Mateso ya wahamiaji nchini Afrika Kusini
10 Novemba 2004Kaajal Ramjathan-Keogh wa shirika la Mawakili Wanaotetea haki za Binadamu, anasema chuki dhidi ya wageni haitoki kwa raia wa nchi pekee bali pia kwa jinsi nchi inavyowatendea watu kutoka mataifa ya nje. Wakili huyo anaelezea kwamba kuna sheria za kulinda wageni nchini humo, lakini sheria hizo hazifuatwi kama inavyotakikana.
Uchumi mzuri wa Afrika Kusini pamoja na uthabiti wa hali ya siasa ni baadhi ya vitu ambavyo vinawavutia wahamiaji kutoka kila pembe ya Afrika, ambao wanaelekea Kusini kutafuta kazi. Hii imesababisha wahamiaji hao kuchukiwa na Waafrika Kusini wenyewe ambao wanahofia kupoteza ajira haba zilizoko, kwa wageni.
Ripoti iliyowasilishwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa serikali, ilisema kwamba wahamiaji walio nchini Afrika Kusini kinyume na sheria, wanakamatwa na kufungiwa ndani ya magereza ambayo hayana nafasi za kutosha na ambapo kuambukizwa maradhi ya ukimwi, udhalilishaji na kupigwa ni tukio la kila siku. Wengi wao wanarudishwa makwao kabla ya kuomba hifadhi au wakiwa bila hati za kuonyesha wanaruhusiwa kukaa nchini humo.
Kamishna Mkuu wa Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, anasema kuna kadri wakimbizi elfu ishirini na sita ambao wameshapewa vibali vya kukaa nchini humo na kuna wengine elfu thelathini na sita ambao wanangojea kupata vibali. Idadi ya wahamiaji ambao wako Afrika Kusini kinyume na sheria ni juu kushinda ile ya wakimbizi.
Wanaharakati wanaotetea haki za binadamu, wanasema wamelenga kituo kimoja kinachojulikana kama Lindela mjini Johannesburg, huu ukiwa ni mji ambao una wahamiaji wengi. Katika kituo hicho cha Lindela, inasemekana wageni wanazuiliwa kwa zaidi ya siku thelathini, ambazo zinazidi siku zinazokubaliwa kisheria.
Wageni wapatao ishirini na tano wamekufa katika kituo hicho huku wengine, wakiwemo watoto wakidhalilishwa. Kuna ripoti za watu kupigwa lakini hakuna jinsi ya kudhibitisha ripoti hizo, kwani idara ya mambo ya ndani imekataa kutoa habari kuhusu visa vya watu kupigwa.
Maafisa kutoka idara ya Mambo ya Ndani wanatarajiwa kuwasili mbele ya kamati ya haki za binadamu baadaye wiki hii. Wachambuzi wanasema wanaamini kuna maelfu ya raia wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini, wengi wao wakitafuta kazi kutokana na mzozo wa kiuchumi nchini kwao.
Raia wa Zimbabwe ni sehemu kubwa ya jumla ya wahamiaji waliorudishwa makwao na serikali ya Afrika Kusini, lakini utaratibu wa kuwarudisha nyumbani wahamiaji hao ni wa kikatili. Wahamiaji hao wanachukuliwa kwa treni hadi mpaka na Zimbabwe, ambapo wanafungiwa katika zizi kama wanyama wakingoja kurudishwa nyumbani. Majaribio ya kutoroka, ambayo ni pamoja na kuruka kutoka kwa treni mara nyingi yanaishia kifo, kuonyesha kwamba watu hawa wamekata tamaa kabisa na hawataki kurudi nyumbani.