Matayarisho ya kuanza msimu Bundesliga yanaendelea
29 Julai 2019Wakati vilabu vya Bundesliga vikijitayarisha kwa msimu ujao wa bundesliga, mabingwa watetezi Bayern Munich wamo katika heka heka ya kuimarisha kikosi chake, hasa ushambuliaji baada ya wachezaji wawili wakongwe Frank Ribbery na Arjen Robben kuamua kutundika madaluga baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 11. Klabu ya Bayern imo katika mazungumzo na mshambuliaji wa pembeni wa Manchester City na timu ya taifa ya Ujerumani Leroy Sane, na kwa mujibu wa jarida la michezo la Kicker, mazungumzo yanaendelea vizuri na kumebakia mambo kama mshahara na marupurupu mengine ambayo Man City itapata kutokana na mafanikio ya Sane katika klabu hiyo.
Hata hivyo mwishoni mwa juma uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund utawaka moto wakati Bayern Munich mabingwa watetezi wa bundesliga watakapojitupa uwanjani kupambana na wenyeji wao Borussia Dortmund kuwania Super Cup nchini Ujerumani , ikiwa ni ishara ya kufunguliwa msimu wa 56 wa Bundesliga.
Waandishi habari za michezo nchini Ujerumani wamemchagua Marco Reus kuwa mchezaji bora wa mwaka katika Bundesliga, na kocha bora wa mwaka amechaguliwa Juergen Klopp wa klabu ya Liverpool ya Uingereza ambayo imekuwa mshindi wa Champions League barani Ulaya mwanzoni mwa mwezi wa Juni.
Huko nchini Uingereza kocha wa Liverpool Juergen Klopp amekiri leo kwamba kikosi chake bado hakija kaa imara wakati kikijitayarisha kwa ajili ya mchezo wa mwishoni mwa juma wa kuwania ngao ya jamii, Community Shield, dhidi ya Manchester City.
Mo Salah , Roberto Firmino na Alisson wanarejea kikosini kwa ajili ya mazowezi leo jioni wakati Sadio Mane atakosa pambano hilo siku ya Jumapili katika uwanja wa Wembley baada ya kuwamo katika kikosi cha timu ya taifa ya Senegal kilichofikia fainali ya kombe la mataifa ya Afrika AFCON mwezi huu.
"Sitaki kutafuta visingizio kabla ya kucheza na Man City lakini tumekuwa katika matayarisho ya kabla ya msimu bila wachezaji sita," Klopp aliwaambia waandishi habari. "Siwezi kulibadili hilo. Siwezi kusema tumekuwa na wakati bora kabisa wa matayarisho ya kabla ya msimu, tumefanya mazowezi vizuri lakini michezo imekuja katika wakati mbaya."
Lakini Klopp amesema kikosi chake , ambacho kilishinda Champions League mwanzoni mwa mwezi uliopita , kitakuwa tayari kukabiliana na mabingwa wa Premier League City katika uwanja wa Wembley siku ya Jumapili.
"Sifikiri kwamba tutacheza mchezo wetu bora siku ya Jumapili, lakini ni suala la ushindi," ameongeza.
"Tukishinda tukishindwa , haitakuwa na athari katika ligi." amesema Klopp.
"Kitu nilichokiona hadi sasa , ni kwamba Manchester wako vizuri" ameongeza Klopp.