1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

Matokeo ya kwanza ya majimbo yatolewa Zimbabwe

25 Agosti 2023

Matokeo ya kwanza ya majimbo yametolewa jana katika uchaguzi wa Zimbabwe baada ya zoezi hilo kucheleshwa, na hata kuongezwa muda katika baadhi ya wadi.

Uchaguzi wa Zimbabwe
Raia wakipiga kura Zimbabwe katika kituo cha kura cha Midlands, KwekwePicha: Mkhululi Thobela/Anadolu Agency/picture alliance

Matokeo hayo yanatolewa katikati ya ripoti za kukamatwa kwa wanaharakati wa mashirika ya kiraia. 

Raia wa Zimbabwe walishiriki zoezi la uchaguzi wa rais na bunge mnamo siku ya Jumatano huku wengi wakionyesha matumaini ya kufanyika mabadiliko baada ya miaka mingi ya hali ngumu ya kiuchumi.

Wachambuzi hata hivyo wameeleza kwamba, kuna uwezekano mdogo wa chama tawala cha ZANU-PF kuachia madaraka baada ya kushikilia uongozi wa taifa kwa miaka 43.

Soma pia: Upinzani Zimbabwe wadai kuwepo "wizi wa kura" uchaguzi mkuu 

Hadi jana Alhamisi, ni chini ya maeneo bunge 10 kati ya 210 ambayo yalikuwa tayari yametangaza matokeo yake, kumaanisha kuwa ni mapema mno kutabiri muelekeo wa jinsi hali itakavyokuwa kitaifa. Kadhalika, matokeo katika kinyang'anyiro cha urais hayatarajiwi kutolewa kwa angalau siku moja au mbili zaidi japo yanapaswa kutolewa kabla ya muda wa mwisho uliowekwa wa siku tano.

Muda wa kupiga kura waongezwa katika baadhi ya wadi

Viongozi wa upinzani wa wananchi kwa ajili ya mabadiliko CCC katika mkutano wa kisiasa uwanja wa White City mjini BulawayoPicha: KB MPOFU/REUTERS

Muda wa upigaji kura uliongezwa jana katika wadi 40, ambazo ni ukubwa wa vitongoji vinavyowakilisha chini ya asilimia 1 ya wadi zote 12, 274. Tume ya uchaguzi imefafanua kuwa, kuongezwa kwa muda huo kumetokana na kuchelewa kwa uchapishaji wa karatasi za kupigia kura.

Rais Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 80, ambaye alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Robert Mugabe kufuatia mapinduzi ya mwaka 2017 na baadaye kushinda uchaguzi wa utata mnamo mwaka 2018, anawania muhula wa pili.

Mpinzani wake mkuu kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita, ni Nelson Chamisa mwenye umri wa miaka 45 kutoka muungano wa upinzani wa wananchi kwa ajili ya mabadiliko CCC.

Promose Mkwananzi, msemaji wa muungano wa upinzani CCC amesema, "Tunahisi kuwa mchakato wa uchaguzi una dosari nyingi na hauwezi kutoa matokeo sahihi. Hata hivyo, tulilifahamu hilo mapema, na ndio maana tumejitayarisha kushinda uchaguzi usio huru na haki."

Wakati hayo yakiarifiwa, Marekani imeishtumu mamlaka ya Zimbabwe kwa kuhujumu zoezi zima la uchaguzi kwa kuwakamata waangalizi wa uchaguzi na Washington imetaka waangalizi hao kuachiliwa huru.

Soma pia: Nelson Chamisa, kijana anayepambana na Mnangagwa

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Mathew Miller ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambao awali ulijulikana kama Twitter, kuwa "Uvamizi wa polisi dhidi ya mashirika ya kiraia yanayoangalia jinsi uchaguzi unavyofanyika, unaonyesha wazi kuwa serikali ya Zimbabwe haiheshimu uchaguzi huru na wa haki.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa katika kituo cha umeme mjini HwangePicha: ZINYANGE AUNTONY/AFP

Polisi imesema imewakamata waangalizi 41 wa uchaguzi, na kuchukua tarakilishi na simu zao za rununu.

Shirika la Marekani la maendeleo ya kimataifa USAID ambalo limeshirikiana na baadhi ya mashirika ya kiraia nchini Zimbabwe, limesema kuwa mamlaka zinakwenda kinyume na ahadi zao wenyewe za kuruhusu uangalizi wa zoezi la uchaguzi.

Katika taarifa, msemaji wa shirika hilo la USAID Jessica Jennings ameitolea mwito serikali ya Zimbabwe kuwaachilia mara moja waangalizi hao na kurudisha vifaa vyao na kuweka mazingira salama ya waangalizi hao kuendelea na kazi zao bila vikwazo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW