Naibu Kansela Sigmar Gabriel ziarani Tehran
4 Oktoba 2016Waziri wa uchumi ambaye pia ni naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel yuko ziarani nchini Iran pamoja na ujumbe mzito ambako analenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na taifa hilo.Ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu Iran ilipoondolewa vikwazo na jumuiya ya Kimataifa kuhusiana na mpango wake wa Nyuklia Ujerumani haitaki kuwachwa nyuma wakati bara la Ulaya,Asia na hasa China zinapojiingiza kwa kasi kuwekeza katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Waziri huyo wa Uchumi wa Ujerumani ambaye pia ni naibu Kansela ameongoza ujumbe mzito wa wakuu wa makampuni ya kibiashara ya Ujerumani zaidi ya 100 lengo likiwa ni kuishawishi Iran kufikia makubaliano ya kibiashara na Ujerumani baada ya hatua ya kutiwa saini makubaliano ya kihistoria ya Nuklia kuifungulia njia nchi hiyo ya kiislamu kuondolewa vikwazo vilivyodumu kwa miaka mingi.Akizungumza na waandishi habari alisisitiza kwamba Ujerumani na Iran zina historia ya muda mrefu katika uhusiano wao wa kibiashara na huu ni wakati mwafaka wa kuuimarisha uhusiano huo.
''Kawaida Iran imekuwa na uhusiano mzuri na Ujerumani.Uhusiano huo haukuimarishwa kutokana bila shaka na mivutano ya kisiasa iliyokuwepo katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita.Iran inahitaji utaalamu wa Technologia wa Ujerumani.Na wakati huohuo katika nchi yao kuna nafasi kubwa ya soko la kiufundi kwa ajili ya utaalamu wa kiviwanda kutoka Ujerumani.Lakini pia tunabidi kutahadharisha kwamba mtu asitarajie itafanyika miujiza.Mafanikio ya kiuchumi hayawezi kupatikana kwa siku moja ikiwa nchi ilikuwa imetengwa na soko la dunia kwa miaka 15 au 20.
Jumatatu (03.10.2016) Kampuni la Siemens la Ujerumani lilisaini makubaliano na Iran ya kuimarisha mtandao wa njia ya reli ya Iran.
Pamoja na hayo ziara ya waziri wa Uchumi Sigmar Gabriel inaelekea kukabiliwa na kizingiti kwa kiasi fulani nchini Iran baada ya spika wa bunge la Iran Ali Larijani kufutilia mbali mazungumzo baina yake na waziri huyo wa Ujerumani Jumanne(04.10.2016)ambaye awali alisisizita juu ya haja ya kufanyika mageuzi katika jamhuri hiyo ya umma wa kiislamu.Larijani ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Iran mwenye msimamo wa wastani kutoka upande wa wahafidhina ni afisa wa ngazi ya juu ambaye alikuwa amepangiwa kukutana na waziri huyo wa uchumi wa Ujerumani na Naibu Kansela Sigmar Gabriel katika ziara yake hiyo ya siku mbili inayolenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara.
Hakuna sababu yoyote iliyotolewa kuelezea juu ya hatua hiyo ya kufutwa kwa mkutano huo ameeleza msemaji wa waziri huyo wa Uchumi.Siku ya Jumatatu Sigmar Gabriel alizungumzia kuhusu haja ya kufanyika mageuzi yaliyoanzishwa na rais Hassan Rouhani akisema kwamba kuwepo kwa serikali mbadala ya iliyopo sasa nchini Iran itakuwa ni kurudisha nchi hiyo katika enzi za mivutano mikubwa iliyokuwepo.Kadhalika aliionya Iran kwamba ili paweko uhusiano wa kawaida na Ujerumani jamhuri hiyo ya kiislamu inabidi ikubali haki ya kuwepo kwa taifa la Israel na kuitolea mwito nchi hiyo ifanye kila iwezalo kutilia msukumo suala la kusitishwa vita nchini Syria,akisema hakuna yoyote nchini Ujerumani anayeweza kuelewa kwanini hospitali zimekuwa zikishambuliwa na raia wakiteseka nchini Syria.
Vikosi vya rais Bashar al Assad vinaungwa mkono na Iran na Urusi wakati vikifanya mashambulizi dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na waasi mjini Aleppo.
Mwandishi:Thurau Jens/Saumu Mwasimba
Source:Tableau DW,Reauters
Mhariri:Daniel Gakuba