1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IEBC: Odinga aongoza, Reuters: Ruto yuko mbele

14 Agosti 2022

Matokeo rasmi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi yanaonesha mwanasiasa mkongwe nchini Kenya, Raila Odinga, akiongoza kwenye mbio za kuwania urais, huku ya Reuters yakimuweka William Ruto nafasi ya juu.

Kenia Wahlen Raila Odinga William Ruto
Picha: AFP

Matokeo rasmi yaliyotangazwa Jumamosi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)yanaonesha mwanasiasa mkongwe nchini Kenya, Raila Odinga, akiongoza kwenye mbio za kuwania urais, huku ikiwa ni asilimia 26 tu ya kura zilizohisabiwa tangu uchaguzi kumalizika siku tano zilizopita.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyowekwa kwenye ubao wa IEBC katika ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi, Odinga mwenye umri wa miaka 77 alikuwa na 54% ya kura mbele ya Naibu Rais William Ruto mwenye 45% kufikia mchana wa Jumamosi (13 Agosti).

Kenya, inayoongoza kwa kuwa na uchumi mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na demokrasia inayoshamiri, ilifanya uchaguzi wa urais, ubunge na ugavana siku ya Jumanne (9 Agosti).

Ruto na Odingawanaonekana kuchuana kwenye kinyang'anyiro cha kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ametimiza ukomo wa mihula miwili madarakani. 

Kenyatta alikosana na aliyekuwa mshirika na naibu wake, Ruto, mara tu  ya uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2017 na tangu hapo amekuwa akimsogeza Odinga karibu yake na hatimaye kumuunga mkono kwenye uchaguzi huu.

Kuzorota kwa matokeo kwazusha wasiwasi

Sehemu ya Wakenya waliopiga kura zao tarehe 9 Agosti 2022. Siku sita baadaye hawajui kwa uhakika nani aliyeshinda nafasi ya urais.Picha: Luis Tato/AFP

Jinsi utangazaji rasmi wa matokeo unavyosuwasuwa umezuwa wasiwasi miongoni mwa wananchi. Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, aliwakosowa mawakala wa vyama vya siasa, ambao wanaruhusiwa kuzichuja fomu za matokeo kabla ya kuwekwa kwenye majumuisho ya mwisho.

"Mawakala kwenye zoezi hili hawawezi kusonga mbele.... ni kama kwamba tunafanya ukaguzi wa kijasusi," aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa.

"Hatwendi mbele kwa haraka kama tunavyotakiwa. Zoezi hili linapaswa kukamilika haraka iwezekanavyo."

Wawakilishi kutoka miungano ya Odinga na Ruto hawakupatikana mara moja kuzungumzia hali inavyoendelea. 

Shirika la habari la Reuters na vyombo vyengine vya habari vimekuwa vikijumuisha fomu za matokeo kutoka majimbo 291 zilizowekwa kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi. 

Hata hivyo, matokeo hayo bado hayajathibitishwa ingawa ujumuishaji wake unakwenda vyema na uko mbele ya ule wa matokeo rasmi ya IEBC.

Matokeo yaliyokusanywa na Reuters

Kwa mujibu wa matokeo yaliyokusanywa na Reuters, William Ruto anaongoza. Picha: Baz Ratner/REUTERS

Kufikia saa 3:00 usiku, Reuters ilikuwa imeshajumuisha fomu 241 zilizomuoneshaRutoakiongoza kwa takribani 52.3% ikilinganishwa na 47% za Odinga, huku wagombea wengine wawili wakiwa na chini ya 1% baina yao. 

Fomu nyengine 30 hazikuweza kujumuishwa kwenye matokeo hayo kwa sababu zilikuwa ama hazisomeki au zilikosa baadhi ya taarifa muhimu kama vile sahihi, majina ya majimbo au jumla kuu ya kura. Fomu zinazojumuishwa na Reuters ni za awali na matokeo yake yanaweza kubadilika wakati wowote. 

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Kenya, baada ya fomu kuwekwa kwenye tovuti ya tume ya uchaguzi, zinatakiwa pia ziwasilishwe moja kwa moja kwenye kituo kikuu cha majumuisho, ambako wawakilishi wa vyama wanaweza kuzihakiki kuona endapo hazina mapungufu yoyote.

Ugumu wa kazi ya kujumuisha matokeo

Kazi ya kukusanya na kujumuisha matokeo kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya inakwenda kwa mwendo wa jongoo.Picha: Sayyid Abdul mAzim/AP/picture alliance

Mchakato huu uliwekwa kwa lengo la kuzuwia malalamiko ya wizi wa kura ambayo yamewahi kuchochea ghasia kwenye chaguzi zilizopita. Zaidi ya watu 1,200 waliuawa baada ya na wengine zaidi ya 100 kuuawa kwenye uchaguzi mwengine uliozuwa utata mwaka 2017.

Maoni ya wakenya wakisubiri matokeo ya urais

01:59

This browser does not support the video element.

Mgombea anayestahiki kutangazwa mshindi wa urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura za nchi nzima na asilimia 25 ya kura kutoka kwenye kaunti 24 kati ya 47.

Reuters haikuweza kuthibitisha majumuisho rasmi kufikia saa 3:00 usiku kwenye kituo kikuu cha majumuisho ya kura kwani mbao zilizowekwa hapo zilikuwa zikionesha taarifa nyengine.

Tume ya uchaguzi ina hadi Jumanne (16 Agosti) iwe imeshamtangaza mshindi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW