1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi Zimbabwe kutatangazwa usiku

Sekione Kitojo
2 Agosti 2018

Rais  wa  Zimbabwe  Emmerson Mnangagwa  amesema  kwamba serikali  yake  imekuwa  ikiwasiliana  na  kiongozi  mkuu  wa upinzani Nelson  Chamisa  kujaribu  kupunguza  hali  ya  wasi  wasi baada  ya  ghasia.

Simbabwe Wahl | Emmerson Mnangagwa, Präsident
Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Ghasia  zilizofuatia  uchaguzi  zilisababisha umwagikaji  wa  damu, siku  moja  baada  ya  kuushutumu  upinzani kuwa  unachochea vurugu. Hivi  sasa  polisi  imeyafunga makao makuu  ya  chama  cha  upinzani  cha  MDC  mjini  Harare.

Wanajeshi wakiwatandika wananchi kwa kuandamana mjini HararePicha: Reuters/M. Hutchings

Wanajeshi  wamewaondoa  watu  kutoka  mitaa  ya  eneo  la  kati  la mji  wa  Harare  mji  mkuu  wa  Zimbabwe  baada  ya  kutumia  risasi jana  kuwatawanya  waandamanaji  ambao  wamekasirishwa kuhusiana  na  madai  ya  udanganyifu  katika  uchaguzi  uliofanyika kwa  amani  siku  ya  Jumatatu, uchaguzi  wa  kwanza  ambao umefanyika  bila  ya  kiongozi  wa  siku  nyingi  Robert  Mugabe kugombea.

Jumuiya  ya  madola, Commonwealth  imejiunga  na waangalizi wengine  wa  uchaguzi  katika kuitaka  Zimbabwe  kutoa  matokeo ya  kiti  cha  urais  haraka  iwezekanavyo  ili  kupunguza  hali  ya wasi  wasi , ikisema  kuendelea  kuchelewesha  matokeo kutaongeza  uvumi  kwamba  matokeo  yanachakachuliwa. Tume  ya uchaguzi  imesema  matokeo  yatatolewa  hivi  karibuni.

Katika  maandishi  kadhaa  katika  ukurasa  wa Twitter, rais Emmerson Mnangagwa amesema "tunawasiliana  na  mgombe  wa upinzani  Nelson Chamisa  na  kwamba  "tunapaswa  kuendeleza majadiano  ili  kulinda  amani  yetu  muhimu." Katibu  wa  chama tawala  cha  ZANU-PF anayehusika  na  masuala  ya  kisheria Paul Mangwana  amesema  matukio  yaliyotokea  jana  yanasikitisha.

Wanajeshi wa Zimbabwe walitumia risasi za moto kuwatawanya waandamanji mjini HararePicha: Reuters/M. Hutchings

"Kutokana  na  matukio  yaliyotokea  jana, ni  masikitiko  makubwa kwamba  watu  walipoteza  maisha. Tunatoa  pole kwa  wale  wote waliopoteza  ndugu  zao. Tulifanya  uchaguzi  wetu  katika  mazingira ya  amani. Na tuna  matumaini  kwamba  hali  hiyo  itaendelea  hadi yatakapotangazwa  matokeo. Tunatoa  wito kwa  wenzetu wa upinzani kuhakikisha kwamba  waungaji  wao  mkono , wanaendeleza utulivu uliokuwapo wakati  wa  kupiga  kura.

Maridhiano

Matamshi  hayo  ya  maridhiano  yanakuja  siku  moja  baada  ya wanajeshi kutumia  risasi  za  moto  na  kuwapiga  waandamanaji , wengi  wao  walikuwa  wakirusha  mawe  na  kuwasha  moto wakipinga  madai  ya  udanganyifu  katika  uchaguzi  huo. Serikali imesema  watu watatu wameuwawa. Tume  ya  uchaguzi  pia  imetoa taarifa  ya  kushutumu  vikali  matukio  ya  jana.

Waandamanaji waungaji mkono wa chama cha upinzani cha MDC wakichoma moto katikati ya mji wa Harare wakipinga udanganyifu katika uchaguziPicha: Reuters/M. Hutchings

"Tume inapenda  pia  kusema  kwamba  inashutumu  vikali  matukio ya  jana, matukio  haya  ambayo yamesababisha  watu  kupoteza maisha  yanasikitisha na  yangeweza  kuepukwa. Tume  inatoa pole kwa  fmilia za  waliofariki  na  wale  ambao  wamejeruhiwa, na tunawatakia  wale  waliojeruhiwa  kupona  haraka."

Polisi ya  Zimbabwe imefunga  makao  makuu  ya  chama  cha upinzani  Movement for Democratic Change MDC  na  wafanyakazi 27  wa  chama  waliokuwa  wanajumlisha hesabu  za  kura wamefungiwa ndani, katibu  mkuu Douglas Mwonzora  alisema  leo. Hali kwa  mujibu  wa  mkaazi  mmoja  wa  mji  wa  Harare  Paul tawanda  ni  shwari.

"Leo  ni  shwari, maduka yote  yamefungwa  kwasababu  hali  ni  ya wasi  wasi  kwamba ghasia  zinaweza  kuanza  tena  leo. Lakini amani imeendelea  kuwapo , polisi wamerejesha  amani , lakini watu wengi  wamekwenda  nyumbani, walikuja  kazini, lakini  wamerejea nyumbani  kwasabahu ofisi  zimefungwa."

Waandamanaji wa chama cha MDC wakiandamana mjini HararePicha: Reuters/P. Bulawayo

Katibu  mkuu  wa  Umoja  wa  mataifa  Antonio Guterres  ameeleza wasi  wasi  wake kuhusiana  na  ghasia  za  baada  ya  uchaguzi nchini  Zimbabwe. Guterres  amewataka  viongozi  wa  kisiasa  na umma  kwa  jumla  kuvumiliana  na  kukataa  kila  aina  ya  ghasia wakati  wanasubiri  matokeo  kutangazwa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae / ape  rtre

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW