Israel yaokoa mateka 2 Gaza chini ya mashambulizi makali
12 Februari 2024Jeshi la Israel IDF limesema oparesheni ya pamoja iliofanywa na huduma ya usalama ya ndani Shin Bet pamoja na kitengo maalum cha polisi huko katika mkoa wa Rafah ilifanikisha kuwaokoa mateka wawili ambao ni Fernando Simon Marman (60), na Louis Hare (70).
Jeshi hilo limeongeza kuwa uokoaji huo umefanikiwa kupitia oparesheni hiyo tata iliofanyika leo Jumatatu katika mkoa wa Rafah, ikihusisha mashambulizi ya anga.
Msemaji wa IDF Daniel Hagar amesema watu hao wawili walikuwa ni miongoni mwa waliotekwa nyara na Hamas kutoka katika eneo la Kibbutz Nir Yitzhak mnamo Oktoba 7 kati ya mateka 250 ambao Israel inasema walikamatwa wakati wa uvamizi wa wanamgambo hao wa Kipalestina, uliosababisha vita katika Ukanda wa Gaza.
Hagar amesema kwamba wanamume hao waliokuwa wakishikiliwa mateka ni bukheri wa afya na kuongeza kuwa takriban mateka 100 wamesalia kwenye himaya ya Hamas.
"Shukrani ni kwa mashujaa waliokuwa katika uwanja wa vita, waliojitoa kwa mapenzi yote na kufiakia wakati ambao oparesheni ilifanikisha kuachiliwa kwa mateka." Alisema Hagar kwa njia ya video.
Soma pia:Israel yapanga kufanya operesheni ya ardhini mjini Rafah
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kupitia tamko lake baada ya kuachiliwa kwa mateka hao leo, ameapa uendelea na mashambulizi makali ya kijeshi katika eneo la Ukanda wa Gaza.
"Shinikizo la kijeshi litaendelea hadi ushindi kamili utakapopatikana, sanjari na kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia." Tamko la Waziri Mkuu Netanyahu lilisema.
Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Gaza
Kufuatia mashambulizi makali yanayoendelea katika eneo hilo la mashariki ya kati, wizara ya afya inayotawaliwa na Hamas imesema leo kwamba takriban watu 28,340 wameuwawa katika eneo hilo lililozingirwa kufuatia mapigano hayo.
Idadi hiyo ni pamoja na vifo 164 katika muda wa saa 24 zilizopita, huku jumla ya watu 67,984 wakijeruhiwa tangu kuzuka kwa vita mnamo Oktoba 7.
Katika hatua nyingine mwanadiplomasia Mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema kuwa shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA linahitaji kuendelea na kazi licha ya madai ya baadhi ya wafanyakazi wake 13,000 huko Gaza kushutumiwa kuhusika katika shambulio la Oktoba 7 lililoongozwa na Hamas dhidi ya Israel.
Soma pia:Wizara ya afya yasema Idadi ya waliouwawa hadi sasa Gaza yapindukia 28,000
Amesema hayo kuelekea mkutano wa mawaziri wa maendeleo wa Umoja wa ulaya mjini Brussels na kuongreza kuwa, hakuna mwingine anaeweza kufanya kile ambacho UNRWA inafanya katika eneo la Gaza ambalo linashuhudia hali mbaya ya kiutu, na kusisitiza madai yanahitaji kuthibitishwa, hivyo ni muhimu kusubiri uchunguzi kufanyika.
Wahuthi wafanya mashambulizi Bahari ya Shamu
Waasi wa Huthi wa Yemen wamesema walishambulia meli ya Marekani katika Bahari ya Shamu baada ya mashirika ya usalama ya baharini kuripoti kwamba makombora yalirushwa kwenye shehena ya mizigo.
Msemaji wa Huthi Yahya Saree alisema leo Jumatatu kwamba walifanya mashambulizi ya makombora ya moja kwa moja wakiilenga meli ya Marekani ya Star Iris kwenye Bahari ya Shamu.
Soma pia:Biden: Operesheni ya kijeshi ya Israel Gaza imepitiliza
Kampuni ya masuala ya usalama ya Ambrey imesema kuwa meli hiyo iliokuwa inapeperusha bendera ya visiwa vya Marshall, inayomilikiwa na Ugiriki ililengwa kwa makombora katika matukio mawili tofauti ndani ya dakika 20.
"Imeshambuliwa na kuna uharibifu umetokea kwenye meli," Ambrey ilisema na kuongeza kuwa katika meli hiyo kulikuwa na walinzi binafsi waliokuwa na silaha.
Mashambulizi ya Wahuthi yamesababisha baadhi ya makampuni ya meli kuzunguka kusini mwa Afrika ili kuepuka masambulizi makali kwenye Bahari ya Shamu, ambayo ni njia muhimu ikichukua takriban asilimia 12 ya biashara ya baharini duniani kote.
Waasi hao wanasema mashambulizi hayo yanalenga kuonyesha mshikamano na Wapalestina huko Gaza, ambayo imeharibiwa vibaya na vita vya Israel na Hamas tangu Oktoba saba mwaka jana.