1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni kwenye hoteli ya Bamako yakamilishwa

20 Novemba 2015

Maafisa wa usalama nchini Mali wamewaokoa mateka baada ya wanamgambo kuwakamata karibu watu 100 ndani ya hoteli ya kifahari mjini Bamako, Mali. Shambulizi hilo lilianza mwendo wa asubuhi

Mali Geiselnahme Hotel in Bamako
Picha: S. Rieussec/AFP/Getty Images

Karibu watu 27 wameuawa isipokuwa ripoti zinaonyesha kuwa idadi hiyo huenda ikapanda. Polisi wameonekana wakiingia na kutoka ndani ya hoteli hiyo ya Radisson Blu yenye vumba 190 wakiwasaidia watu kutoka nje baada ya saa kadhaa za mapambano na wangambo waliokuwa na silaha.

Waziri wa usalama wa ndani wa Mali Kanali Salif Traore amesema kupitia televisheni ya taifa kuwa watu 76 wameokolewa na vikosi vya usalama.

Maafisa wa usalama wa Mali wamesema watu 2 wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Jihadi wamefyetua risasi katika orofa ya saba ya hoteli ya kifahari mjini Bamako na wanawashikilia mateka wageni 170 pamoja na wafanyakazi.

Polisi wa Mali wakijaribu kudhibiti hali mjini BamakoPicha: H. Kouyate/AFP/Getty Images

"Mapema leo kulisikika milio ya risasi katika jaribio la utekaji nyara. Polisi wako hapo na wamelifunga eneo hilo," chanzo kimoja kimeliambia shirika la habari la Reuters. Chanzo hicho kimezinukuu duru za usalama zikisema washambuliaji wapatao 10 waliokuwa wakipiga kelele wakisema "Alahu Akbar" au "Mungu ni mkubwa" katika lugha ya kiarabu waliingia katika hoteli hiyo, lakini utambulisho wao haukujulikana.

Wizara ya ulinzi imesema watu wasiopungua 3 wameuawa wakati washambuliaji walipofyetua risasi ndani ya hoteli hiyo. Inaripotiwa washambuliaji hao wanatembea kutoka orofa moja hadi nyingine na sasa wamefika orofa ya saba.

Duru hiyo imeliambia shirika la habari la Reuters kwamba walinzi wawili wa shirika binafsi wamejeruhiwa katika hatua za mwanzo za shambulizi hilo.

Uvamizi katika hoteli ya Radisson Blu inayopatikana magharibi ya eneo la katikati ya mji wa Bamako karibu na wizara za serikali na ofisi za kidiplomasia, umefanyika wiki moja baada ya kundi la Dola la Kiislamu kuwaua watu 129 katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Wafaransa ni miongoni mwa wanaoshikiliwa

Duru zilizo karibu na ofisi ya rais wa Ufarans Francois Hollande zinasema Wafaransa 4 ni miongoni mwa watu wanaoshikiliwa mateka katika hoteli hiyo mjini Bamako.

Wanajeshi wakiingia ndani ya hoteli ya Radisson Blu, BamakoPicha: Getty Images/AFP/H. Kouyate

Shirika la habari la serikali ya China Xinhua limesema watalii wapatao 7 Wachina ni miongini mwa watu walionasa ndani ya jengo la hoteli hiyo. Nalo shirika la habari la serikali nchini Uturuki limesema wafanyakazi 6 wa shirika la ndege la Turkish Airlines ni miongoni mwa mateka wanaozuiliwa.

Kampuni inayoimiliki hoteli hiyo, Rezidor Group, imesema inafahamu washambuliaji ni wanaume wawili waliokuwa wamejihami na silaha. Kampuni hiyo aidha imesema wanaume hao wanawazuia wageni 140 na wafanyakazi 30 na kwa wakati huu haina taarifa zaidi lakini inaendelea kufuatilia hali ilivyo.

Afisa wa Ikulu ya Marekani amesema Rais wa nchi hiyo Barack Obama amearifiwa kuhusu uvamizi wa hoteli ya Bamako na mshauri wake wa masuala ya usalama wa kitaifa, Susan Rice. Obama yuko Malaysia kuhuduria mkutano wa Jumuiya ya ASEAN.

Maafisa wa vikosi maalumu vya usalama wa Mali wameingia katika hoteli hiyo kukabiliana na washambuliaji. Rais wa Mali Boubakr Keita amekatiza ziara yake nchini Chad ambako alikwenda kuhudhuria mkutano wa kilele wa kikanda kuhusu eneo la Sahel.

Mwandishi:Josephat Charo/RTRE/APE

Mhariri:Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW