Mateso ya Taliban kwa wanawake ni uhalifu dhidi ya ubinadamu
26 Mei 2023Kwenye ripoti mpya, shirika la Amnesty International na Tume ya Kimataifa ya Wanasheria au ICJ, yalisisitiza jinsi ukandamizaji wa Taliban dhidi ya haki za wanawake pamoja na vifungo gerezani, watu kupotezwa kwa lazima, mateso na dhuluma nyinginezo, vinaweza kuzingatiwa kama mateso ya kijinsia chini ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC.
Ripoti hiyo yenye kichwa: "Vita vya Taliban dhidi ya Wanawake, Uhalifu dhidi ya Ubinadamu na mateso Afghanistan" ilitaja sheria ya mahakama ya ICC inayoorodhesha unyanyasaji wa kijinsia kama uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Afghanistan yajadiliwa kimataifa
Agnès Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International, ameitaka jamii ya kimtaifa kuuvunja ule aliosema ni "mfumo wa ukandamizaji na mateso wa kijinsia", huku akisisitiza kuwa yanayofanyika Afghanistan ni vita dhidi ya wanawake.
Amnesty International pia ilitaja visa vya wanawake na wasichana kuozeshwa kwa lazima kwa wanachama wa Taliban.
ACJ_ Vita vya Taliban vinaingia kwenye kundi la uhalifu dhidi ya ubinadamu
Santiago A. Canton, Katibu Mkuu wa shirika la ICJ, amesema vitendo vya Taliban vinatekelezwa kwa ‘wingi na utaratibu' na kwamba "vinaingia kwenye kundi la uhalifu dhidi ya ubinadamu hasa unyanyasaji wa kijinsia."
Mataifa yajadili haki za wanawake wa Afghanistan
Mashirika hayo yametoa wito kwa nchi pia kuliwajibisha kundi la Taliban chini ya sheria ya kimataifa.
Ripoti hiyo pia imelituhumu kundi la Taliban kwa kuwalenga wanawake na wasichana walioshiriki maandamano ya amani na kuwafunga jela au kuwapoteza kwa lazima na kuwatesa wakiwa vizuizini. Ripoti imeongeza kuwa kundi la Taliban pia limewalazimisha wale waliokamatwa kusaini ahadi za kiapo kwamba hawataandamana tena.
Kundi la Taliban lilichukua madaraka nchini Afghanistan Agosti 2021, wakati majeshi ya Marekani na ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO yalipojiondoa nchini humo baada ya miongo miwili ya vita.
Taliban na tafsiri yake ya Sharia
Licha ya ahadi za awali za kutekeleza sheria za kawaida, utawala wa Taliban ulianza kuweka vikwazo dhidi ya wanawake na wasichana, kuwazuia kushika nyadhifa na kazi nyingi za umma.
Umoja wa Mataifa walaani Taliban "kuwakandamiza" wanawake
Aidha kundi hilo liliwapiga marufuku wasichana kupata elimu ya zaidi ya darasa la sita. Hatua hizo zilirejesha misimamo ya utawala uliopita wa Taliban nchini Afghanistan, mwishoni mwa miaka ya 1990, wakati walipoweka tafsiri yao kali ya sheria za dini ya Kiislamu au Sharia.
Sheria hizo kali zilizusha shutuma za kimataifa dhidi ya Taliban, ambao utawala wake haujatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa.
(Chanzo: APAE)