruPicha: dapd

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg kupinga kutoa hakimiliki kwa mwanasayansi wa Kijerumani, inahusika na utaratibu wa kutumia viinitete ili kuweza kupata chembe chembe za neva za kutumiwa kutibu maradhi kadhaa. Basi tutaanza na gazeti la NORDWEST ZEITUNG linalosema:

"Uamuzi huu mpya unadhihirisha waziwazi jinsi katiba na mahakama zinavyvotathmini maisha ya mtoto ambae bado hajazaliwa. Bunge la Ujerumani liliwapa wazazi haki ya kuchunguza mimba ya mtoto ili kujua iwapo ana maradhi ya urithi na hivyo kujiamulia kuitoa au la. Katika mdahalo uliozuka kuhusu utoaji mimba, katiba imetetea haki ya mwanamke kujiamulia mwenyewe. Lakini imepinga kuandikisha hakimiliki ya utafiti wa viinitete, utakaoweza pia kutumiwa kibiashara. Bila shaka huo sio uamuzi wa mwisho."

NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo limeandika hivi:

"Majaji wa Mahakama Kuu ya Umoja wa Ulaya hawakupinga utafiti unaohusika na mashina ya viinitete kwa jumla. Walichofanya ni kueleza kuwa kuambatana na mwongozo uliopo hivi sasa, hakimiliki haiwezi kutolewa kwa mafanikio ya utafiti uliofanywa. Uamuzi huo unapunguza matumaini ya kuweza kunufaika kibiashara kwa utafiti huo katika kanda ya Umoja wa Ulaya - lakini utafiti huo haujapigwa marufuku. Kwa maoni ya gazeti la Osnabrücker Zeitung huo ni uamuzi wenye usawa."

Tukitupia jicho mada inayohusika na kuachiliwa huru kwa mwanajeshi wa Kiisraeli kwa kubadilishana na wafingwa elfu moja wa Kipalestina, DER NEUE TAG linasema:

"Hatua hiyo ya kubadilishana wafungwa huenda imeleta matumaini, lakini matatizo ya kimsingi ya mzozo wa Mashariki ya Kati yapo palepale: ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi unaokwenda kinyume na sheria, hatima ya jiji la Jerusalem na kuundwa kwa taifa la Palestina."

Hata gazeti la DONAUKURIER linakubali kuwa kubadilishana wafungwa haimaanishi kuwa kisiasa kuna mabadiliko. Linaongezea:

"Ni nadra kupata habari nzuri kutoka Mashariki ya Kati. Picha za furaha za kumkaribisha mwanajeshi Gilad Shalit baada ya kuwa mateka kwa miaka kadhaa, zinasisimua - lakini hiyo haiashirii kupunguka kwa mvutano wa kisiasa katika kanda hiyo. Yawezekana kuwa uamuzi wa kubadilishana wafungwa uliopitishwa na Netanyahu ulichochewa na hofu. Kwani hivi sasa, jeshi la Misri ni mshirika anaeweza kuaminiwa na anaetegemwa kama mpatanishi kati ya Israel na Hamas. Haijulikani hali hiyo itaendelea kwa muda gani hasa mtu akizangatia wimbi la mageuzi nchini Misri."

Mwandishi:MartinPrema/dpa

Mhariri: Yusuf Saumu