1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya Uchaguzi yasubiriwa Mali

29 Julai 2013

Wapiga kura walijitokeza kwa wingi katika eneo la kusini wakati tume ya uchaguzi ikifanikiwa kudhibiti hali ya mambo bila matatizo.Na katika eneo la Kaskazini hakuna mashambulio yaliyoshuhudiwa.

Wapiga kura katika mji wa Gao eneo lililokuwa likihofiwa kukabiliwa na fujo
Wapiga kura katika mji wa Gao eneo lililokuwa likihofiwa kukabiliwa na fujoPicha: Katrin Gänsler

Wananchi wa Mali wanasubiri matokeo baada ya kupiga kura katika uchaguzi wa rais, 28.07.2013,uchaguzi ambao umeendeshwa vizuri kuliko ilivyotarajiwa.Wapiga kura walijitokeza kwa wingi katika eneo la kusini wakati tume ikifanikiwa kudhibiti hali ya mambo bila matatizo. Aidha katika eneo la Kaskazini hakuna mashambulio yaliyoshuhudiwa hasa ikizingatiwa vitisho vilivyokuwa vimetolewa na waasi. Matokeo ya hadi wakati huu yanaonyesha waziri mkuu wa zamani Ibrahim Boubacar Keita anaongoza. Kutokana na hali hiyo pongezi zimeanza kumiminika kutoka kila pembe ya dunia kuusifu uchaguzi huo na wananchi wa Mali.

Pongezi

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameridhishwa na jinsi zoezi la uchaguzi lilivyopita huku waziri mkuu wa nchi hiyo Jean-Marc Ayrault akisema uchaguzi huo wa Mali uliofanyika salama na kwa njia nzuri na hayo ni mafanikio makubwa kwa Ufaransa iliyotuma wanajeshi wake katika taifa hilo la Afrika mwaka huu kupambana na makundi ya kiislamu yenye itikadi kali.

Waziri huyo akiwa ziarani nchini Malaysia amesema uchaguzi wa rais nchini Mali na dhima ya Ufaransa katika taifa hilo ni mambo yanayoipa sifa kubwa Ufaransa katika ulimwengu.Louis Michel mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya pia amesifu uchaguzi ulivyokwenda huku akisema wananchi wengi walikuwa na shauku kubwa ya kupiga kura.Imeelezwa kwamba mamia ya wapiga kura wanazungumzia juu ya kuchoshwa na utawala mbaya na wengi wangetaka kuona wagombea wote wanayaridhia matokeo ya uchaguzi huo ili nchi hiyo iendelee mbele.

Matokeo yakoje

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo bado hayajatangazwa lakini tayari ushindi unaelekezwa kwa mgombea urais aliyekuwa waziri mkuu Ibrahim Boubacar Keita anayeongoza kwa mujibu wa kura zilizokwisha hesabiwa hadi sasa.Matokeo hayo ambayo sio rasmi yamezingatia taarifa za waandishi habari wanaofuatilia shughuli ya kuhesabu kura kote nchini humo.

Bango la mgombea anayetajwa kuongoza Ibrahim Boubacar KeitaPicha: Katrin Gänsler

Inatajwa mgombea huyo mwenye umri wa miaka 69 huenda akaibuka na ushindi wa moja kwa moja katika duru hiyo ya mwanzo ya uchaguzi.Tayari wafuasi wake wameanza kushangilia katika mji mkuu Bamako nje ya makao makuu ya chama chake baada ya kupata taarifa za matokeo hayo kupitia matangazo ya redio.

Kumbukumbu

Itakumbukwa kwamba uchaguzi huu umefanyika ikiwa ni baada ya nchi hiyo kutumbukia katika vita baada ya mapinduzi ya kijeshi mnamo mwezi Marchi mwaka jana yaliyouondowa utawala wa kidemokrasia wa rais Amadou Toumani Toure,hali iliyozusha mfadhaiko nchini humo uliolitumbukiza eneo la Kaskazini chini ya wanamgambo wa kiislamu wenye itikadi kali wanaofungamanisha na mtandao wa kigaidi wa Alqaeda.

Hali ni shwari hata katika eneo la Kaskazini ikiwemo mji wa GaoPicha: Katrin Gänsler

Ni kutokana na hilo ndipo ulipoanzishwa uvamizi wa kijeshi mnamo mwezi Januari mwaka huu ukiongozwa na Ufaransa na kikosi cha Umoja wa Afrika kuwatimua waasi kutoka miji mbali mbali waliyokuwa wameiteka katika eneo hilo.Umoja wa Mataifa nao ukaamua kutuma kikosi chake cha kulinda amani mapema mwezi huu hatua iliyotowa nafasi kwa vikosi vya Ufaransa kuanza kuondoka katika taifa hilo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW