1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matukio ya Michezo ya wiki

Charles Hilary10 Machi 2006

Katika michezo juma hili,washabiki wenye tikiti za kombe la dunia la soka kwa mwaka huu sasa rukhsa kuziuza wakipenda,ratiba ya raundi ya pili ya klabu bingwa ya soka barani Afrika yatolewa,mbali na kushutumiwa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani anafikiria kurefusha muda wa mkataba wake baada ya kombe la dunia na,mashindano ya riadha ya ndani mjini Moscow.

Tiketi za Kombe la Dunia.
Tiketi za Kombe la Dunia.Picha: dpa

Tuanze na Kombe la Dunia la soka hapa Ujerumani.Kamati ya Maandalizi ya fainali hizi ya Ujerumani imeeleza wiki kwamba washabiki wa soka wenye tikiti kwa ajili ya kuingia kwenye viwanja wakati wa patashika za kombe hilo,sasa wanaweza kuziuza chini ya utaratibu maalum ama kuzipeleka kwa washabiki wengine.

Utaratibu wa kuuza au kuzitoa tikiti hizo ambazo tayari zimeshanunuliwa,utawezekana kuanzia tarehe 27 mwezi huu tu kupitia tovuti ya FIFA ambayo inasomeka kama fifa.worldcup.com.

Inawezekana kwa watu wa familia moja kupeana tikiti hizo pale itokeapo tukio maalum kama kifo au kuugua kwa mwenye tikiti.

Mwalimu wa timu ya soka ya taifa ya Ujerumani Juergen Klinsman pamoja na kukabiliwa na shutuma nyingi kutokana na timu hiyo kufanya vibaya katika mechi za maandalizi,amesema anafikiria kurefusha mkataba wa kuifundisha timu hiyo baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia.

Klinsman ambaye amewekwa kiti moto baada ya timu ya taifa ya Ujerumani kuzabwa mabao 4-1 na Italia katika mechi ya kujipima nguvu wiki iliyopita,ameshutumiwa na Franz Beckenbauer kwa kurejea nyumbani kwake California badala ya kuhudhuria kongamano linalohusu kombe la dunia lililofanyika mjini Duesseldorf.

Kuhusiana na shutuma hizo Klinsman alisema alikuwa anafahamu kile kitakachokuwemo katika kongamano hilo na ndio maana wakachukua jukumu la kumtuma msaidizi wake Joachim Loew kuhudhuria.

Tangu alipochukua jukumu la kuifundisha timu ya taifa ya Ujerumani mwezi wa Agosti mwaka wa 2004,Klinsman amekuwa mara kwa mara akisafiri kati ya nchi aliyozaliwa ya Ujerumani na nyumbani kwake anakoishi kwa sasa kusini mwa California.

Hata hivyo kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Shirikisho la soka la Ujerumani Hans-Georg Moldenhauer,wapi Klinsman anaishi ndio kitakuwa kigezo muhimu cha kumfikiria kumuongezea mkataba wa kuifundisha timu hiyo ya taifa baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa kombe la dunia.

Wiki hii wapenzi wa soka wa Ujerumani walikuwa katika majonzi mengine baada ya timu za Italia kuzifanyika kitu mbaya timu zao,pale AC Milan ilipoivurumishia mabao 4-1 mabingwa wa soka wa Ujerumani Bayern Munic na timu nyingine ya Ujerumani Werder Bremen kuzabwa mabao 2-1 na Juventus na hivyo kuifanya Ujerumani kutokuwa na timu inayowakilisha katika mashindano ya ligi ya mabingwa.Vipigo hivyo vimetonesha kidonda baada ya wiki iliyopita timu ya taifa ya Italia nayo kuizaba bila huruma timu ya taifa ya Ujerumani mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki.

Kocha wa Bayern Felix Magath alisema wamevunjika moyo baada ya kushindwa kutimiza malengo yao.Magath amesema ligi ya mabingwa ni mashindano makubwa na kutolewa kwao hata hivyo hakutaathiri azma yao ya kufanya vizuri msimu huu.

Bayern ambayo Wajerumani wengi walikuwa wakiipa matumaini ya kufanya vizuri katika mashindano ya Ulaya,ilisafiri hadi San Siro huku ikiwa na kumbukumbu ya kuuchukua ubingwa wa Ulaya mwaka 2001 pale walipowatoa Valencia kwa mikwaju ya penalti.

Nchini Uhispania Waziri wa Michezo wa nchi hiyo Jaime Lissavetsky,ameeleza wiki kwamba nchi yake inaandaa muswada mkali wa sheria utakaopambana na vitendo vya ubaguzi wa rangi michezoni na hasa katika viwanja vya soka.

Amesema serikali yake inakusudia kubadilisha sheria na adhabu kali zitawaangukia watu binafsi wanaojihusisha na vitendo hivyo.Katika siku za karibuni vitendo vya ubaguzi wa rangi katika viwanja vya soka vimekuwa vivikithiri nchini Uhispania,lakini adhabu inayotolewa chini ya sheria za sasa ni ndogo sana.

Mwezi uliopita mshambuliaji wa Barceleona raia wa Cameroon,Samwel Eto’o alitishia kutoka nje ya uwanja wakati wa mechi ya ligi na Real Zaragoza,baada ya kufanyiwa vitendo vya kibaguzi pamoja na kutukanwa na mashabiki wa Zaragoza.Klabu ya Zaragoza ilitozwa faini ya euro 9,000 na Shirikisho la Soka la Uhispania.

Katika mechi za Ligi ya mabingwa zilizofanyika wiki hii zimeshuhudia Arsnel ikiipiga kumbo Real Madrid nje ya mashindano hayo kwa jumla ya bao 1-0 walilofungwa Uhispania wiki mbili zilizopita na kuifanya Madrid kumaliza msimu wa tatu bila taji lolote la maana.Pia Chalsea ya Uingeraza nayo ilitolewa katika patashika hizo na Barcelona ambapo Liverpool ya Uingereza mbali ya kutolewa katika mashindano hayo lakini ilipata mshituko wa aina yake baada ya kushindiliwa mabao 2-0 na Benfica tena nyumbani kwao.

Tukiangalia bara la Afrika wiki hii ratiba ya raundi ya pili ya ligi kuwania ubingwa wa soka kwa vilabu vya bara hilo ilitolewa,ambapo kwa ufupi Tusker ya Kenya itakumbana na Al Ahli ya Misri,FC St Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itamenyana na Coton ya Cameroon huku wenzao wa Daring Motema Pembe watakaribishwa nchini Tunisia kumenyana na CS Sfaxien.

APR ya Rwanda itawakaribisha Royal Armed Forces ya Morocco,wakati Ferroviario ya Msumbji itakuwa na kibarua kigumu pale itakapokumbana na Asante Kotoko ya Ghana.Klabu ya Polisi ya Zanzibar mchezo wa awali katika uwanja wa Amani Zanzibar watapepetana na Etoile sahel ya Tunisia huku ZANACO ya Zambia imepangwa kucheza na JS Kabylie ya Algeria.Stade Malien ya mali itaikaribisha Renaciemento ya Guinea ya Ikweta,kule Dakar Port Autnome ya Senegal itakuwa wenyeji wa USM Alger ya Algeria na ASEC Abidjan ya Ivory Coast itakuwa na mihadi na Civics ya Namibia mjini Abidjan wakati kule Port Louis timu ya AS Port Louis ya Mauritius itamenyana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Nao Enugu Rangers ya Nigeria imepangwa kuanza na Al Hilal ya Sudan mjini Enugu,wakati Diaraf ya Senegal itawakaribisha Enyimba ya Nigeria.

Timu ya USCAFOOT ya Madagascar itakuwa na kibarua kigumu mjini Antananarivo watakapoanza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini,wakati mjini Addis Ababa timu ya St George itawakaribisha Hearts of Oak ya Ghana na Raja Casablanca ya Morocco watawapa nafasi CAPS United ya Zimbabwe.

Mechi za awali zitaanza kuchezwa kuanzia Machi 17-19 na zile za marudiano zitachezwa baina ya tarehe 31 Machi na kati ya Aprili 1-2.

Katika riadha binadamu anayeaminika ndie mwenye kasi ya kukimbia kuliko wote kwa sasa Asafa Powell alionesha wiki kwamba yupo tayari kwa ajili ya mashindano ya Madola ya Melbourne baada ya kupata ushindi rahisi.

Mjamaica huyo anayeshikilia rekodi ya mbio fupi za mita 100 duniani,alikimbia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi saba iliyopita kwa kutumia sekunde 10.29 katika mbio za ziara ya dunia zilizofanyika uwanja wa Olympiki Park.Rekodi yake ya dunia anayoishikilia ni ya sekunde 9.77 aliyoiweka Athens mwezi wa Juni.

Na katika mashindano ya ndani dunia ya riadha ya Moscow,bingwa wa mbio za mita 100 kwa wanawake Mmarekani Lauryn Williams,jana alilalamika kwamba mlio wa bunduki inayoanzisha mbio,ulikuwa ni wa kimya saana lakini hata hivyo aliweza kushinda mbio za mita 60.Williamsa alisema kwamba awali alisita kuchomoka kwa vile hakuweza kusikia mlio wa bunduki kuashiria waanze kutimka.

Mwanariadha wa Ufaransa Christine Arron,alikimbia kwa muda wa kasi katika raundi ya kwanza wa sekende 7.16,lakini nae ameelezea kusikitishwa kwake na mlio wa bunduki wa kuashiria kunza mbio.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW