1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Saar

26 Machi 2012

CDU wanaendelea kushika hatamu za uongozi mjini Saarkbrücken huku SPD,licha ya kujipatia kura zaidi,ikilazimika kuwa mshirika mdogo serikalini.

Waziri mkuu wa jimbo la Saar Annegret Kramp-KarrenbauerPicha: dapd

Matokeo ya uchaguzi katika jimbo dogo kupita yote ya Ujerumani-Saar yamehanikiza magazetini.Mbio za sakafuni huishia ukingoni na hayo ndio yaliyowasibu wana SPD na mgombea wao mkuu Heiko Maas huku FDP wakiendelea kutoweka katika majukwaa ya kisiasa na chama kidogo -Die Piraten kikizusha maajabu.

Tuanze basi na gazeti la Hessische/Niedersächsischer Allgemeine linalosema "mkamia maji hayanywi:Gazeti linaendelea kuandika:Heiko Maas amecheza vibaya karata zake na kushindwa.Kwasababu mgombea huyo wa chama cha Social Democratic alitaka kuwa waziri mkuu wa jimbo la Saar,lakini sasa atalazimika kuwa mshirika mdogo wa muungano alioupigia upatu pamoja na CDU-matokeo ambayo Maas hata bila ya uchaguzi mpya wa bunge la jimbo,angeweza kuyapata.Lakini baada ya kuvunjika serikali ya muungano ya CDU,FDP na walinzi wa mazingira ya waziri mkuu Annegret Kramp-Karrenbauer,aliona bora kuvunja mazungumzo ya kupima uwezekano wa kuunda serikali ya muungano pamoja na CDU na kujimwaga katika zoezi la tatu ili kulifikia lengo lake la kuwa waziri mkuu mjini Saarbrücken.Kwasababu za kibinafsi amewatwika wakaazi wa jimbo hilo dogo kabisa mzigo wa mamilioni ya Euro kutokana na kuitisha uchaguzi kabla ya wakati.

Sigmar Gabriel (kulia) na Heiko Maas baada ya uchaguziPicha: Reuters

Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten linatathmini matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Saarland kwa jicho la serikali kuu mjini Berlin.Gazeti linaendelea kuandika:Kansela Angela Merkel anaweza kushangiria matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Saarland pamoja na bibi Annegret Kramp-Karrenbauer.Fikra ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu inazingatiwa pia mjini Berlin,lakini kwa mtazamo wa kansela Merkel:ikimaanisha CDU ndio wapishi na SPD wahudumu.

Gazeti la Augsburgerr Allgemeine linahisi matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Saarland hayawezi kulinganishwa na yale ya daraja ya shirikisho.Gazeti linaendelea kuandika:Jimbo la Saar ni dogo sana kuweza kuleta uwiano wa hali namna ilivyo kote nchini.Mbali na SPD na FDP,uchaguzi huo umetoa funzo pia kwa chama cha walinzi wa mazingira Die Grüne na kile cha mrengo wa shoto Die Linke.Miti ya walinzi wa mazingira haioti tena mbinguni,nao Die Linke wamebakiwa na jina la Oscar Lafontaine tu.Washindi wa kweli wa uchaguzi wa jana ni Die Piraten-ambao hata nje ya ngome yao Berlin,wanaonyesha hawapati shida ya kujipatia kura.

Washindi wa chama cha Die PiratenPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la Cellesche Zeitung linamulika ushindi wa Die Piraten katika jimbo la Saar na kuandika:Waliberali wanaonyesha kuvipa kiisogo viwanja vya kisiasa vya Ujerumani.Die Piraten wanajikuta kule walikokuweko walinzi wa mazingira Die Grüne miaka kama 20 au 30 ilioyopita.Kwa namna hiyo kizazi kipya kina kila fursa ya kujipiga kifua.Kwanza lakini kitabidi,kama walivyofanya walinzi wa mazingira hapo zamani, waachane na sifa za kuwa chama cha mada moja na kutoa mapendekezo kuhusu sekta tofauti za kisiasa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri Yusuf Saumu