1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurundi

Matumaini mapya ya kupatikana haki kwa mauaji ya Gatumba

15 Agosti 2024

Human Rights Watch yasema kwenye ripoti yake kwamba kuna matumaini mapya ya kupatikana haki baada ya waathiriwa wa mashambulio kwenye kambi ya wakimbizi ya Gatumba nchini Burundi kufungua kesi kwenye mahakama ya jinai.

Burundi Refugees Flüchtlingscamp
Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP via Getty Images

Walionusurika pamoja na ndugu wa waathiriwa wa shambulio la mwaka 2004 katika kambi ya wakimbizi ya Gatumba nchini Burundi wamefungua kesi dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu katika nchi zao za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Madai yao yanajumuisha mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika juhudi za kutafuta haki baada ya uhalifu waliotendewa miongo miwili iliyopita. Wakili anayehusika katika kesi hizo amesema taarifa hii imewasilishwa pia kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ya mjini The Hague.

Naibu Mkurugenzi wa Shrika la Human Rights Watch kanda ya Afrika, Laetitia BaderPicha: Human Rights Watch

Amesema malalamiko hayo mapya yanawahusisha pakubwa viongozi wawili wa FNL, Agathon Rwasa na aliyekuwa msemaji wa kundi hilo Pasteur Habimana.

Soma Pia:  Ndayishimiye: Burundi bado inao maadui licha ya utulivu

Mnamo Agosti 13, mwaka 2004, Jeshi la Ukombozi wa Taifa nchini Burundi (FNL) ambalo ni kundi la zamani la waasi, liliwalenga zaidi wakimbizi wa Banyamulenge, Watutsi wa Kongo kutoka jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kambi ya Gatumba, iliyoko karibu na mpaka kati ya Burundi na Kongo.

Zaidi ya raia 150 waliuawa na wengine 106 walijeruhiwa. Wakimbizi hao walikuwa wamekimbia mapigano yanchini Kongo. Kundi la waasi la FNL ambalo wengi wao ni Wahutu wa Burundi, liliwaua kwa kuwafyatulia risasi au kwa kuwachoma moto wakimbizi wa Banyamulenge, huku wakiwaacha wakimbizi wa makabila mengine na Warundi waliokuwa wakiishi katika kambi hiyo.

Soma Pia:  Rais wa zamani wa Burundi azikwa Rutovu baada ya mwili wake kurejeshwa Burundi

Utafiti wa shirika la Human Rights Watch, wakati huo ulibaini kwamba wanajeshi wa Burundi hawakuingilia kati, ingawa mauaji hayo yalifanyika umbali wa mita chache kutoka kwenye kambi za kijeshi.

Agathon Rwasa, kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini BurundiPicha: Antéditeste Niragira/DW

Utafiti huo pia ulibaini kuwa wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa hawakuweza kuwalinda wakimbizi hao kwa sababu walifahamu tu juu ya mashambulizi hayo yalipomalizika.

FNL, ilithibitisha kuhusika na mashambulio hayo yaliosababisha mauaji ya raia. hata hivyo, miaka kadhaa baadaye, aliyekuwa msemaji wa kundi hilo wakati huo, Pasteur Habimana, alikanusha kwamba FNL ilitoa kauli hiyo.

Mnamo mwaka 2009, kikundi hicho cha waasi wa FNL kiliweka silaha zao chini na kubaki kuwa chama cha kisiasa, hatua iliyoashiria mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Soma Pia:  Rwanda yakanusha madai ya Burundi kuwapa silaha waasi

Mnamo mwaka 2004, mamlaka ya Burundi ilitoa hati za kukamatwa kwa viongozi hao wawili wa FNL, Agathon Rwasa, kiongozi mashuhuri wa upinzani na Pasteur Habimana. Hata hivyo Rwasa, hakuwahi kukamatwa.

Mnamo Septemba 2013, mahakama ilitangaza kufunguliwa kwa kesi dhidi ya Rwasa ya madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa katika kambi ya wakimbizi ya Gatumba, lakini kesi hizo zilicheleweshwa kwa muda usiojulikana.

Jengo ilipo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC mjini The Hague, UbelgijiPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Shirika la Human Rights Watch limesema licha ya kucheleweshwa kesi hizo kwa miaka mingi hatua ya sasa ya kuwafungulia mashtaka waliohusika na mauaji hayo ya kutisha, ni hatua ambayo itasaidia kuwapa ahueni ndugu na jamaa walioathiriwa na mauaji hayo na pia hatua hiyo inaonyesha kwamba haki inaweza kupatikana ili kujibu ukatili mbaya zaidi uliowahi kutokea kwenye eneo la Maziwa Makuu.

Chanzo: https://www.hrw.org/news/2024/08/14/renewed-hope-justice-burundi-massacre

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW