1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matthijs de Ligt na Mazraoui wajiunga na Manchester United

12 Agosti 2024

Klabu ya Manchester United imefikia makubaliano ya kuwanunua mabeki Matthijs de Ligt na Noussair Mazraoui kutoka miamba wa Ujerumani Bayern Munich katika uhamisho ambao huenda ukapindukia pauni milioni £50.

Bayern München Matthijs de Ligt
Beki wa kati wa Bayern Munich Matthijs de Ligt Picha: Nick Wass/AP Photo/picture alliance

Mashetani hao wekundu wamemsajili De Ligt kwa dau la pauni milioni 43 wakati leo akitarajiwa kukamilisha uchunguzi wa kimatibabu.

Beki huyo wa kati, raia wa Uholanzi atamwaga wino kwa kandarasi ya miaka mitano kuichezea Manchester United huku kukiwa na kipengee cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Bayern pia imeridhia dau la pauni milioni 17 kwa ajili ya beki wa pembeni wa timu ya taifa ya Morocco Mazraoui.

De Ligt na Mazraoui wataungana tena na Eric ten Hag, aliyekuwa kocha wao katika klabu ya Ajax na kuisaidia klabu hiyo ya Uholanzi kufika nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya mnamo mwaka 2019 na kushinda mataji matatu ya ligi kuu ya Uholanzi Eredevisie.

Soma pia: Ten Hag arefusha mkataba United

De Ligt alijiunga na Juventus mwaka 2019 kwa dau la pauni milioni £67.5m na baada ya kushinda taji moja la ligi kuu Serie A na kombe la Coppa Italia, alijiunga na Bayern mwaka 2022 kwa dau la £65.6m.

Ameichezea miamba hao wa Ujerumani mechi 73 na kushinda Bundesliga.

Beki wa pembeni wa Bayern Munich Noussair Mazraoui Picha: DeFodi Images/picture alliance

Eric ten Hag anatumai kuwa mabeki hao wawili watapatikana katika mechi ya kwanza ya Manchester United ya ligi kuu ya Premia dhidi ya Fulham uwanjani Old Trafford, mnamo siku ya Ijumaa Agosti 16.

Kuwasili kwa Mazraoui Old Trafford kulihusishwa na kuondoka kwa Aaron Wan Bissaka aliyejiunga na Manchester United akitokea Crystal Palace kwa dau la pauni milioni £50m mwaka 2019.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 26 anatarajiwa kujiunga na Westham United leo Jumatatu Agosti 12. 2024. 

Manchester United pia imerusha ndoano kwa Everton kwa nia ya kumsajili beki Jarrad Branthwaite, japo klabu hiyo imekataa mara mbili maombi ya Mashetani Wekundu. 

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW