1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya kutia moyo ya Mkutano wa G7 Magazetini

27 Agosti 2019

Mada mbili kuu zimehodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani : Mkutano wa kilele wa mataifa saba tajiri kiviwanda mjini Biarritz na matokeo yake na pendekezo la chama cha SPD kutaka matajiri watozwe kodi maalum.

Frankreich | G7-Gipfel in Biarritz
Picha: picture-alliance/dpa/NurPhoto/R. Franca

Tunaanzia Biarritz ambako safari hii hali ilichangamka na matukio ya kutia moyo kupatikana ikilinganishwa na mikutano kadhaa ya kilele ya mataifa saba yanayoendelea kiviwanda G7 iliyoitishwa miaka iliyopita. Itakumbukwa mwaka jana rais wa Marekani alikataa kutia saini taarifa ya mwisho mkutano huo uliopitishwa nchini Canada. Mhariri wa gazeti la "Stuttgarter Nachrichten anasema hali hiyo imesababishwa zaidi na uhusiano mzuri ulioko kati ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais wa Marekani Donald Trump. Mhariri wa gazeti hilo la kusini mwa Ujerumani anaendelea kuandika: "Uhusiano kati ya mataifa yanayopakana na bahari ya Atlantik utaendelea kuwa mgumu- hali isiyokadirika na yenye kutegemea mazingira ya siku yakoje ndio inayotoa muelekeo wa hutuba za kisiasa na maamuzi ya rais Donald Trump.

Katika mkutano wa kilele wa G7 nchini Ufaransa, mwenyeji Emmanuel Macron amefanikiwa kupata imani ya kiongozi mwenzake wa Marekani, jambo ambalo kansela wa Ujerumani, limemshinda kwasababu ya tahayari. Kutokana na usuhuba wa hali ya juu kati ya mabwana hawa wawili, ndio maana mkutano wa kilele wa Biarritz umezaa matunda ambayo hakuna aliyekuwa akiyatarajia. Kidirisha kimefunguka kusaka ufumbuzi wa kidiplomasia pamoja na Iran."

Trump azungumzia azma ya kuitembelea Ujerumani

Upepo wa pwani wa Biarritz umemburudisha rais wa Marekani kufika hadi ya kuahidi kuja ziarani nchini Ujerumani. Gazeti la "Südkurier" linaandika kuhusu uhusiano kati ya Trump na Ujerumani. "Kwa jinsi gani uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani umedhoofika, utatambua unapozingatia ukweli kwamba Donald Trump hajawahi hata mara moja kuitembelea nchi hii ambako wazee wake wametokea. Hivi sasa Trump anataka kuibadilisha hali hiyo-kama kweli.... Mvutano pamoja na Danmark na Greenland ni onyo la kutosha. Rais wa Marekani amevunja ziara yake katika nchi hizo jirani kwasababu wenyeji mjini Kopenhagen wamelipinga pendekezo lake la kijeuri. Na ziara nchini Ujerumani pia itakuwa na maana ikiwa pande zote mbili zitaridhia kuzungumzia mada zote ambazo hadi wakati huu zimekuwa zikizusha mivutano. La sivyo basi bora Trump asalie kwao."

SPD na pendekezo la kodi ya matajiri

Mada yetu ya mwisho inahusu mjadala unaohanikiza kuhusu pendekezo la chama cha Social Democrat SPD kutaka matajiri watozwe kodi maalum ya wenye kujimudu kifedha. Kuna wanaohoji eti pendekezo hilo limelengwa kukinusuru chama hicho kikongwe kabisa cha kisiasa nchini Ujerumani kisitoweke. Hata hivyo mhariri wa "Freie Presse" anaandika: "Ukweli ni kwamba pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kuwa pana. Kodi ya wenye kujimudu haitoweza kuibadilisha hali hiyo, lakini angalao itasaidia kusawazisha mizani."

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW