Trump anaongoza matokeo ya awali uchaguzi Marekani
9 Novemba 2016Kulingana na matokeo ya hivi punde ya uchaguzi mkuu wa kumpata mrithi wa Rais Barack Obama, Trump anaongoza katika majimbo mawili muhimu ya Florida na North Carolina.
Kama ilivyotarajiwa, katika utabiri wa vyombo vikubwa vya habari vya Marekani Clinton ameshinda katika majimbo ya Rhode Island, New York, illinois, Colorado, Virginia na Nevada na amepata kura 209 za wajumbe maalum.
Trump ameshinda tayari kwenye majimbo ya Oklahama, Kansas, North Dakota, South Dakota, Texas, Wyoming, Nebraska, Ohio na Iowa na amejipatia kura 244 za wajumbe maalum. Aidha, Trump ameshinda katika jimbo la Georgia, ambalo lina wajumbe 16 muhimu.
Trump pia anatabiriwa kushinda katika jimbo muhimu la Wisconsin, ambapo anaongoza hadi sasa.
Kila mgombea anahitaji kupata kura 270 za wajumbe maalum ili kuweza kuingia katika Ikulu ya Marekani.
Hadi sasa, Trump amepata asilimia 48.27 ya kura zilizohesabiwa hadi sasa ambazo ni 51,506,337, huku Clinton akipata asilimia 47.17, ambazo ni kura 50,339,130.
Vituo vya kupigia kura tayari vimefungwa nchini Marekani, lakini bado majibu yanasubiriwa, katika mchuano huo mkali kati ya wagombea hao wawili.
Ili kuweza kufanikiwa kuingia katika Ikulu ya Marekani, Clinton sasa atapaswa kushinda katika majimbo ya Pennsylvania, Michigan na Wisconsin.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, DW
Mhariri: Sekione Kitojo