1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matatizo ya watoto wa mitaani nchini Burundi

Epiphania Buzizi2 Septemba 2005

Vita na umaskini katika mataifa ya Afrika ya Kati ikiwemo Burundi,vimeyaacha mataifa hayo yakikumbwa na matatizo kem kem yakiwemo ya watoto wa mitaani na wahuni

Watoto wa mitaani, Bujumbura
Watoto wa mitaani, BujumburaPicha: UNICEF/HOWARD DAVIES

Nchi ya Burundi ambayo sasa inatoka kwenye vita, sawa na matifa mengine yaliyokubwa na migogoro ya vita katika eneo la maziwa makuu ,imerithi matatizo ya watoto wa mitaani.

Baadhi ya watoto hao walipokelewa kwenye vituo vinavyotoa huduma kwa watoto wasio na makwao, huku wengine wakiendelea kuzurura katika mitaa ya Bujumbura ambako wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Wengi wa watoto wenye matatizo hayo, wamekata tamaa ya maisha. Tofauti na vijana wengine katika mataifa yanayoendelea, ambao wana matumaini ya kuwa watu maarufu maishani, watoto wa mitaani nchini Burundi, hawajui hatima ya maisha yao. Wanasema ,Mungu ndiye atakayeamua hali yao ya baadaye.

Watoto hao wameshuhudia mabaya mengi. Wengi wamekosa wazazi kutokana na mauaji na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi, na hata wengine hawajui wazazi wao walikokimbilia.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za makadirio ya watoto wa mitaani, ambazo zimezotolewa na serikali ya Burundi,kuna watoto wapatao 3,000 wa mitaani wanaoishi mjini Bujumbura na katika vitongoji vya mji huo.

Baadhi ya watoto hao, wamefanikiwa kuwasili katika mji huo baada ya kuhangaika sana na kuzunguka huko na huko katika makambi ya wakimbizi kwenye nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.

Mfano wa watoto hao wa mitaani, ni vijana wawili Francois na Cedric, ambao wanaishi kwenye kituo cha watoto yatima cha mjini Bujumbura. Wao kwanza walipata bahati ya kutunzwa katika vituo vya watawa, na baadaye kupokelewa ktika kituo cha serikali kinachohusika na ustawi wa jamii, ulinzi na maendeleo ya watoto,ambacho kinachojulikana kama OPDE kwa ufupi katika lugha ya kifaransa.

Uongozi wa kituo hicho na mashirika mengine yanayohudumia watoto nchini Burundi, wanasema kwamba idadi ya sasa ya watoto wa mitaani, imeongezeka mara dufu ya idadi iliyokuwepo mwaka 2001.

Migogoro ya kivita iliyotokea Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo miaka iliyopita, na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi, vimechangia katika ongezeko la watoto wa mitaani nchini humo. Burundi inao watoto laki sita ambao wamekuwa yatima kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Wakati watoto waliopokelewa kwenye kituo cha OPDE kilichoko Cibitoke wakiwana maisha ya yenye hali ahueni kidogo, wenzao wanaozurura mitaani wanakabiliwa na matatizo kem kem ya ukosefu wa chakula na malati.

Kila siku jioni, ukweli wa maisha wanaoshuhudia watoto hao, ni kuparamia mashimo ya taka katika vitongoji vya mji wa Bujumbura, wakijaribu kupata chakula chao cha usiku.

Kukicha, biashara yao inaendelea kuwa ile ile ya kuomba omba,na pengine hawapati chochote kama hawajakutana na wasamaria wema.Mara nyingine, watoto hao wanalazimika kujihusisha na vitendo vya wizi kwa ajili ya kupata chochote cha kula.

Matumaini yaliyopo sasa kwa watoto wa mitaani nchini Burundi, amesema afisa mmoja wa kituo cha watoto wa mitaani cha OPDE, Anasthase Rwamo, serikali ya nchi hiyo inao mpango wa kupitisha sheria inayowalinda watoto. Amesema sheria hiyo huwenda ikapitishwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW