Matendo ya Israel na Hamas yaweza kuwa uhalifu wa kivita
9 Aprili 2018Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu Fatou Bensouda ametoa wito wa kukomeshwa kwa umwagaji damu unaoendelea katika Ukanda wa Gaza na kuonya kuwa mahakama hiyo huenda ikawashtaki wale ambao wanatenda uhalifu mkubwa. Bensouda amesema huenda Israel na Hamas wametenda uhalifu wa kivita wakati wa vurugu za ukanda wa Gaza.
Katika taarifa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ICC, yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi, Fatou Bensouda amesema machafuko laazima yokomeshwe katika Ukanda wa Gaza. Na kwamba yeyote anayechochea au anayehusika na machafuko hayo kwa kutoa amri, kuhimiza au kuchangia kwa namna yoyote ile kufanya uhalifu wa kivita, anastahili kushtakiwa katika mahakama hiyo.
ICC: Wahusika katika machafuko ya Ukanda wa Gaza wanastahili kushtakiwa
Akizungumzia ghasia za hivi karibuni, Bensouda amesema machafuko dhidi ya raia yanaweza kuchukuliwa kuwa uhalifu wa kivita, kulingana na mkataba wa Roma.
Katika kauli yake nyingine iliyoonekana kuwalenga viongozi wa kundi la Hamas, Bensouda amesema kutumia uwepo wa raia kama ngao au kinga katika maeneo ya vita vya kijeshi, pia kunaweza kuchukuliwa kuwa uhalifu wa kivita.
Kwa mujibu wa Bensouda, uhalifu wowote ambao umefanywa kwa muktadha wa hali ya Palestina, unaweza kuchunguzwa na ofisi yake.
Israel inakabiliwa na maswali kuhusu kutumia risasi za moto na kuwaua Wapalestina 30 katika maandamano ya siku kumi, ambayo yalikumbwa na vurugu katika mpaka wa Ukanda wa Gaza.
Katika maandamano yaliyofanyika Ijumaa iliyopita, maelfu ya watu waliandamana na Wapalestina 9 waliuawa akiwemo mwandishi wa habari.
Mnamo Januari mwaka 2015, maafisa wa Palestina walitia saini mkataba wa Roma hivyo kujiunga na Mahakama ya Kimataifa ICC.
Uchunguzi wa ICC kuhusu matukio ya Palestina
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda amekuwa akiendelea na uchunguzi wa awali kubaini ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuanzisha uchunguzi wa kina dhidi ya madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa ndani ya Palestina tangu mwezi Juni mwaka 2014.
Israel imesema maandamano yanayofanyika katika Ukanda wa Gaza, ni kifumba macho tu ili vikosi vyake vishambuliwe, na ni juhudi za kuvunja uzio wa mpaka. Imejitetea kwamba wanajeshi wake wamewashambulia tu wale wanaojaribu kuchochea mashambulizi.
Lakini kauli za walioshuhudia pamoja na kanda za video zilizonaswa na watu wa kawaida, zinaonesha baadhi ya waandamanaji walipigwa risasi licha kwamba hawakuwa na silaha au walikuwa mbali na mpaka huo.
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimetaka uchunguzi huru ufanyike kuhusiana na matukio hayo.
Hamas, ambalo ni kundi linalofuata msimamo mkali na ambalo haliitambui Israel, limeitisha maandamano hadi Mei 15, siku ambayo ni maadhimisho ya Israel, lakini kwa Palestina, itakuwa kumbukumbu ya Wapalestina wengi waliotimuliwa wakati wa vita vya 1948 kupinga kuundwa kwa Israel.
Mwandishi: John Juma/AFPE/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga