1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matayarisho ya Kombe la dunia na polisi ni mabingwa wa Afrika mashariki na kati

Ramadhan Ali29 Mei 2006

kocha wa Ujerumani Jürgen Klinsmann anataka kuacha urithi jinsi timu ya Ujerumani inavyopasa kucheza siku zijazo na anaelewa kwamba ikishindwa kuwika Ujerumani nyumbani,basi urithi huo hautabakia.

Jürgen Klinsmann
Jürgen KlinsmannPicha: AP

Baada ya siku 11 tu firimbi Italia katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich,kuanzisha Kombe la dunia ujerumani kifungua dimba na Costa Rica iliozabwa jana mabao 4:0 na Ukraine.

Na wakati makocha wengi watapania kuepusha kutotimuliwa endapo timu zao zikiteleza, Klinsmann hajali nini yeye kitamfikia na iwapo atasalia kocha au la.Anachojali ni kuona mfumo wa mchezo wa timu ya Ujerumani alioujenga tangu katika mchezo hata ufundishaji dimba unakubaliwa.Na ili afanikiwe katika shabaha hiyo, anapaswa kuiongoza Ujerumani kukaribia alao kutwaa Kombe na taji lake la 4 la dunia.

Klinsmann alipitisha hatua za kutatanisha, kwani mshambulizi huyu aliekuwa katika ile timu ya Ujerumani iliotawazwa mabingwa huko Roma, Itali, 1990,alimvua unahodha kipa Oliver kahn na kumpa Michael Ballack cheo hicho.Halafu akampandisha cheo kipa wa Arsenal, Jens Lehmann na kumfanya Oliver kahn kipa nambari 2.Hii ilizusha mvutano sio tu kati ya makipa hao wawili,bali pia kati ya klabu bingwa Bayern Munich na kocha Klinsmann.

Nae kocha wa Brazil,Carlos Alberto Parreira ametetea maandalio ya timu yake kwa kombe lijalo la dunia baada ya kukosolewa kuwa hakupanga changamoto za kutosha katika kipindi hiki kinachoelekea kutetea taji lake-siku11 kutoka leo.Brazil inayoania taji lake la 6 imekuwa ikijiandaa pole pole bila ya changamoto kali na imepanga mpambano mmoja tu kabla ,kuanza dimba hilo tena na timu hafifu ya New Zealand.Brazil ina miadi na Croatia Juni 13 kuanza kutetea taji lake.

Timu kadhaa zitakazo shiriki katika kombe la dunia zinaendelea na matayarisho huku Uingereza ikipanga changamoto kesho na Hungary.Kwa kuwa mshambulizi wao wayne Rooney ameumia, kocha Eriksson amepanga kumteremsha mshambulizi Peter Crouch kushirikiana usoni na Michael Owen.

Ukraine imeanza uzuri safari yake ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika Kombe la dunia.jana,Ukraine ilizaba Costa Rica mabao 4:0.Ukraine hatahivyo, ilicheza bila ya nahodha wake –mshambulizi hatari wa AC Milan, Andriy Shevchenko.

Saudi Arabia ambayo imeshawasili kambini Ujerumani imepanga kucheza na Uturuki hapo mei 31 mjini frabnkfurt keshokutwa na baadae ina miadi na Angola mjini Berlin,Juni 2.Kikosi cha Uturiki kinajumuisha ndugu 2 wanaocheza katika Bundesliga-Ligi ya ujerumani Halil na Hamit Altintop.

Taarifa kutoka Berlin zinasema maalfu ya tiketi zilizo mikononi mwa watu mashuhuri VIPS zinaweza kuzuwiwa kutumika na watu hao kwavile hazina majina ya waheshimiwa hao.

Kamati ya maandalio ya kombe la dunia ya ujerumani pamoja na kampuni la ISE yalipewa dhana na FIFA kusimamia uuzaji tiketi za kombe la dunia zimesema hazibebi dhamana ya kosa hilo.Mbali na majina ya mashabiki wanaoingia uwanjani ,tiketi zinahitaji kuionesha namba za pasiport au kadi ya utambulisho.

Kinyanyonganyiro cha Kombe la klabu bingwa za Afrika mashariki kimemalizika mjini Dar-es-salaam,Tanzania kwa ushindi wa klabu ya polisi ya Ugand.Hii ina maana Kombe hilo limetoka mikononi mwa Villa, mabingwa wa hadi sasa, na limerudi Uganda mikononi mwa Polisi ilioshiriki kwa mara ya kwanza katika kinyan’ganyiro hiki.

Katika mashindano ya kila mwaka ya kimataifa mjini Hengelo,Holland, wanariadha wakenya walitamba katika masafa ya kati na marefu:

Suleiman Simotwo alishinda mbio za mita 1500 kwa muda wake wa dakika 3:36.88

Khaled El Amri wa Morocco a,lifuata nafasi ya pili na mkenya Michael Too alikuja watatu.

Kama desturi ya mashindano ya Hengelo,Ethiopia ilitamba katika mita 10.000 ushindi mara hii ukienda kwa Ibrahim Jeylan.Wakenya walichukua nafasi ya pili na ya tatu.Micah Kogo alikuja wapili na Moses Mosop akabidi mkuridhika na nafasi ya tatu.

Katika mita 5000 wanawake, muethiopia Meseret Defar alitamba na mkenya Irene Kwambai akachukua nafasi ya pili.Mestawet Tufa wa ethiopia alikuja watatu.

Marion Jones –malkia wa zamani wa mbio fupi za kasi kutoka Marekani alirudi uwanjani mjini Hengelo na kuchukua ushindi wa mita 100 wanawake.Jones aliekumbwa na tuhuma za madhambi ya doping, alichukua muda wa sek. 10.65.

Na huko Eugene,Oregon,Marekani, bingwa wa Olimpik Justin Gatlin alichukua muda wa sek. 9.88 kumpiku bingwa wa rekodi ya dunia mjamiaca Asafa PÖowell ingawa walikimbia katika mbio tofauti.Powell alichukua muda wa sek. 9.93.Mapema mwezi huu,Justin gatlin alisawazisha rekodi ya dunia ya Asafa Powell.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW